The Chant of Savant

Wednesday 9 November 2016

Kijiwe chashangaa Makufuli kuogopa ‘makaburi’

 
       Baada ya Dokta Joni Kanywaji Makufuli kutoa mpya akisema kuwa anaogopa kufukua makaburi kwa vile hawezi kuyafukia, Kijiwe kimeamua kumpa ushauri tena wa bure. Kijiwe hakikuamini kuwa mtu jasiri na jabari kama yeye angeogopa makaburi.
            Mgosi Machungi analianzisha “wagoshi mmesikia huu nkanda wa makabui aitoa dokta Kanywaji juzi akisema eti anaogopa kufukia akini si kuchimbua makabui? Je mnafahamu haya makabui ni akina nani na waifanya nini kayani kwetu? Je mnafahamu kuwa haya makabui si makabui kama muyajuavyo bai waja waio hai akini waiofanya mambo kama wafu kiasi cha kuitwa makabui?”
            “mgosi hapa sasa nimeamini kuwa wewe ni bonge la mfalasafa jirani na Msomi na mzee Mpayukaji mwenyewe baba wa busara au Abu Hikma kwa lugha ya kinyantuzu.”
            Msomi Mkatatamaa ambaye siku hizi hajivungi anatia guu mapema anakula mic “kama anaogopa makaburi tena si kufukua bali kufukia, atawezaje kuweka kaya kwenye mstari kama anavyotuaminisha? Nadhani hapa tukubaliane tu. Jamaa amepotoka; au tuseme amepitiwa hata kuyataja hayo makaburi. Alipaswa ayaogope; kwa vile yana walio hai tena waliomtangulia katika ukaburi na ufu wao kisiasa na kiutawala. Hata hivyo, nampongeza kwa kuwaita makaburi wakati bado wako hai. Kwa tunaojua ukubwa wa makaburi tajwa, tunaanza kutia shaka dhima na dhamira yake ya kupambana na uovu kwa kuchagua. Huwezi kufukua na kufikia matuta tu ukakingia kifua makaburi. Nadhani makaburi yana uoza zaidi ya matuta hata majipu.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic mapema “hebu tusiogope kuita kulego kulego. Ameyataja vipi wakati ametumia mafumbo. Je mwafahamu kuwa haya mnayodhani ni makaburi ni waja hai tena wenye majina yao? Tena ni wale ambao hamuwezi kuwategemea japo mnawafahamu. Wengi walijipiga vifua na kujitukuza wasijue ulaji una mwisho. Hata naye anapaswa kulijua na kulikubali hili tena kwa unyenyekevu. Sitaki niseme mengi. Kila kilicho na mwanzo shurti kiwe na mwisho. Hata haya makaburi hai yatakufa hata kama yamemeza mali kibao za wachovu.”
“Yakhe kwa mafumbo sikuwezi. Yaani mwenzio aogopa kuwataja watu kwa majina na hali yao wewe wafumbua kila kitu tena waweka wazi. Hapa unkata kweli kweli. Hata mie nlisituka sana kusikia watukufu wakiitwa makaburi japo kweli kwa walotutenda ni makaburi yaniyotembea hata kuenziwa na kuabudiwa bila chochote cha maana walotenda kwetu sie wachovu ati,” Mpemba anachomeka kwa nahau za kipwani.
            Mipawa anakula mic, “kama huyu jamaa anaogopa makaburi, ataweza mizungu na wazungu wa bwimbwi, majambazi, mafisadi na kila aina ya wahalifu waliotamalaki kayani? Je amesahau ahadi alizotoa kuwa hataogopa wala kupendelea mtu awe hai au mfu? Sasa kwanini anawakingia tena kifua hawa wafuhai aliokwisha kuwaahidi ulinzi? Kwani alilazimishwa kurongo aliyoronga au ndiyo hayo ya kupayuka,” ananigeukia na kuniangalia na kusema “mzee simaanishi kukosea heshima. Ila wanapaswa kujua kuwa kupayuka pwenti kuna mwenyewe na mwenyewe ni wewe.” Sijibu kitu zaidi ya kutabasamu kwa ujiko anaonipa huku akimkandia big mwenyewe.
            Kapende naye hangoji; anakwatua mic “kaka usinchekeshe. Ina maana jamaa ameanza kuishiwa nguvu, kuisha, kutuingiza mkenge au ndiyo hivyo anaanza kubadilishwa na mfumo uliofuma na kufunika haya makaburi ambayo hataki kuyafunika japo anao uwezo wa kuyafukua?
Kama hawezi hata kufunika makaburi basi aseme mapema kuwa mzigo umemshinda.” Anapiga chafya na kuendelea, “kama hali ndiyo hii si awapishe wenye msuli wayafukue kuyapekua na kuyafukia hayo makaburi na hata kuchoma moto uchafu uliomo makaburini hasa ikizingatiwa kuwa hakuna maiti mle zaidi ya uchafu.”
            Da Sofia Lion aka Kaunugaemba anakula mic “mwenzenu nimeshangaa sana. Sikutegemea kusikia niliyosika kwa niliyemsikia tena mwenye jabari asiyeogopa kitu wala ntu. Ameaniachia swali moja kuu: Kama nawezafukua kaburi sasa naogopa nini kyafukia au anataka tumsadie kufanya hivyo kama kweli anaogopa?”
             Kanji anaamua kumchomekea mshirika wake Sofi; anampoka mic na kuronga “mimi ona siyo ogopa kaburi. Iko ogopa maiti. Kaburi iko simo tu. Kule Bombey kaburini iko ishi mitu mingi kweli. Vatu hapana naogopa witu kama makaburi bali iti.”
Mzee maneno naye anaamua kumchomekea Kanji; anachonga “naona mtani wangu anaanza kujua Kiswahili hadi mafumbo. Maana alivyowaumbua wenzake kwa kuwapa sifa ya ukaburi sina hamu. Na kweli hawa jamaa ni makaburi yaliyowahi kukaa ikulu na kugeuza pango la wanyang’anyi kama alivyowahi kuonya mzee Mchonga (Mungu amuweke mahali pema peponi mzee wetu). Nadhani hata wao hawakutegemea kuwa–pamoja na kuwakingia kifua–bado jamaa anawalinganisha na makaburi. Wazaramizi tuna msemo mmoja kuwa aliyekuchoka hakuna anachoweza kukulinganisha nacho bali kaburi.”
                        Kijiwe kikiwa kinanoga si ukapita msafara wa mashumbwengu ya kaburi moja! Wacha tuyatoe mkuku kuona yana nini yananuka vipi! Kama siyo ndata kufunga barabara, tungemnasa kwenye mataa na kumpa vipande vyake huku tukimfukua na kutaka, atumbuliwe na kufukiwa lupango.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: