The Chant of Savant

Sunday 6 November 2016

Mpayukaji aitwa kwa Joji Kichaka kupiga tafu kampeni


Image result for clinton and trump           























Baada ya lile baguzi la kunuka liitwalo Don Drumpfy kuanza kuchafua hali ya hewa kule kwa Joji Kichaka na Obamiza, chama cha Kidemokrasi kilimwomba mzee Mzima kutia timu kuokoa jahazi. Nilitua zangu La Guardia International Airport pale New York na kupokelewa na Bill na Hill. Kumbuka hii ilikuwa ni mara ya pili kuitwa kwenda kuokoa jahazi.
            Hata hivyo, nimejifunza vitu viwili vitatu kwenye kampeni hizi za taifa kubwa ulimwenguni lenye kusifiwa kwa kudengua na kujivuvumua.
            Kwanza, nimegundua kuwa taifa hili linaanza kuishiwa kulhali. Sikuamini kuwa ningekutana na ombaomba kibao na wachovu wasio na makazi kwenye jiji kubwa kama New York. Hivyo, naweza kusema kuwa uchumi wa wa kaya hii unaanza kuharibwa na vita vya kipuuzi vya kujitakia.
            Pili, niligundua kuwa kumbe na kule kuna uchakachuaji. Maana Drumpfy amekuwa akipiga kelele kuwa uchaguzi utachakachuliwa hata kabla uchaguzi wenyewe haujafanyika. Drumpfy alinikumbusha kisa cha Joji Kichaka kumshinda Al Gore kwa bao la kisigino lililochezwa kwenye jimbo la Florida kipindi kile.  Hali ninayoiona hapa, kama ingekuwa inatokea kwenye kaya ya Kiswahili , kwa mfano kuhusiana na vitisho anavyotoa Drumpfy, bila shaka wakubwa wa kaya hii wangekuwa wameishabweka kwa kupiga mkwara wakitishia  na kuwaonya wanakaya kutochagua bomu kama Drumpfy.
            Tatu, nimejifunza kuwa kaya ya kwa Joji Kichaka haijajifunza lolote tokana na historia yake ya ubaguzi wa rangi, dini na kijinsia. Nani amesahau namna waswahili walivyokuwa wakibaguliwa sawa na makaburu kule kwa mzee Diba wa Madiba? Kitu kingine kilichonichekesha ni kwa Drumpfy kuwachukia walatino wakati wanakuja kule kufanya vibarua na kulipwa njuluku kidogo na kuwafanya wakulima na waajiri wa kule kupiga njuluku bila kutoa jasho. Sijui hili nalo linahitaji PhD?
Ukimsikia huyu Drumpfy sera zake ni ubaguzi mtupu na ushenzi usio na mfano. Huyu jamaa anakera Mungu pekee ndiye ajuaye. Pia ni mkware wa kunuka anayejifisia kuweza kumfanyia mwana mama yoyote kitu chochote hata bila ridhaa yake. Anachukia waislamu na walatino hakuna mfano. Amependekeza kujenga ukutua kwenye mpaka na Mexco ili kuzuia wazamiaji kuingia Umarekanini na kufaidi kama magabacholi wanavyofaidi afria.
            Kama haitoshi, aliwahi kutamka kuwa Afrika ilipaswa kutawaliwa upya ili iweze kuendelea. Juzi nilikuwa na mpango wa kumvamia na kumuuliza kama aliwahi kusikia habari za Joni Kanywaji Makufuli na mambo Anayofanya. Pia nilitaka kumuuliza kama anamjua Bob Jongwe Mugabe ambaye aliwahi kutaka kutuma wasimamizi wa uchaguzi Umarikanini hasa baada ya uibuka lile sakata la uchakachuaji ulimuingiza Joji Kichaka White House.Ajabu, pamoja na kuwa baguzi la kunuka, mkwepa kodi, muongo mkubwa, bado anapata kura.
            Nani angeamiani kuwa kaya inayojifanya mtetezi mkuu wa demokrasia ingeishia kuwa kiongozi wa ghasia?
            Nne, nimegundua kuwa watasha nao wana mambo ya Kiswahili usiambiwe. Wakati wa mchana wanajifanya kumchukia Drumpfy tokana na kutokuwa na sera na kama anazo ni za kibaguzi ingawa usiku wanamuunga mkono. Wanafanya kama wale wazee na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Maulaji (CCM) wanaoshinda CCM na kulala kwenye upingaji kama alivyowahi kusema jamaa mmoja.
            Tano, nilishangaa jitu ambalo linasifika kwa kukwepa kodi na kutapeli wachovu kuruhusiwa kugombea cheo kama hiki. Hapa bila shaka kuna namna. Sitashangaa kuona Umarekanini ikifilisika kama Uingerezani ambayo kwa sasa imebakia kuwa mkia wa Umarikanini wakati hapo zamani ndilo lilikuwa taifa kubwa kuliko yote likisifika kwa ujambazi, ujangili na ukoloni duniani kote.
            Ukigeukia mgombea wa upande wa pili yaani bi Mkubwa Hill, nako kuna wingu hasa usiri na utumiaji wa vifaa binafsi kupitisha barua pepe kiasi cha kuhatarisha usalama wa kaya hii kubwa. Hata hivyo, ukilinganisha substance ya wagombea wawili, lau mwana mama anaonyesha mwelekeo. Kama atashinda, atakuwa ni mama wa kwanza kukaa White House kama top na kuwa amiri jeshi wa kwanza mwanamke ukiachia mbali kuwa First Lady wa kwanza kuwafanya hivyo.
            Kama siyo sirikali nyingi za Umarekanini zilizopita kutawaliwa na ufisadi na ulafi, huyu mama angesepa bila kutoa jasho hadi kulazimika kuniita nimpe tafu. Guess what.  Wamarekanini wanachukia sirikali; na hawana imani nazo tena. Wanachukia kile wanachokiita Washington Bureaucracy. Wanaona mji wao mkuu kama kikwazo cha maendeleo yao ambapo vigogo huenda kupiga dili badala ya kuwatumikia wachovu.
            Tokana na kutokuwa na muda wa kuchonga, kijiwe cha leo kitakuwa kifupi. Kwanini nina ratiba ya kuruka na pipa kwenda kwenye kampeni ya kuua mtu.  Hadi hapo tarehe 8 Novemba, nitakuwa nikijitahidi kumpiga tafu bi mkubwa. Hata hivyo, pamoja na misukosuko anayopata, mambo basi yanatia imani. Anapiga Drumpfy mbele nyuma na kila kona tena bila huruma.
Hivyo, nawasalimia wasomaji wote na wanakijiwe wote toka mlioko huko kutoka huku duniani.
Chanzo: Tanzania Daima Juzi Jumatano.

No comments: