The Chant of Savant

Saturday 4 March 2017

Neema Muita Wa-mura: Wanene wote waige moyo wa Mugful

Image result for photos of neema mwita wambura
            Japo si mara ya kwanza au ya mwisho kwa munene Joni Kanywaji Mugful kutenda wema kwa mlevi wa kipato cha chini, kitendo chake cha hivi karibuni cha kumjulia hali na kumsaidia fedha kidogo mhanga wa vurugu za kifamilia bi Neema Muita Wa-mura ni jambo la kupigiwa mfano na kupongezwa. Licha ya kuwa moyo wa upendo wa kweli kwa walevi hasa wanyonge, rahis amewasuta wasaidizi wake na wanene wengine wa kila ngazi. Hakuna waliosutwa kama wanene wa mkowa wa Mara kuanzia mnene wake, waishiwa na wengine wengi ambao–licha ya tukio hili ovu kutokea mkoani mwao–walilichukulia kivyepesi kiasi cha kulazimisha rahis kuingilia kati.
            Kinachogomba kuhusiana na kitendo hiki cha upendo uliopindukia ni ukweli kuwa rahis alipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii. Hii maana yake ni kwamba wanene wa wilaya na mkowa mzima hawakushughulilikia kadhia hii vilivyo. Sijui kama mtuhumiwa alishakamatwa. Na kama alishakamatwa, inakuwaje muathirika aliyehitaji matibabu hakushughulikiwa aachwe hadi munene mwenyewe aingilie kati? Maana, tunaelezwa jinai ilitokea Mei, 2015 kabla ya rahis Kanywaji kuchaguliwa? Je wapo akina Neema wangapi wanaodhulumiwa haki na wenzi wao Kayani ambao taarifa zao hazijulikani kwa walevi hata kama zinajulikana kwa wanene wa maeneo yao wasiopenda kuzisambaza wala kushuzishughulikia? Je kwanini kadhia hii iliachwa hadi imfikie munene wakati kulikiwa na wanene wa ngazi ya chini? Je munene ana haja ya kuwa na watendaji kama hawa wasiojali wenzao?
            Hakuna kitu kinamfariji mnyonge kama munene kumjali ukiachia mbali kumsaidia kama alivyofanya al rais.  Sipati picha muathirika alipata faraja na nafuu kiasi gani alipopigiwa simu na munene tena bila kujitambulisha hadi alipofikishiwa msaada wa madafu laki tano na ahadi ya kumtibia zaidi na kutunza vitegemezi wake.
            Baada ya taarifa hii kusambaa kwenye mitandao, walevi wengi walionekana kuguswa na kitendo cha munene kisicho cha kawaida. Pamoja na wachangiaji wengi kutokubaliana na munene katika masuala mengi kama yale anayosema kwenye hotuba zake ambazo ziko mtandaoni, katika hili, waliungana. Nadhani hapa–licha ya kusukumwa na huruma na utu–wengi walijiuliza swali moja: Je ingekuwa mimi ndiyo muathirika ningependa nitendewe vipi? Nadhani hili ni swali adimu ambalo walevi wetu wa madaraka na wenye uwezo wanashindwa kujiuliza katika kutimiza majukumu yao. Hakuna kilichonivutia na kunihamasisha hadi nikapiga kanywaji kumtakia mafanikio mnene kama wema wake. Mbali na hili, wengi wameandika ujumbe mbalimbali. Tutanukuu baadhi.  Mary Njeri, ambaye bila shaka ni kutoka kwa manyang’au, aliandika “munene wa Tz Ngai (God) akubariki kwa kazi hunayo fanya.Hata ninahisi kama sasa nitahamia Bongolalaland” huku Sharo Mosses akiandika “machozi yamenitoka,  Sir God akubariki muthamaki Kanywaji, kwa kweli ni mutongolya (kiongozi) wa kuigwa dunani kila la heri, tunafarijika kiukweli.” Naye Soleil Neema aliandika “yaani Afrika ingekuwa na wanene kama Kanywaji, ingekuwa mbali sana yaani Nyasae amufunike kwa damu yake juu munene kama huyu vita inapashwa inuka.”
            Kwa muda mfupi ambapo tukio hili liliwekwa kwenye mtandao wa yutube lilivutia wachangiaji wapatao 92 ndani ya masaa mawili.
            Japo munene ametoa mchango wake kama mlevi mwenye mapenzi mema na huruma kwa wenzake hasa wanyonge, tunashauri awawajibishe wanene wote walionyamaza baada ya kutokea kadhia hii huku akihakikisha aliyetenda kitendo hiki cha kihayawani anapata stahiki yake kulingana na kitendo alichotenda. Tunaamini akiwatia adabu wanene wa wilaya na mkoa husika, litakuwa somo si kwa wahalifu na wanyama wanaoumiza wenzao bali hata wanene wao wasiojali maisha na haki za wanyonge kwenye kaya yote.
            Itakuwa ukosefu wa shukrani na wizi wa fadhila kama sitampongeza mjane Mariam Amir (Bibi Mwaija) aliyemuibua Neema kwa kumchukua na kumweka nyumbani kwake pamoja na umaskini wake. Ningekuwa munene, ningemteua bi huyu kuwa mkuu wa mkowa wa Mara ili liwe suto kwa waliozembea kushughulikia unyama huu. Kufanya hivyo, licha ya kuwa faraja kwa wanawake wengine mkowani Mara na Bongolalaland walioumizwa, kukatwa mikono, kuharibiwa sura na madhira mengine ukiachia mbali kuwa onyo kwa wahalifu na wanene wanazembea kuwahudumia walevi.
            Tumalizie kwa kuwahamasisha wadanganyika wote kuwa na moyo wa huruma kama walivyofanya rais munene na bi Mwahija. Badala ya wengi kupoteza muda kuandaa matamasha ya kuombea Kaya huku wakikalia ukwasi wa kutisha na wa kutia shaka, wawekeze kwa wanyonge. Kwani hata Mwana wa Adam ambaye baadhi wanajidai kumuhubiri aliacha wosia huu Matayo 22: 38 alipotaja amri kuu mbili yaani ya kwanza kumpenda God wako; na ya pili kumjali jirani yako. Je jirani yako zaidi ya Neema ni nani? Hakika munene na bi Mwahija wamezijua na kuzitekeleza amri hizi kuu mbili yaani kumpenda God kwa kuwajali walevi wake hasa wenye mahitaji na shida na kuwajali majirani zetu ambao kimsingi si wale wanaoishi nyumba ya pili bali maskini, wajane, yatima, wanaokeketwa na wengine kama hawa ambao wengi wa wahubiri wetu wa kujipachika wanawadhulumu na kuwahadaa bila kuwapa msaada wowote. Nawapongeza munene na Mwahija. Mungu awalipe mara milioni kwa upendo wenu wa dhati. Munene tafadhali nipigie nami nikubomu kitu kidogo.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: