The Chant of Savant

Wednesday 26 April 2017

UDSM: Makufuli fungia makufuru ya kughushi kayani

        Juzi rahis Joni Kanywaji alisema kuwa yeye ni mgumu wa kushukuru. Aliyasema hayo wakati akifungua mabweni mapya ya chuo kikuu cha Manzese. Hata nami Mpayukaji ni jiwe inapokuja kushukuru. Tokana na mfano alioonyesha hivi karibuni wa kuamuru ujenzi wa mabweni ya chuo cha Manzese ufanywe na makandarasi wa ndani tena kwa njuluku kiduchu, amenikuna kwelikweli.
            Kama nilivyosema, mimi ni mwepesi wa kulaumu. Hamkuona nilivyokuwa nikimsakama kuhusiana na kashfa ya Bashit? Hamkuona nilivyokuwa nikimpa vipande pale alipotaka kuminya vyombo vya umbea na vyama vya upingaji? Uzuri naye ananifahamu. Huwa anapokea ushauri wangu na wa kijiwe kwa ujumla na kuufanyia kazi bila kusita kama ambavyo atapokea huu wa leo na kuufanzia kazi.
            Rasmi na toka moyoni, nampongeza mheshimiwa rahis kwa kuona mbali. Pamoja na kumshukuru na kumpongeza, namshauri awatumbue waliojenga mabweni ya Mabibo. Kwa maneno yake mwenyewe alisema kuwa yale mabweni yalijengwa kwenye miaka ya 2000 kwa gharama ya madafu bilioni 27. Sasa iweje miaka takriban 20 baadaye, mabweni kama hayo hayo yajengwe kwa moja ya tatu ya thamani ya miaka 20 iliyopita kama hakuna majipu ya kutumbua? Nashauri uchunguzi ufanywe na wote walioshiriki jinai hii nyingine watumbuliwe kwa kutaifishiwa mali walizopata tokana na jinai hii. Kama atashindwa aombe Kijiwe kimpe tafu kuwanasa na kuwafanyia kitu mbaya.
            Juzi baada ya rahis kusema hayo, wana Kijiwe walipigwa na butwaa kiasi cha kutamani waandamane kumtaka rahis aanzie pale pale chuo cha Manzese kutumbua angalau kwa kutaja majina ya waliotoa tenda na waliopewa tenda ili wachovu wawajue lau wawazomee. Nilimsikia mchovu mwingine akisema kuwa huenda hii Standard Gauge Railway ingejengwa zama za utawala wa kijambazi, huenda gharama zake zingekuwa mara kumi kuliko ilivyo sasa.
            Hebu tujiulize. Hivi tangu tunyake uhuru tushapoteza matrilioni mangapi ya madafu? Kama mabweni yalipaishwa bei hivyo, ilikuwaje kwenye ununuzi wa magari ya umma? Ajabu hawa hawa ndiyo walioruhusu wawekezaji ambao wamegeuka wachukuaji kuendelea kuiba madini yetu kwa miaka 20 bila kulipa hata ndururu! Kwanini wasikamatwe wakanyongwa ili uwe mfano na somo kwa wengine?  Kabla ya kusahau, nimuombe rahis ateue Makamu mkuu wa chuo mpya badala ya kurefushia mikataba waliostaafu muda wakati tunao vipanga wengi wanaoweza kuongoza chuo cha Manzese. Tokana na utamu wa maneno ya Dk Kanywaji, natamani kurejea chuo kikuu cha Manzese lau nisomee shahada yoyote hata kama ni ya kupiga ngoma au michezo.
            Tokana na gharama za kuishi kwenye mabweni ya Mabibo, kwanini yasiuzwe na kupanua ujenzi wa mabweni mengine karibu na chuo ili kuondoa usumbufu kwa wanachuo? Japo nakumbuka kichovu, wakati sisi tukipiga book zama zile, kila kitu kilikuwa swaafi kiasi cha kuotesha hata viriba tumbo. Wakati ule elimu ilikuwa mali siyo kama sasa inapoghushiwa ukiachia mbali wengi wachovu kupenda kuuza bwimbwi na kuukata haraka. Pia nichukue fursa hii kumpongeza rahis kwa ahadi aliyotoa wakati akifungua hayo mabweni ya kuwatumbua wenye vyeti feki bila kujali umbali wala ukaribu naye. Nadhani wengi tutapigwa na mshangao atakapoamua kufanya kweli na siku si nyingi.
            Kwa sasa miji yetu mingi ina ukosefu wa majumba ya wafanyakazi wa umma, je kama tutaamua kutumia Taifa Building Agency (TBA) badala ya mashirika kama National Social Insecurity Fund (NSIF) ambayo yameonyesha kufanya madudu kule Kigamboni, tungeweza kujenga majumba mangapi kwa ajili ya wafanyakazi wa lisirikali? Pia nimkumbushe Dk Kanywaji zile nyumba za wachovu zilizopunyuliwa na wanene zama za Ufichi na Uongo wa mzee Dugong. Je bado haoni kuwa hili nalo ni jibu au ni kaburi analoogopa kufukua asishindwe kulifukia? Kwanini hata ujenzi wa majumba ya kuuza ya umma yasifanywe na TBA hawa hawa ambao wameonyesha mfano wa kuigwa? Niwapongeze TBA kwa kuonyesha mfano kuwa hata makampuni yetu ya ndani yana uwezo na sifa za kufanya mambo tuliyozoea kuyapa makampuni ya kigeni baada ya kuahidi ten au twenty even thirty percent. Natamani hata siku moja Standard Gauge Railway nyingine ijengwe na makampuni ya nchini.
            Hakuna rahis Makufuli aliponiacha hoi kama aliposema ametia makufuli kwenye makufuru ya walaji wa kaya yetu. Nataka wote waliozoea kutuibia awatie makufuru kwa kuwatumbua na kuwataifishia mimali waliyojilimbikizia baada ya kutuibia. Kabla ya kusahau, akina Mgoshi Machungi, Kapende, Mipawa, Sofia Lion aka Kanungaembe, Mipawa, Mijinga, Mheshimiwa Bwege Mbwamwitu, Msomi Mkatatamaa na Kanji wamenituma kumpa kavukavu Dk Kaywaji kuwa utumbuaji hautakamilika wala kuleta maana bila kuwatumbua Bashit  na swahiba yake mchunaji Jose Gwajimmy vinginevyo awatangaze kuwa makaburi ambayo anaogopa kuyafukua kwa kuhofiak ushindwa kuyafukia. Hata hivyo, wana Kijiwe wako tayari kumpa tafu kwa kuyafukulia na kuyafukilia mbali makaburi yote kayani bila kujali ukubwa wala uozo wake. Otherwise, Congrats Dr Mugful.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: