The Chant of Savant

Saturday 15 July 2017

Barua ya wazi kwa wanufaika wa Escrew

Image result for photos of chenge, ngeleja, tibaijuka kilainiImage result for photos of wahongwaji wa escrow
            Baada ya juzi kumshuhudia mnufaika mmoja wa mamilioni na mabilioni ya Escrew, ile kashfa ambapo baadhi ya matapeli wa ndani na nje na baadhi ya wanene kwenye lisirikali walipiga njuluku za walevi, nimeamua kuwatahadharisha wale wanaodhani wataendelea kufwaidi zile njuluku zs walevi wakati walevi wakiendelea kunyotolewa roho na mikasa itokanayo na umaskini unaosababishwa na udokozi na wizi wao. Hii ni baada ya walevi kunituma nifanye hivyo kabla hawajakwenda wenyewe kugawana kila kitu wajalaana hawa wanachomilki bila kujali kuwa kinatokana na mshiko huu au mishemishe mingine. Kwa wasiojua inshu ni kwamba jamaa mmoja aitwaye Jimmy Rugetumbuliwa aka Rugemalayer aliyeshirikiana na wanene wetu majizi kuanzisha kampuni feki iitwayo IpTL, aliamua kuchafua hewa. Si alitembeza mshiko kinomi kiasi cha kuhonga kila aliyesimama mbele yake ilmradi dili lake lipite.
            Katika wale waliohongwa njuluku hizi za walevi ni Bill Ngereza aliyeamua kuzitema juzi baada ya kuona joto la Dokta Kanywaji likizidi kupanda huku akitaka majipu yajitumbue kabla hajayapasulia mbali bila kujali yameota kwa vifito au vigogo. Kwa kufanya hivyo, Bill ameanzisha ngwe nyingine ya kuona wenzake wakizitapika njuluku zetu ili tuzitumie lau kupata kanywaji na huduma nyingine kama jamii.
            Rugetumbuliwa mfano, anadaiwa kuwahonga jamaa mmoja aitwaye Endelea Chenga aliyekuwa mwanasharia mkubwa wa lisirikali zamani kiasi cha madufu 1.6 bilioni sambamba na aliyekuwa waziri mmoja wa mambo ya mahekalu mwenye cheo cha profwedheha aitwaye Annae Kajuamlo kiasi hicho hicho. Jamaa hakuishia hapo, alihonga majaji, makasisi, makuhani hata wafagiaji kutegemea na thamani ya muhongwaji. Wapo walioambulia vijesenti kidogo vya kununulia mboga toka kwa jamaa huyu aliyewahi kusema kuwa mamilioni na mabilioni aliyokuwa akihonga vilikuwa ni vijisenti vya ugolo.
            Hivyo, wahongwaji wote walionekana kushabikia ugolo kiasi cha kuhitaji msaada wa jamaa huyu mchafu kama nguruwe ambaye kwa sasa yuko lupango akingojea kulipia madhambi na udokozi wake. Tokana na ukweli kuwa business as usual era is long gone, natawatahadharisha wote waliopokea mamilioni na mabilioni haya kurejesha mara moja huku wakijipeleka wenyewe lupango kabla ya kuzolewa mzobemzobe na kurundikwa kwenye karandinga na magereza. Tena nitamshauri mnene awafungulie kesi za makosa ya mauaji kutokana kuwa ujambazi huu umeishaua walevi wengi waliokosa huduma muhimu kama madawa, elimu na hata kufaidi maisha kwa ujumla.
            Tukijrejea kwa wapendwa wahongwaji, napenda kumpongeza mwenzao aitwaye Bill aliyeamua kutema vijisenti vya ugolo. Inaonekana jamaa kaachana na tabia ya kunusu au kubwia ugolo.  Je marafiki zangu mnaojijua mnangoja nini au hadi kinukishwe ndipo msituke baada ya kujikuta lupango? Pia nawafahamisha; kurejesha njuluku siyo mwisho wa stori. Huu siyo wakati wa EPA ambapo mkuu wa kashfa hii aliwashauri wenzake warejeshe halafu akawasamehe utadhani yeye ni mahakama.  Tunajua kuwa jamaa huyu aitwaye Njaakaya alifanya hivyo ili kuficha asiumbuke pamoja na wenzake wa karibu waliopunyua njuluku hizi na kuzitumia kujipatia ulaji kisiasa. Kwani hatujui? Mbona mauzauza na ujambazi huu ulianikwa na mwanasheria aitwaye Bhindika aliyesaini uhamishaji wa njuluku za EPA?  Tena nichukua fursa hii kumkumbusha Munene atumbue na kufumua kashfa hii bila kumbakiza kiongozi wa ujambazi huu aliyeitwa Kagoda aka Roast Tamu la Aziz. Akimaliza hii aende pake UdA kampuni la walevi lililotwaliwa kijambazi na jamaa mmoja ajiitaye Saimo ambaye hivi karibuni alikabidhiwa mradi mwingine mkali utokanao na njuluku za walevi wa DrT akajitwalie kama alivyofanya kwa UdA.
            Nikirejea kwa wanufaika wa Escrew, mjue fika. Chini ya utawala wa sasa, rejesheni–na kuonyesha wazi mlivyo mafisadi–halafu mjiandae kwenda lupango kunonihino kwenye mtondoo. Chini ya kanuni hii ambayo kilevi huitwa self-tumbualing, yaani majibu kujitumbua yenyewe, wengi walionufaika na ujambazi huu watakwenda kuimba kwaya na bosi yao Jimmy aliyewahonga kule korokoroni. Inapendeza siyo?
            Ngoma haiishii hapa. Lazima akina Bill na wenzake warejeshe njuluku zetu na interest juu. Maana walikaa nazo na kuzitumia kutengeneza utajiri kinyume cha sheria. Kwa wale ambao wako kwenye ofisi za umma, kuanzia siasa, dini na magumbashi yoyote waachie ngazi kwanza ndipo wapelekwe lupango. Kwa wale ambao wameisharudisha namba, nitamuomba Mungu awaadhibu huko huko tena kwa nyongeza ya mateso. Natamani kumuona mzee wa Vijisenti akimfuata mzee wa Vijisenti vya Ugolo ili wakaimbe kwaya pamoja tena kwa kigabacholi huku choir leader akiwa Singasinga. Wakimaliza waimbe nyimbo za kinshomile, kisukusi na nyingine nyingi tokana na watokako wapunyuaji hawa aka mijizi kama alivyowahi kuwaita mhishimiwa Tundu Jissu sometimes back kwenye mjengo alipotaka wakamatwe mara moja. Kiko wapi sasa. Sijui wale waliokuwa wakiwatukana wenzao kuwa ni tumbili ni nani tumbili sasa? Mtaisoma namba zamu hii. Au siyo? Bring back our escrew dosh as soon as possible. Loo! Kumbe vitu vimepanda hadi ninaongea kimakonde! Tuonane wiki ijayo basi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: