The Chant of Savant

Tuesday 12 September 2017

Zetu ni Uhamiaji au uhamishaji, biashara au bi hasara?

      Image result for photos of wachina morogoro      Taarifa kuwa kuna wachina walikamatwa wakiendesha kiwanda bila kibali nchini kwa tangu mwaka 2010 huko Morogoro ni za kuchefua na kuchukiza. Sikujua kuwa nchi yetu itafikia hapa kiasi cha kuibiwa kana kwamba ni nchi ya mataahira au marehemu kiakili. Tokana na kadhia hii, kuna maswali tunayopaswa kujiuliza kama taifa na watu wenye akili mojawapo yakiwa: Je uhamiaji hakikuwa na taarifa au walikatiwa kitu? Je kuna wachimbaji wa kigeni wangapi nchini? Je mchezo huu ulianza lini?  Pia visa vya wachina kukamatwa ima wakichimba madini au kufanya kazi na kuishi bila vibali au kutorosha nyara za umma na madini vimezidi nchini. Sijui wako wahindi, wapakistani, waturuki, wanigeria na wengine wangapi wanaofanya mambo kama haya nchini wakati wananchi wetu wakishuhudia au kuripoti mamlaka zisichukue hatua?
            Ukiachia mbali uhamiaji, ilikuwaje wizara ya madini haikujua au nao wana ushirika katika kuliibia taifa kwa kufumbia macho wezi kama hawa ili mradi wanapata chao?  Japo ni mapema kutoa lawama, kuna uwezekano huu ni mchezo wa baadhi ya maafisa wa juu nchini. Maaana, hakuna kilichonishangaza kama kusikia kuwa wachina hao waliokutwa wakihujumu nchi walikuwa wapelekwe Dar es Salaam ili warudishwe kwao. Warudishwe kwao wakasherehekee kuwaibia mataahira siyo? Kwanini warejeshwe kwao wakati wanakabiliwa na mashitaka lukuki yakiwemo ya kuhujumu uchumi na kutishia usalama wa taifa kwa kuingia na kuishi na kufanya kazi kinyemela? Je hawa wanaotaka kuwarejesha kwao kweli hawajui sheria au kuna kitu wanataka kuficha. Haiwezekani mtu avunje sheria ya nchi hata kama ni mgeni aondolewe nchini bila kuhukumiwa na mahakama nchi ikawa salama.  Hata mhalifu kama huyu akikamatwa na chizi, achia mbali mtu mwenye akili timamu, atamsulubu. Hata akikamatwa na mbwa, hataaacha lau kumng’ata kwa kujua na kutambu aanavyomhujumu. La msingi, mafisadi na wasaliti wanaokula na wahalifu hawa, ni kujua kuwa wakati wakiwaachia wachina hawa au wahalifu wa mataifa mengine, kuna vijana wengi wa kitanzania wanaozea kwenye magereza ya nchi mbali mbali hasa China wakingoja kunyongwa kwa kupatikana na hatia za kusafirisha madawa ya kulevya. Hawa nao ni watafutaji sawa na hawa wachina hata kama wanafanya uhalifu tofauti. Nadhani hapa tofauti yao ni kwamba hawa wanauza unga na hawa wanaiba raslimali za nchi. Hivi watanzania tulirogwa na nani na kuwa na roho mbaya hivi itokanayo na ujinga, upogo, ulafi na ubinafsi? Tunachezea raslimali zetu kana kwamba tutaishi milele. Hivi mababu zetu wangekuwa wapumbavu hivi tungekuta nini zaidi ya mashimo na mabwana wa kutugeuza watumwa?  Mamlaka zinazohusika na kupambana na rusha na ufisadi, zifuatilie kisa hiki zinaweza kugundua vingi na mengi hasa wakati huu ambapo jinai ya kushirikiana na wageni kuibia taifa inazidi kuwa kidonda ndugu.
            Mbali na wizara ya madini, ilikuwaje wizara ya biashara na viwanda nayo haikufahamu kama hakuna mchezo mchafu hapa?  Maana, ushahidi kuwa kuna mchezo mchafu, ni maneno ya Afisa mmoja wa madini aliyelalamika kuwa aliwahi kushughulikia sakata hili akasimamishwa kazi. Je wako wezi kama hawa wangapi nchini na wameishaliingizia taifa hasara kiasi gani? Je wapo watendaji wangapi wa serikali wako nyuma ya hujuma hii na kwa muda gani? Haiingii akilini eti kwa nchi yenye vyombo vyote vya usalama isiwe na taarifa za watu tena kutoka mbali kama China wenye rangi tofauti kwa miaka yote hii. Kama ni hivi basi Tanzania ni nchi ya ajabu na usalama wake uko hatarini.
            Pamoja na kwamba kwa sasa China inaonekana kama mwekezaji mkubwa nchini, tunapaswa kuwa makini. Kwani haina tofauti na nchi za magharibi zilizotutawala na kutunyonya kwa muda mrefu kabla ya mababu zetu kujitoa mhanga kupigania uhuru. Tofauti na nchi za magharibi zilizokuwa zikituma vikundi vichache vya mawakala wao kama vile wamisionari, wafanyabiashara, wavumbuzi na watawala, wachina wanatutumia watu wao wasio na ajira kuja kuchukua ajira za watu wetu ukiachia mbali kujiingiza kwenye shughuli za jinai baada ya kubaini kuwa baadhi ya watendaji wetu ni walafi na wapumbavu wasio na mapenzi na taifa lao. Huu upuuzi unaoripotiwa kila siku huwezi kuutenda China ukaachiwa uende kwenu. Watakupiga risasi. Ni bahati mbaya kuwa kosa la kuhujumu uchumi au ufisadi nchini linafanyiwa mchezo tokana na kuhusisha wakubwa wengi. Kule China wanapiga risasi bila kujali wewe ni rais, raia au mgeni.
            Tumalizie kwa kuzitaka mamlaka kuchunguza aina hii ya ufisadi na uhujumu kwa taifa. Pia tunashauri zitungwe sheria kali za kupambana na wezi hawa pamoja na washitili wao. Mbali na hilo, kuna haja ya kuelimisha wananchi wetu kuwa macho na mali zao. Maana hazitaishi milele. Pia haina sababu wao waendelee kuishi kwenye umaskini wa kunuka wakati wageni wanakuja na kujichotea watakavyo.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.

No comments: