The Chant of Savant

Friday 16 June 2017

Kashfa ya IpTL: Barua ya wazi kwa EWuuRA

        Baaada ya kuchacha kiasi cha kukosa njuluku ya kupatia ulabu, niliamua kujisomea magazeti lau nijue umbea wa mjini; na nikakutana na kiroja cha mwaka! Guess what. Eti vilaza wetu wa mamlaka ya ulaji angani, nchi kavu na majini walioruhusu ujambazi wa IpTL wanatutaka tutoe maoni juu ya kuendelea kuhalalisha ujambazi huu. Mnakumbuka shuka asubuhi siyo? Mbona mlipoingia huu ujambazi hamkutaka maoni yetu; au mnataka mpate kisingizio cha kusema kuwa tulishirikishwa kubariki ujambazi huu? Mshindwe na kulegea. Kwanini kutangaza kwenye magazeti binafsi na si govt gazette?
            Kwa vile mmejivua nguo wenyewe, acha niwape ya moyoni kama ifuatavyo:
Kwanza, IpTL si kampuni sawa na makampuni mengine. Hivyo, haipaswi kufikiriwa wala kufaidi haki sawa na makampuni mengine yasiyotupiga kama wao. Hivyo, kama mnatafuta sababu ya kutushirikisha kwenye uchafu wenu, mkome.
Pili, kabla ya kutaka maoni yetu, mnapaswa kutueleza ni kwanini mliingia ujambazi huu; na nani walihalalisha hii jinai; walipata nini na kiasi gani kwa sheria ipi? Kwanini sasa; na si huko nyuma mliponyea na kuivuja sheria kiasi cha kuigeuza kaya kichwa cha mwendawazimu aka shamba la chizi?
Tatu, muweke wazi mikataba yenu na majambazi haya ili tujue kuna nini; na tunaongelea na kuchangia nini badala ya kutuuzia nguruwe kwenye gunia. Kumbaff.
Nne, mtupe uhakikisho kuwa hamna nia mbaya nasi na kaya yetu kama ambavyo mmekuwa mikifanya ili kujipatia njuluku za haraka wakati mkiendelea kutupandishia bei ya umeme. Mnadhani hatujui kinachoendelea?
Tano, muwachukulie hatua wote walioshiriki kuingiza kaya kwenye balaa hili la kiuchumi. Kama hamuwajui, ngoja niwatajie makuwadi wao. Yupo Jimmy Rugemalayer ambaye anasifika kuwahonga walafi kuanzia mawaziri, wabunge, viongozi wa kiroho wenye uroho hata majaji. Pili, yupo gabacholi Singasinga anayeishi Kenya ambaye aliibuliwa na majambazi wetu wa ndani ili kuficha uchafu wao.
Sita, mtwambia chanzo cha upendo na uwazi huu ambavyo havikuwapo hapo mwanzo mlipofunga ndoa hii haramu ya kuangamiza kaya na walevi wake.
Saba, mtuhakikishie kuwa walioingia mikataba hii hatari hamtawaita makaburi na kushindwa kuwafukua kwa kuhofia kushindwa kuwafukia kama alivyowahi kusema dingi ambaye ameonyesha wazi kuwagwaya hawa jamaa kana kwamba ana faida nao. Haiwezekani mkaendelea kutugeuza hamnazo huku mkitusanifu kuwa mnataka maoni yetu wakati mlipoingia kitandani kufanya ufuska huu wa kiuchumi tulipiga kelele mkatupuuza. Tutaamini vipi kama hamtatupuuza wakati huu. Kimsingi, kama mnataka mawazo nenda kwa akina Bashite wanaosikika na kusifika. Huenda watapata fursa hii kuanzisha sinema nyingine ili kuendelea kuwa madarakani wakati wana vyeti feki na wanatumia majina feki.
Tukiachia mbali hawa vidagaa tuliowatajia hapo juu, je mko tayari kuweka wazi majina ya marais na mawaziri walioshiriki kusuka dili hili hadi likazaa jingine liitwalo EPA ambalo lilisababisha hasara ya mabilioni kwa kaya? Je mko tayari kuwaumbua waliotumia njuluku za EPA kuukwaa ulaji huku wakituache tuendelee kuliwa mbele na nyuma? Je hapa mnataka kumsanifu nani; na kwanini mnaendelea kututia madole machoni?
Guess what. Nimeamua kugusia kashfa hizi ili kuwaumbua Eula kuonyesha mnavyotaka kuendelea kuula wakati sisi tukiliwa. Mbona hamuongelei njuluku ya rada ambayo wakoloni kwa kiingereza walitaka kuwarejeshea mkakataa? Mbona  hamkumbushii kukataa kwenda Uswizini kupewa njuluku nyingi tu ambazo majambazi wetu wakubwa, mibaka na mipapa imeficha kule? Mbona hamuongelei kubadili sheria kuhusiana na kashfa kama ya IpTL?
Kwa uzembe wenu mmekatiwa kitu kidogo na kikubwa mkalegea na kuachia kila kitu; halafu mnaanza kujishaua kuwa mnatafuta maoni. Nenda mkamuulize Kafulia aliyeibua na kuvalia njuga sakata hili hadi mkamtosa mjengoni. Kwani hatujui? Katika kufanya utafiti wangu juu ya kashfa hii niligundua kuwa kumbe IpTL inaweza kuwa Independent Protectorated Tanzia Ltd ambayo inalindwa na sirikali kama siyo sirikali ndani ya sirikali tena inayofanywa kuwa siri kali.
Nimalizie kwa kutoa maoni yangu na ya walevi ninaowangoza kama ifuatavyo:
Mosi, wanyonge wote walioguswa na kashfa hii bila kujali vyeo wala sura zao au ubashite wao.
Pili, taifisheni mitambo ya IpTL kutokana na ukweli kuwa ni mali ya walevi ambayo imekuwa ikitumiwa kuwalangua umeme na kuwaibia.
Tatu, taifa mimali ya wale wote waliohusika kwenye ufuska huu wa kiuchumi ndipo mje tuongee; na tuwafundishe jinsi ya kusimamia mali za umma. Itoshe kusema; walevi wamechoka kutiwa vidole na kugeuzwa samaki ambaye hukaangwa kwa kugeuzwa geuzwa kwa vile yu mfu.
Leo hii tosha. Ngoja nikapige kanywaji tayari kuwatolea uvivu zaidi pale itakapobidi. Kwanini msiunde tume huru kama ya makanikia yatokanayo na ukosefu wa umakini?
Chanzo: Nipashe Jumamosi kesho.

No comments: