The Chant of Savant

Tuesday 14 March 2017

Kijiwe chawapa shavu CCM kuvuana magamba

    Image result for photos of sofia simba
      Juzi karibu kijiwe kilikuwa na mikutano na vikao visivyo rasmi. Hii ni baada ya Chata Cha Magamba (CCM) kuamua kujivua magamba angalau kwa juu juu huku mengine yakibakizwa na kupewa onyo. Hata hivyo, sijui kama nyoka akijivua gamba anageuka fimbo.  Sisi tunaamini kuwa nyoka ni nyoka na dawa yake ni kumsigina au kumpiga rungu kichwani. Tunawapongeza na kuwapa pole waliotumbuana ingawa ni kile walichofanya kitasha huitwa cosmetics kama siyo window dressing.
Sofia Lion aka Kanungaembe anaingia akiwa amenuna. Japo wote tunajua kilichompata, tunajitahidi kuvuta subira tusikie maoni yake. Anaamkua na kusema “jamani yameishakuwa nimevuliwa gamba kama mlivyosikia tena kwa uonevu mtupu. Hakika naanza kuamini mliyonya siku nyingi kuwa wale si watu. Hata hivyo, sina kinyongo na mtu na isitoshe nitajiunga na upingaji lau kuongeza nguvu ya kuwavua waliotuvua gamba magamba pia.”
Mbwamwitu anamchomekea “nasikia hata mrithi wa nafasi yako ya urahis wa akina maza ashateuliwa uheshimwa tayari kuja kuendeleza utawala wa familia.”
“Huna haja ya kulalamika da Sofi. Umesafishwa  na kutakata. Huna gamba wala si nyoka tena. Hivyo, nakushauri ukae kijiweni na kutulia na kufanya mapambano bila makeke wala mshawasha,” anampoza Kapende.
Mgoshi Machungi anaamkua kula mic “sisi tiijua kuwa azima wapo watakaotumbuiwa tena wasiotegemea kama wewe da Sofia ambaye nakupa poe hata hivyo. Unakumbuka niiwambia kuwa Madabidabi pamoja na kuonekana na Kondakonda kia siku aikuwa kwenye target tena haya ya mibwimbwi? Tinajua na tinangoja tione nani watatumbuiwa zaidi akiwamo Dave Basheti aka Poo Kondakonda ambaye nasikia aihis anamkingia kifua bia mafanikio tokana na uzito wa tuhuma zake. Tinangoja kujua mbivu na mbichi ii titoe meseji yetu wati-understand na kuti-compiend.”
Mheshimiwa Bwege anakula mic “da Sofia hayo ndiyo malipo. Unakumbuka kipindi kile ukinsifia mwenyekiti hadi tukawa na wasi wasi kabla ya wewe kutondoa shaka. Kimsingi, wamekusaidia hasa ikizingatiwa kuwa kama tutasema ukweli, ulimshabikia jamaa ambaye kijiwe wakati ule kilimshuku kuwa fisadi baada ya wapingaji wenyewe kusema hivyo baadaye wakankumbatia.”
Sofia anajitetea “kwani kumshabikia mtu ni kosa katika kaya ya kidemokrasia kama yetu? Mie sikujua hivyo. Kama ni hivyo, mchakato mzima wa kumsaka mgombea urahis kumbe ilikuwa ni uchakachuaji wa kawaida uliovishwa jina zuri la mchakato ili uonekane wa kidemokrasia wakati ni udkiteta mtupu?”
Kanji anapunyua mic “sisi iko naambia veve kaya chonjo lakini nakataa. Iko jua veve haikujua iko gamba hadi natumbua na kuvua veve gamba. Sasa shikaji hapana danganyika tena. Nenda fungua dukani nyingine ya siasa kwa pinjani kama ile sanii nakamatwa kwa bimbi nafanya.”
Mipawa anaamua kutia guu “hebu tuwe wakweli jamani. Hivi uanachama wa chama fulani ni uuzaji wa uhuru kumshabikia amtakaye na kumkataa asiyemtaka? Sioni kosa la da Sofi na wenzake hasa ikizingatiwa kuwa waliyekuwa wakimzimia kipindi kile alikuwa mwanachama na kada mwenzao. Hapa kosa liko wapi jamani kama siyo ubangaizaji, usanii na kulipiziana visasi na kufanyiana visa? Ama kweli waliosema kigumu chama cha mapandikizi hawakukosea!”
Mijjinga aliyekuwa akinong’ona jambo na Msomi anaamua kula mic “nadhani wengi mnashindwa kuelewa dili. Hapa mkiti anatoa tangazo kuwa hatavumilia yeyote mwenye mawazo huru au kinzani na yake. Kimsingi, hiki ni kiboko alichotumia ili kuwajaza wenzake woga awaburuze atakavyo hata kama ni kuwaelekeza shimoni. It doesn’t add up for me so to speak.”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamchomekea “Mijjinga lugha hiyo kaka. Punguza kikameruni tafadhali.”
Mijjinga anajibu “shukrani kaka japo najitahidi kuonyesha kuwa mie sina cheti cha wengine na wala si kughushi kama akina Bashite na Gwajimmy. Tukiendelea na suala la kuvuliwa da Sofi, sijui nani amejiandaa kumchukua kabla wengine hawajamnyemelea.”
Kapende anarejea “da Sofi wala usiwe na shaka. Wewe sasa ni mali kweli kweli. Wapo wengi wanadondosha udenda. Muhimu ni kutulia tuli kama unanyolewa au vipi dada yangu?”
Mchunguliaji ambaye hana kawaida ya kuchangia anakwanyua mic ‘duh! Kaka Mijjinga na Kapende mmeniacha hoi. Eti da Sofia kavuliwa na wengi wanandondoshea udenda na tena atulie! Aangalie asivuliwe zaidi na kufanyiwa kitu mbaya.”
Mpemba aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia guu “yakhe acheni utani. Aniposema anvuliwa amaanisha gamba na si nguo yakhe. Pia aniposema atulie kama anyolewa amaanisha asiwe na papara ya kujiunga na vyama vingine bila kufanya utafiti ati. Hivo, mie ntaka niweke wazi kuwa kweli wapo wengi wanasiasa wannyemelea da Sofia. Hankuona yule nsanii aniyedaiwa avuta unga alivodandiwa haraka haraka hata bila kunchunguza wasijue aweza kuwa bomu?”
“Unaongolea yule mwenye jina kama kulego siyo? Hapo kimsingi imekula kwao hasa ukiangalia maisha yake na mama yake yalivyokuwa ya kisanii na walivyojiachia wakatumiwa na magamba kabla ya kugeukwa,” anachomekea Kapende.
Msomi aliyekuwa kimya muda wote anakula mic “najua wengi mmeshangaza na uvuanaji magamba huu. Kimsingi, huu ni mwanzo na utashangaza wengi. Ukitaka kuharibu demokrasia kayani, unaanzia nyumbani kwako. Leo sisemi mengi. Kwani, bado natafakari ya kusema.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likakatisha shangingi la first lady mbunge! Acha tulizomee!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho

No comments: