The Chant of Savant

Wednesday 28 June 2017

Byakanwa alitumwa au anajikomba tu?

Image result for photos of byakanwa
Shamba la Freeman Mbowe  baada ya kuharibiwa 
Image result for photos of byakanwa
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Byakanwa akiharibu shamba la Freeman Mbowe.
Niliwahi kuandika makala kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wanaonekana kama wakoloni wanaotumwa kwenye mikoa na wilaya hasa wale wanaosifika kuwanyanya wananchi. Japo si wote, baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya–hasa wale ambao ima wamelewa madaraka, hawajui madaraka yao au hawafai au wanatukana madaraka na ofisi za umma–wamegeuka wakoloni kwenye maeneo yao ya kazi kiasi cha kuzusha hisia kuwa baadhi ya sehemu za nchi yetu hazijapata uhuru; na kama zimepata uhuru, basi haujakamilika. Malimbukeni hawa, ambao kweli ni wakoloni, wamefikia pabaya kiasi cha kukera na kugeuka kikwazo na hatari kwa maendeleo taifa. Wapo ambao walifikia hata kulitukana na kulidhalilisha bunge ukiachia mbali ambao wamejigeuza miungu watu wasijue miaka mitano si mingi. Wengi wanasahau kuwa cheo ni dhamana. Kosa kubwa sana. Zamani wateule wengi kwenye ngazi hizi walikuwa ni watu wenye mashiko na historia zinazojulikana lakini si wa kuzua na kuibua wakaishia kuonyesha uhovyo wao kama ilivyo kwa baadhi ya wateule hawa.
Leo tatajadili na kulaani hujuma iliyotokea Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro. Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuharibiwa na kuhujumiwa shamba la Mbunge wa Hai (CHADEMA) Freeman Mbowe kulikosimamiwa na kutekelezwa na mkuu wa wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa. Kitendo hiki cha ajabu na cha kizamani, licha ya kustua na kusikitisha wengi, kinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote. Kwani licha ya kuwa cha hatari, kichukuliwe sawa na jinai yoyote; aliyeiamuru na kuisimamia afikishwe kwenye vyombo vya dola baada ya wananchi wa Hai na Kilimanjaro kwa ujumla na kule atakapohamishiwa washinikize awajibishwe; ili uwe mfano kwa wengine wenye kulewa madaraka.
Sijui huyu alipoamua kutekeleza hujuma hii kama alijiuliza kama shamba lingekuwa lake angefanya nini? kama Byakanwa ana shamba basi atakuwa amefanya alichofanya kwa ubinafsi wa ajabu zinazolenga kufanikisha uchu wake wa madaraka kisiasa. Au ni yale ya mkuki kwa nguruwe.
Hata hivyo, hujuma ya Byakanwa imetoa somo kuwa kuna wateule wanaotumia madaraka vibaya kiasi cha kuharibu mali za wenzao. Sijui rais John Magufuli kama atamvumilia uharibifu huu wa mali hasa ikizingatiwa alivyowahi kuingilia kupiga marufuku kubughudhi wamachinga vinginevyo. Ajabu wakati kuna madai ya kutokuwapo na chakula cha kutosha, wapo wanaoharibu chakula! Tunakaribisha wawekezaji wakati tukihujumu waliokwishawekeza kama ilivyotokea kwa Mbowe.
Byakanwa ashitakiwa kama mtu binafsi au Mbowe afunguwe kesi mbili tofauti moja dhidi ya Byakanwa na nyingine dhidi ya serikali. Hakuna kinachoshangaza kama suala hili kuonekana kuwa la kisiasa zaidi ya kisheria. Maana, hata baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani kulaani kitendo hiki, wenzao wa chama tawala hawakufanya hivyo. Kuna nini hapa?
Japo Magufuli amekuwa akipenda kuwabeba wateule wake wanaolalamikiwa, akina Byakanwa hawamsaidii. Hawajui dhima, mipaka na dhima ya madaraka yao. Unaweza kusema wamelewa madaraka au hawajui hata hicho wanachofanya. Tangu lini mkuu wa wilaya akageuka mgambo wa tume ya mazingira? Je ametumwa, amejituma, anajipendekeza au ana ugomvi na Mbowe? Je alifanyiwa vetting kweli huyu ambaye hajui hata sera za bosi wake kuwa ni kukuza uchumi?
Imekuwa bahati mbaya. Siku hizi hatupewi historia na habari tosha juu ya wateule wetu kama ilivyokuwa wakati wa awamu ya kwanza ambapo mteule yoyote alipoteuliwa ilikuwa lazima kuelezea historia yake ili umma umjue na kuweza kumkubali au kuistua serikali kuwa ni bomu. Kwa mfano, hatujui elimu wala afya ya kiakili ya mhusika katika sakata hili ambalo kwa watu wenye akili linashangaza kiasi cha kujenga shaka juu ya akili husika.
Byakanwa alikaririwa akisema kuwa shamba alilohujumu lilikuwa linachafua mazingira. Kituko. Kwani lilianzishwa jana? Mbona waliomtangulia hawakulihujumu kama hakuna namna hapa? Ina maana wakuu wa mkoa na wilaya waliomtangulia hawakujua umuhimu wa mazingira au ni kutafuta sifa kama siyo kukomoana na kulipiziana visasi ima kwa kujituma au kutumwa? Je Byakanwa ni kati ya wale wakuu wa mikoa au wilaya wanaopenda kujipendekezapendekeza kwa kunyanyasa wenzao ili waonekana wanafanya kubwa ili wapate promosheni au kupendwa kama wanaojulikana kubebwa kwenye jinai zao? Je vyeti vya Byakanwa viko sawa au ni yale yale ya akina Bashit? Je hili ni shamba pekee nchini? Sijui kama Byakanwa ni mtaalamu wa kilimo au mazingira hasa ikijulikana kuwa aliteuliwa na kupachikwa pale bila kujulikana historia yake ili kujua kama anafaa au ni bomu. Hata hivyo, matendo huongea zaidi ya maneno. Kwani waswahili husema: Ada ya mja hunena muungwana ni kitendo.
Byakanwa anadai shamba husika lilikuwa linasababisha madhara kimazingira. Vipi? Kwa kiasi gani na kwa namna gani? Kisomi, mhusika alipaswa aje na utafiti wa kitaalamu kueleza ni kwanini amefikia uamuzi aliofikia. Na je hilo ndilo jibu? Byakanwa ananikumbusha maneno ya baba wa taifa Marehemu Mwl Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa baadhi ya mambo kuyafanya yanahitaji uwe na moyo wa mwendawazimu.  Kwa ushahidi uliopo ni kwamba shamba husika limekuwapo kwa zaidi ya miaka 30. Je uchafuzi huu wa mazingira umeanza au kuonekana leo? Je Magufuli atakingia kifua hujuma hii?
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: