The Chant of Savant

Wednesday 14 March 2018

Kijiwe chaadhimisha siku ya wanawake duniani kinamna

             Wiki iliyopita ilikuwa ni siku ya akina mama duniani. Hivyo, kijiwe hakikubaki nyuma. Kwani, nani hana bibi, dada, mama au shangazi ndipo asiwajali wala kuwasaidia akina mama popote walipo? Hata mitume walikuwa na.? Kwa kuzingatia hili, wanakijiwe–wa vile ni magwiji wa haki za binadamu na usawa–hawakubaki nyuma. Baada ya kuamkuana tulikubaliana; kila mmoja aelezee alivyosherekea siku hii adhimu.
 Tukiwa hatuna hili wala lile, Mgoshi Machungi wa Shekiango ndiye anaanzisha mada. Anakunywa kahawa yake na kuronga huku akitabasamu kwa mbwembwe na bashasha “mwenzenu kwenye siku ya akina mama niimsaidia bi mkubwa kupeeka kitegemezi zahanati kue Mashindei Ushoto. Niipofika kue niipigiwa vigeegee kwa sana na akina mama waiokuwa wamepeeka vitegemezi vyao kucheki afya zao.”
Mijjinga alipoka mic na kuchekesha kijiwe. Alisema “mimi tokana na mapenzi makubwa kwa bi mkubwa wangu, siku hiyo, niliamua kwenda kisimani kuchota maji. Acha maji yanimwagikie ukiachia mbali kushindwa kubalance ndoo ya maji kichwani.”
Mbwamwitu anamchomekea “usemayo kweli au unataka kuchekesha kijiwe? Haya mahaba yameanza lini; hebu tujuze tukuelewe.”
Mijjinga alijibu “nidanganye nini wakati hicho ndicho nilichofanya? Unanishangaa mimi kubeba ndoo ya maji kichwani? Mbona humshangai yule waziri mdogo wa maji aliyetundika ndoo kichwani tena si kwa ajili ya bi mkubwa wake bali kwa ajili ya kuzindua kijimradi kidogo cha maji kule Mji Kasoro Bahari?”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea “nasikia kule UG M7 alisherehekea sikukuu ya akina mama kwa kumwacha bi mkubwa wake atawale tokea bedroom.”
Kijiwe kinacheka na kuvunja mbavu juu ya usanii huu wa kisiasa. “Nani anataka waziri anayebeba ndoo? Tunataka waziri anayeleta maji kwenye mabomba siyo visima” anachomekea Kapende.
Mpemba naye hakutaka kuachwa nyuma. Anakwapua mic na kuronga ‘wallahi mie hiyo siku nlimpikia bi Nkubwa pilau ya kukata na wembe. Hata hivyo nilipatikana hasa ikizingatiwa twatumia jiko la nkaa. Huo moshi ulivoniumiza matoni wala sina nfano.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anamkonyeza Gau Ngumi aka Linungaembe. Leo Sofia kaupara kama hana akili nzuri! Baada ya kumaliza kukonyezana na mwenzio da Sofia anasarandia mic na kunena “kijiwe cha leo cha kihistoria. Kwani, inapendeza kwa baba kumsaidia mama hata kama ni mara moja kwa mwaka. Mie ningeshauri huu moto wa mahaba mliowasha wala msiuzime. Endeleeni kuwasaidia wake zenu japo mjifunze na kujua masahibu yao. Au vipi kaka zangu?’
Kanji kuona hivyo naye anaamua kuonyesha mapenzi ya kigabachori. Anakula mic “mini kosaidieni mama kwenda dukani ya maua nanunulia yeye maua.”
“Halo halo! Veve Kanji hiyo kazi nafanya iko dogo sana. Mimi ile siku iko nabeba toto na kubembeleze yenyeve hadi bi kuba nafurahi sana kwa moyo, mwili na roho. Kwani hiyo bibi yako iko zungu au mbuzi hadi naleta majani kwa yeye?” anachomekea Mchunguliaji.
Bwana mdogo Mchunguliaji kama ni mashindano naona hunifikii mimi. Kwani, nilitandika kitanda na kumbeba bi Mkubwa hadi nikamlaza salama salimini kwa furaha na maraha.”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa kimya anaamua kutia guu “mwenzenu mie sikumsaidia mke wangu. Huwa sipendi lugha hii tamu ya kusaidia. Nilichofanya ni kuwajibika kwangu kwake. Hata hivyo, siku hii adhimu nilikuwa na kibarua cha kumfanyia homework yake. Mwenzenu shemeji yenu anasomea shahada yake ha upili kwenye Uongozi na Utawala Bora. Japo huwa nawajibika kwa kufanya mambo mengi ambayo wengi wanaonekana wameyafanya. Sidhani kama tutakuwa wa kweli kuwasaidia wenzetu siku moja kwa mwaka ni jambo la kujivunia.”
Kabla ya kumalizia tunaangaliana kwa aibu na mstuko namna Msomi anavyotusuta.
Kabla ya aibu ya kusutwa kuzama si Mipawa akaja na mpya ambaye ilitusahaulisha yote! Bila kuonyesha chembe ya woga wala shaka anasema “kama kuwasaidia washirika zetu wa bedroom ni kukvunja rekodi basi mie ndiyo nimeweka rekodi mpya. Kwani, pamoja na kumfanyia mambo yote mengi ambayo sina haja kutaja, cha mno nilimsukaga nywele akapendeza hadi nikahisi wivu usipime. Alipowaambia mashoga zake kuwa mie ndiye niliyekuwa nimemsuka walishangaa sana hadi wakamshauri tufungue saluni nikagoma.”
Wakati tukiwa tunakenua si Mzee Maneno akatoa mpya. Alisema “mwenzenu mie nilideki nyumba na kuhakikisha kuwa najazia maji kwenye mboga.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchokoza “ulivaa na gagulo siyo?” kabla ya kuendelea sim zee Maneno akaamka na kutaka kumtia mikono! Huku akiwa amechukia aliuliza “je baba yako huwa analivaa hilo gagulo unaloona la maana sana siyo? Koma na ukomae na ushike adabu ikushike kabla sijakushikisha adabu. Wewe ni wa kuniambia kuwa nilivaa gagulo? Mimi siyo saizi yako. Kama utani mali basi naweza kutaniana na baba yako au mama yako.”
Huku tukiwa hatukutegemea, mzee Maneno anaamka kutaka kumshikisha adabu kweli Mbwamwitu ambaye bila kukawia anaamka na kutoka mkuku huku tukibaki tukiwa tumeghubikwa na taharuki tusijue la kufanya!
Kapende anahanikiza na kusema “siku ya akina mama hoyee!”

Je wewe umesherehekeaje?
Chanzo: Tanzania Daima leo Machi 14, 2018.

No comments: