The Chant of Savant

Wednesday 30 November 2016

Kijiwe chamuunga mkono askofu Mokiwa

 
             Baada ya kuzidi kuongezeka kwa matapeli na wapigaji wanaotumia majoho, askofu Zaky Mokiwa ameamua kuwatolea uvivu. Ameripotiwa akitaka mamlaka kuwachunguza hasa aina ya mahubiri wanayotoa. Uzuri hili limetoka kwenye kinywa cha mwenzao ambaye hata hivyo siyo wa kujipachika wala kanjanja kama wale alishauri washughulikiwe.
            Mipawa ndiye anaanzisha mada baada ya kutua gazeti la Rongaronga mezani ambalo Mchunguliaji analidaka na kuanza kulibukua. Anauliza “wazee mnalisemeaje hili la kutaka wachungaji, wachunaji na wapigaji wanaotumia neno la Mungu kutuvuruga, kutunyonya, kutudanganya, kutuibia hata kutudhalilisha ambalo limetolewa na askofu wa kweli Zaky Mokiwa?”
            Kapende anakula mic “hili halina njadala. Lazima wajanja hawa wanaowarubuni na kuwaibia wajinga wetu wachunguzwe ndani na nje bila ya cha nsalie Ntume. Haiwezekeni kama kaya tukaendelea na aina hii ya ufisadi wa kiroho ulioshamiri uroho.”
            Mpemba anampoka mic Kapende na kuronga “hata mimi nakubaliana na pendekezo hili hasa wakati huu wa “Hapa Kazi Tu”. Kwani, waliachiwa na kujitajirisha huku wakiwasikinisha wajinga wengi walioharibikiwa maisha kutokana na elimu haba. Wanachofanya baadhi ya wachunaji waliojivisha majoho ni ufisadi, ujambazi na wizi wa wazi wazi. Lazima mahubiri yao yachunguzwe na wanaokiuka maadili, sheria na taratibu washughulikiwe mojawapo ikiwa ni kuwapiga marufuku hata kuwatupa lupango.”
            Msomi Mkatatamaa anakula mic “ushauri huu umekuja kwa wakati wake. Kwanini tuwawajibishe watumishi wa umma kama vile vihiyo, watumishi na wanafunzi hewa wakati tuna wachungaji wanaohubiri mahubiri hewa na hasi? Napendekeza wachunguze mapato kama ni ya kweli na kama sadaka zinatumika vizuri na si kupigia ulabu kama ilivyotokea  kwa mzee wa mipako  hadi akapayuka na kupakwa kinomi.’
            Anakohoa na kuendelea “wachunguze tabia binafsi maana wapo walevi, mafisadi, wazinzi na kila aina ya matapeli. Wachunguzwe elimu zao kubaini vilaza na vihiyo. Wachunguzwe biashara zao wapo wauza bwimbwi na utumiaji misamaha ya kodi kujineemesha kwa kupitisha bidhaa za wafanyabiashara wezi wanaowatumia. Wachunguzwe historia zao maana wengine hata si wana kaya bali wakimbizi wa kiuchumi toka kaya jirani. Hapa ni kuchunguzana ili kuepuka kuchuuzana kama ilivyokuwa chini ya tawala zandiki zillizopita ambazo nazo zinapaswa kuchunguzwa na kutumbuliwa bila huruma wala kulindana.”
            Mgoshi Machungi anakatua mic “ningependa nimchomekee askofu Mokiwa kwa kupanua wigo wa uchunguzi. Hapa lazima tiwachunguze hata maisha yao binafsi ikiwezekana tiwatoze kodi na kukagua shuhui zao. Napendekeza wakaguzi wa fedha za umma wawe wanawakagua hawa jamaa ii kuepuka kuendeea kuwabia wachovu watu na kutajiika wakati sisi tikipigika kwa ukapa. Niseme wazi. Nakubaiana na wae wanaoita huu kuwa aina mpya ya ufisadi na ujambazi wa kumtumia Mungu.”
            Kanji hajivungi. Anakwanyua mic “mimi iko sangaa sana. Naona chungaji hubiri lakini hapana nafanya kazi. At the end nakuwa tajir sana. Nazidi hata ile nafanya biasara. Sana napata wapi juluku? Iko uuza neno na kupata juluku au iko biasara nafanya sirini?”
            Mpemba anakamua “yakhe hapa unkuna kweli kweli. Hata mie nshangaa kuona watu wasiofanya kazi yoyote isipokuwa kupiga kelele kuishi kwenye mahekalu, kununua hata madege na kuishi maisha ya kikwasi. Hapa lazimu iwepo biashara waniyofanya nyuma ya pazia wallahi.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anampoka Mpemba mic na kudema “kumbe hamjui! Baada ya dokta Kanywaji kuwabana wapigaji, sasa dili limebakia kuwa kuanzisha madhehebu ya dini. Hapa ndipo hitajio la kuchunguza maisha yao binafsi linakuwa muhimu. Lazima wataje vyanzo vya mapato na matumizi yao hasa wakieleza zinapokwenda sadaka. Hamkuona mmoja alivyofikishwa kwa pilato akidaiwa kuiba bilioni 15 za waumini? Kimsingi, hawa hawana tofauti na waganga wa kienyeji. Hawahubiri kuchapa kazi, uadilifu wala ukweli bali uponyaji utadhani kaya nzima ni ya wagonjwa. Wapo matapeli wanaojifanya kuombea ndoa, biashara hata elimu bila kujua kuwa ufanisi wa mambo haya hutegemea juhudi na si maombi.”
            Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea da Sofi na kusema “wao wenyewe wanapaswa kuombewa kwa ushirikina na uganga wa kienyeji na uganga njaa wanavyofanya. Na niseme hapa.  Kama kweli kuna pepo, hawa hawataingia. Wataingiaje wakati wametengeneza pepo zao hapa duniani? Kama pepo hii ipo sitaingia kama nitwakuta hawa wezi wa majoho kusema ule ukweli.”
            Mheshimwa Bwege anapoka mic “msemayo ni kweli. Nakubaliana nawe Mbwamwitu. Hawa wezi walishajitengenezea pepo zao hapa hapa duniani kwa kuwaibia wachovu. Angalia migari, mijumba na wengine midege wanayoangusha wakati Yesu wanayemhubiri alikuwa kapuku wa kutupwa. Je wanamhubiri Yesu yupi zaidi ya farao tajiri mwenzao? Biashara ya kuchuna inalipa. Unajenga duka na kuliita nyumba ya ibada. Unaweka mabenchi na wajinga wanafurika kulipa kodi wakidhani ni sadaka. Miaka nenda rudi wanamchangia Mungu. Mungu gani maskini asiyejajirika pamoja na kupewa sadaka miaka yote hii. Je yeye atatoa lini? Haiwezekani Mungu akageuzwa pakacha lisiloshiba wakati ukweli Mungu mwenyewe ni hao hao wanaowanyonya wachovu wa kaya hii. Ama kweli wachovu hawa wanahitaji ulinzi wa lisirikali hata kama wanaibiwa kwa ujinga wao na kutojiamini.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita mzee wa Upayuko akiwa amelewa chakari akitukana na kumwaga radhi! Acha tumtokee na kudai arejeshe chetu!
Chanzo: Tanzania Jumatano leo.

No comments: