The Chant of Savant

Saturday 13 August 2016

Mlevi aanza kuhisi anaanza kulewa madaraka

Man And A Half
Baada ya walevi kufanya makosa kwa kunichagua kuwa kiongozi wao, walisahau kitu kimoja muhimu. Walisahau kuwa walevi–hasa wana politiki– huwa hatabiriki wala kuaminika. Sawa na mwana politiki yeyote, baada ya kukaa kwenye kitu cha utukufu–nikiwa nimesheheni utukufu wangu–najihisi kuanza kulewa–si kanywaji bali madaraka. Najihisi kama mimi si gendaeka tena bali muungu-mtu ambaye hakosei wala hapaswi kukosolewa. Katika kujitathmini, nimejikuta nikihisi kuwa mimi ndiye kijogoo pekee kwenye kaya ya walevi. Waliobaki wote ni tetea wanaopaswa kunisikiliza, kuniamini na kupokea amri toka kwangu, tena kwangu pekee. Hivyo, zaidi yangu, hakuna anayeruhusiwa kufikiria kuwika achilia mbali kuwika. Wika nikusikie na kukukata hicho kidole na ushungi vinavyokupa kiburi. Kwa wale ambao hawajapata wala kuelewa somo, tafadhalini, nawajulisha kuwa Danganyika ina jogoo moja tu linalopaswa na kuruhusiwa kuwika yaani mimi munene wa wanene na mkuu wa wakuu. Yeyote anayetaka kuwika angoje nipige miaka yangu kumi ndipo afanye hivyo. Hivyo, kwa usalama wa maisha na ulaji wake anapaswa kufanya kitu kimoja tu–kuramba makalio na viatu vyangu na kutenda nitakavyo vinginevyo atakoma na kukiona cha mtema kuni. Nani hajitaki huyu usawa huu wa kulewa madaraka? Najua wengi wanadhani wataniingiza mkenge kwa kucheza na kuimba nitakavyo wakati kimsingi wanatetea ulevi wao. Mie sijali, uwe  unafanya kweli au kuzuga, ilmradi unakubali kuwa mimi ndiye kijogoo pekee anayepaswa kuwika, sijali huo usanii na usaliti wako kwa roho yako.
Kama haitoshi–baada ya kulewa ulaji sana–najihisi kujua na kuweza kila kitu kwenye kaya ya wadanganyika na walevi. Hivyo, amri zanguhisia na mawazo yangu ni sheria zisizopaswa kupingwa wala kuhojiwa. Kuhakikisha hili linatimia bila kukwama, nimeamuru walevi wengine wanaojitiatia kunipinga–eti kwa kuwatetea walevi wengine ambao hata hivyo, ni wangu tokana na kuwa mkuu wa walevi wote bila kujali nani alinipa au kuninyima–wafunge mabakuli yao vinginevyo nitawatia adabu. Wanapaswa kufahamu kuwa mimi najua kila kitu; na lolote nipangalo, lazima litekelezwe bila kusuasua, kuhoji, kushuku wala kuuliza maswali. Walevi walizoeshwa kudekadeka na kujipayukia hovyo hovyo na watakavyo. Kwangu hili halikubaliki.  Anayepaswa kusikika ni mmoja yaani mimi mlevi mkuu mwenye mamlaka na ulaji wote mikononi mwangu na sirikali yangu. Hata chama changu kilichoingia mkenge kikanidhamini hakifui dafu hata nisingekuwa mkiti wake. Mimi ni Alpha na Omega, mwanzo na mwisho, mbele na nyuma, kulia na kushoto. Ukitaka uwe salama, sikiliza na zishike amri zangu vingenevyo unahatarisha maisha yako.
Kama alivyowahi kusema Dan son of Mwai Kibaka kule kwenye kaya ya Nyayo na nyang’au, “Chini ya mzee Jomo nilikuwa naimba kama kasuku. Sasa nimepata ulaji. Kwanini nanyi msiniimbie kama kasuku?” sasa nasema, “Hapa ni kuimba tu.” Na hii ni amri; siyo ombi. Kama wahenga wa Kirumi walivyosema “Roma Lucuta est, causa finita est” yaani kilichoamriwa Roma ni mwisho na hakina rufani. Kama bi nkubwa wa Ku-Tulia pale mjengoni, langu lazima lisikike na kutekelezwa bila kusuasua wala kuwazawaza. Hivyo, wale wote wanaoota mchana kudhani watapingana na mimi wajiandae. Kwanza, wajue mambo muhimu yafuatayo:
Mosi, mimi nina shahada ya uzamivu ya utawala na ubunifu PhD in Creativity and Leadership.
Pili, wafahamu kuwa kila ninachopanga na kusema ni sahihi na hakina shaka yoyote.
Tatu, waelewe huu si wakati wa siasa bali kutekeleza yale niliyojipangia kwa ajili ya walevi.
Nne, waelewe kuwa kwenye kuwania nafasi hii ya kiongozi wa walevi, niliwashinda hawa wanaojitiatia kunikosoa chini ya kisingizio cha domoghasia. Ninataka mambo muhimu matatu yaani:
Wacheze, wafikiri na kutenda nitakavyo. Lazima kila mmoja acheze ngoma niamuruyo na si ngoma yake. Japo unaweza kuuita huu ulevi uliopindukia, kimsingi, ni utawala uliotukuka na kujitenga na utukutu wa domoghasia na ghasia nyingine. Nataka kaya yetu ya walevi iwe Bongolalaland kweli kweli aka Danganyika ambapo hakuna atakayedanganya tena isipokuwa mimi msemakweli. Ninachopanga, kuamuru na kuwaza mimi ndicho kinachofaa; na huu ulaji nimepewa na Mungu kupitia wapika kura ya kula. Kwani, kuna ubaya gani kula hata ikibidi kuwala wote? Kwani, mimi ni wa kwanza au wa mwisho kwenye zama hizi za kuburuzana?
Kwa vile nafaidi ulevi wangu wa madaraka, natoa fursa kwa wote wanaosoma waraka huu ambao umevuviwa na Muumbaji mwenyewe watafakari na kuwa tayari kutekeleza niwaamuruyo na niwaambiayo. Huu ndiyo uhuru wa kutumia madaraka. Nisisikie mlevi yoyote akisema eti mimi ni imla au dikteta. Dikteta gani wa kuchaguliwa tena kwa kishindo? Kama asemavyo munene fulani, meseji sent and received. Hivyo, namalizia kwa kusema wazi kabisa kuwa huu ni wakati wangu wa kufanya vitu vyangu. Sitaki wapingaji wanijazie mbu. Nitawatumbu…we! Koma na ukomae.
Sitaki niseme mengi leo. Acha niwaage kwa kuwataarifu na kuwaonya kuwa atakayekaidi ujogoo wangu ajue ameumia. Siko tayari kuona walevi wakinikwamisha kwa kuhoji au kupinga maagizo, mawazo, mipango na ndoto zangu hata kama ni za kukurupuka au za mchana.
Inshara tuonane wiki rijaro. Ni mimi lais wenu ambaye nimefulahi kufikisha ujumbe wangu. Jitu Pande Makwelini aka JPM.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: