The Chant of Savant

Tuesday 7 March 2017

Waandishi wa habari hamjamtendea haki Janet Magufuli


          Image result for photos of janet magufuli     
         Tangu aingie madarakani, rais John Pombe Magufuli, licha ya kujizolea sifa kemkem, amekuwa kitendawili. Leo tutazungumzia mkewe mama Janet Magufuli. Ukiachia mbali watanzania kumjua kama mke wa rais, first lady, hajulikani inavyopaswa. Kwani, kama mke wa kiongozi mkuu wa nchi, historia yake haijuliani. Umma una haki ya kuijua historia ya mke wa kiongozi wao sawa na wengine.
            Ukiondoa mama Magufuli, historia za wake wa marais waliotangulia zinajulikana kwa watanzania wote. Hivyo, ni haki kabisa, kutaka kujua historia ya mke wa rais wetu. Nadhani watanzania wengi wana tashwishi na mshawasha wa kutaka kumjua first lady wao. Ukiachia mbali kujua tu, kujulikana kwa historia yake kunaweza kuwa motisha kwa wanawake wengine, hasa watoto wa kike. Hivyo, si vibaya kusema kuwa vyombo vya habari ima kwa kutojua uzito wa mhusika au kutojua tu, vimeshindwa kujitokeza kumhoji lau taifa lipate kumjua vilivyo.
            Janet licha ya kutojulikana vilivyo kwa watanzania ambalo ni haki yake, ana sifa ambazo watangulizi wake wote ukiondoa mama Maria Nyerere mke wa baba wa taifa Marehemu Mwl. Julius Nyerere, ana sifa kemkem alizojizolea sambamba na mumewe kwa muda mfupi waliokuwamo ikulu. Ni mama ambaye, tangu aingie ikulu, hajihusishi na ufanyaji biashara akiwa ikulu ingawa wapo wanaoona kama anafanya biashara ya NGO kwa mlango wa nyuma hasa ikizingatiwa kuwa wakati mwingine anavyozunguka huku na kule akitoa misaada amejenga shaka kuwa huenda angependa awe nayo ila mumewe saa nyingine hauruhusu. Maana amekuwa akionekana na mke wa waziri mkuu Kassim Majaliwa, Mary wakitoa misaada bila kuelezea wala kueleweka namna walivyopata hiyo misaada jambo ambalo kidogo linamchafulia sifa hapa.  Akihojiwa huenda ataeleza kinachoendelea ili kuweka mambo sawa.
            Wake za marais waliomtangulia, ukiondoa mama Maria, wanasifika kwa sababu za hovyo hasa kutumia mamlaka ya waume zao kuanzisha Mashirika yasiyo ya kiserikali almaarufu kama NGO kujitafutia utajiri wa haraka kwa kutumia mbinu zenye kutia kila aina ya shaka. Wapo waliowachafua hata waume zao walioingia madarakani wakisifika kama Mr. Clean lakini wakaondoka wakiwa wamechafuka hakuna mfano. Hakuna haja ya kutaja majina; kwa vile wanafahamika. Mtu wa namna hii si wa kupuuzwa. Wengi wangetaka kusikia mawazo yake juu ya hizi NGO ambazo umma wa watanzania walio wengi walizichukia na kuziona kama sehemu ya ufisadi wa kimfuko uliokuwa umeanza kuzoeleka. Kwa kujitenga na biashara hii ya hovyo, Janet, amejijengea imani na heshima kubwa kwa watanzania.
            Watanzania wangependa kujua namna alivyolelewa, wakati alipozaliwa, alivyosoma na hata kazi alizofanya kabla ya mumewe kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania. Pia wangetaka kujua changamoto anazopambana nazo na namna anavyozikabili na kumsaidia kiongozi wake kama mwenzi na mtu wake wa karibu. Tunasema haya si kwa kutaka kumchimba mke wa rais wetu. Hasha. Tunataka kumjua lau awe motisha kwa mabinti zetu. Kama kiongozi wa umma, lazima umma umjue vilivyo. Yeye hatakuwa wa mwisho wala wa kwanza. Tumeshuhudia hivi karibuni namna mke wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, Michelle, alivyodurusiwa na vyombo vya habari kiasi cha kujulikana karibu sawa na mumewe duniani kutokana na historia yake kama mama na mke wa rais kiasi cha kupigiwa debe agombee urais wa Marekani. Mfano mwingine ni wa Hilary Clinton, mke mwingine wa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton aliyegombea urais mwaka jana akashindwa na rais Donald Trump kwa mizengwe ya kila aina. Ukiachia mbali wake wa marais wa Marekani, mke wa imla wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh, Zenab, anasifika sana kuwa kuwa mstari wa mbele kuliibia taifa hili dogo la Afrika Magharibi, ukiachia mbali Simone Gbagbo mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast aliyechangia kikubwa kuanguka kwa utawala wa mumewe ambaye yuko korokorini The Hague, Uholanzi akingojea kusikilizwa kwa kesi yake dhidi ya umma wake aliousababishia matatizo tokana na upogo na uroho wa madaraka. Baada ya kudondoka kwa Gbagbo vyombo vya habari viliripoti kuwa kama si mkewe, hakuwa king’ang’anizi wa madaraka.
            Siku hizi, baadhi ya wake za marais katika baadhi ya nchi wana ushawishi mkubwa kiasi cha wakati mwingine kuogopewa kuliko waume zao kama ilivyokuwa kwenye utawala wa Gbagbo. Katika nchi ya jirani ya Uganda, kwa mfano, mke wa rais, Janet Museveni, licha ya kuwa first lady, ni waziri katika serikali ya mumewe. Huko nchini Zimbabwe, mke wa rais, Grace Mugabe, anaogopewa kuliko Robert Mugabe, rais mzee na king’ang’anizi. Mpaka sasa hatujui kinachosababisha hali hii kati ya udhaifu wa mume au ujanja wa mke. Hata hivyo, kwa namna alivyoanza rais Magufuli, mkewe ameonyesha kutokuwa na hamu ya kutumia mgongo wa mumewe kama watangulizi wake kujitajirisha au kujiingiza kwenye biashara ya aibu kama kusaka madaraka kupitia mgongo wa ikulu kama baadhi ya waliopita ambapo wake zao wanaonekana kwenye vyeo kwenye vyama vyao jambo ambalo ni aibu na ishara ya uroho wa madaraka. Viongozi hawa hawakupaswa kulipwa hata marupurupu ya ustaafu hasa ikizingatiwa kuwa bado wako kwenye active politics.
            Tumalize kwa kuvitaka vyombo vya habari nchini kumtendea haki mama Magufuli kwa kuleta historia yake kwa jamii ya umma anaoongoza sambamba na mumewe. Naomba nitoe hoja.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
 

No comments: