The Chant of Savant

Saturday 4 March 2017

First lady kuwa mbunge ni demotion au promotion?

Image result for photos of magufuli and salma kikwete
          Japo rais ana mamlaka ya kumteua amtakaye kuwa mbunge–kwa nchi ya kidemokrasia na utawala bora na kuepuka mgongano wa maslahi–hawezi kumteua mkewe au mwanae kuwa mbunge wa kuteuliwa. Sijui katiba yetu inasemaje hapa. Pia, kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu kama wenye nchi yaani wananchi, sijui kama kuna anayefurahia rais kumteua mke wa rais mstaafu ambaye yeye na mumewe wanalipwa marupurupu ya ustaafu.         Hivi karibuni, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, rais John Magufuli alimteua mke wa rais mstaafu Kanali mstaafu Jakaya Kikwete, Salma kuwa mbunge. Kitendo hiki kimevutia hisia tofauti. Wapo wanaoona kama kitendo hiki ni matokeo ya kujuana na kufadhiliana ukiachia mbali kumshusha mke wa rais. Kwa mfano Mwenyekiti wa Mkoa wa zamani wa Shinyanga wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mgeja alikaririwa akisema “namuomba Mama Kikwete aige mfano wa mama Regina Lowassa (mke wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa) ambaye wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baada ya uchaguzi Chadema ilimpa heshima kwa kumteua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu lakini kwa heshima aliikataa nafasi hiyo.”  
          Pia kitendo hiki kinaweza kutafsiriwa kama uroho wa madaraka ukiachia mbali matumizi mabaya ya ofisi na fedha za umma. Je Salma ataendelea kuhudumiwa kama mke wa rais mstaafu na hapo hapo kama mbunge? Je kitendo cha Magufuli kumteua Salma hakipingani na ahadi yake kuwa hataruhusu mtu kuwa na kofia mbili? Baada ya kuwa mbunge, ina maana, Salma ataacha kuwa mke wa rais mstaafu? Na kama ataendelea na kofia ya first lady mstaafu anayepewa kila stahiki sambamba na mumewe, kwa kupewa mshahara na marupurupu ya ubunge siyo kuwa na kipato zaidi ya kimoja tena vyote vikitolewa kwenye kodi ya watanzania maskini? Je watu wanaofaa ubunge aliopaswa kuteua Magufuli wameadimika kiasi hiki au ni ubabe tu?
          Wapo walioonyesha kuwa Salma alianza zamani kupenda vyeo alipoamua kujiingiza kwenye vyeo vya kichama kupitia chama cha mumewe tena akiwa madarakani na asikemewe. Wengi tuliandika kulalamikia chama kugeuka mali ya familia na mke wa rais kushiriki kunyang’anyana vyeo vidogo ikilinganishwa na hadhi yake ya kuwa mke wa rais lakini hatukusikilizwa. Hata hivyo, hili la kuteuliwa alipaswa akatae kulinda hadhi ya nafasi yake kama mke wa rais mstaafu. Ni bahati mbaya, alipoanza kusaka vyeo, watanzania walimnyamazia akaendelea kufaidi nafasi yake kisiasa na ile ya mke wa rais. Je kitendo hiki kinaashiria nini huko tuendako? Ina maana sasa rais anaweza kumteua mkewe kuwa mbunge hata waziri akitak na asivunje sheria. Maana, hana tofauti na mke wa rais mstaafu. Je Salma anamwakilisha nani na anatoa picha gani? Kwenye kutumia NGO wakati wa utawala wa mumewe kwa kisingizio cha kuwasaidia watoto wa kike hakutosheka. Kwenye kumilki shule iliyotokana na biashara ya NGO hakutosheka. Kwenye kupeleka karibu misaada yake mingi mkoani alikozaliwa hakutosheka. Je atapewa nini atosheke au ana mpango wa kugombea urais baadaye?
           Sipati picha atakapokuwa bungeni akinyukana na wabunge wengine hasa wa upinzani. Hata hivyo, anaweza kuingia bungeni na kuamua kukaa kimya na kula fedha ya uheshimiwa ambao hajautolea jasho wala hana anayemwakilisha zaidi ya tumbo lake. Jamani, tufike mahali tutosheke. Maana, kama tutaendelea madaraka kufadhiliana kuhudumiana, kuzawadiana kwa namna tutakavyo wakati huo huo tukiwaaminisha wanyonge wasio na uwezo wa kuteuliwa wala kuajiriwa, tutakuwa tunajipinga licha ya kuwa sura mojawapo ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Hapa ndipo umuhimu wa kurejesha rasimu ya Katiba Mpya iliyouawa kifisadi unapojitokeza. Maana, katika hii ilikuwa imeeleza vilivyo dhana nzima ya utawala bora na wa sheria. Kamakweli rais Magufuli ana nia njema na taifa letu na ana nia ya kupambana na uoza na kuleta uongozi bora na wa sheria, basi arejeshe rasimu ya Katiba Mpya ili ipitishwe na watanzania kama ilivyopendekezwa na watanzania na si CCM. Katiba mpya inaitofautisha Tanzania na nchi zinazotawaliwa na maimla wanaoweza kuwateua wake zao na watoto wao kwenye serikali zao kama ilivyo nchini Equatorial Guinea, Uganda na kwingineko. Nani anataka nchi kama hii ambayo watu wake wamegeuzwa mateka na watumwa wa watawala wabovu? Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuongozwa kwa utashi wa wananchi na si watawala. Hivyo, uteuzi wa Salma utumike kama kumbushio kuwa tusiporejesha Katiba Mpya, watatokea watawala watakaofanya mambo kana kwamba taifa letu ni la kifalme na si kidemokrasia ukiachia mbali kuligeuza kama mali binafsi.
           Tumalizie kwa kuhoji. Je rais na Salma wanatoa picha gani kwa wanyonge wasio na namna ya kuchaguliwa wala kuteuliwa? Heri angemteua mama wa kijijini lau aende kuwawakilisha wanyonge wenzake badala ya mke wa mkubwa mwenzake. Je uteuzi wa Salma ni wa kikatiba, na kibusara? Maswali ni mengi kuliko majipu. Je uteuzi wa Salma ni promotion au demotion?
Chanzo: Tanzania Jumapili kesho. 

No comments: