The Chant of Savant

Saturday 11 June 2016

Mlevi kutia timu mjengoni na michupa


            Baada ya Ana Makidamakida kuachia ngazi baada ya kuvurunda Njengo, walevi walidhani ubabe mjengoni ungekuwa ndiyo mwisho. Kumbe tulinoa. Hatukujua kuwa atakuja yule ambaye hajaTulia kutembeza undavandava tena kishenzi zaidi ya Makidamakida! Kutokana na upuuzi huu, Kijiwe kimeamua kulaani kwa sana kikiwaunga mkono wahishimiwa wa upingaji kwa kumsusia upuuzi wake.
            Kwa vile mjengo si mali ya gendaeka wala mama yake au murumewe, Mlevi nimeamua kutia timu kule kwenda kutoa somo. Najua washikaji zangu akina Kitwangaji na Mlingaji watanipa tafu. Tutakwenda tuuchape mma na kupaga misokoto kibao ili tufyatuke na kumfyatukia  kama siyo kumfyatua huyu anayehitaji kutulizwa ajue kuwa Mjengoni siyo sehemu ya kufanyia uhuni uchwara wa kubeba chata fulani huku akiwaumiza wapingaji.  We ambaye hujaTulia, unafanya utukutu kwenye mjengo mtukufu siyo? Nitashughulikia hadi upepewe na kutulia kama siyo kuzimia. Hujui kuwa zama za Njaa Kaya za kitwahuti zimeishakuwa historia kwenye kaya hii ya walevi? Wakati wenzio tunakunywa kanywaji na kulewa eti wewe unalewa madaraka siyo? Shame on you!
            Kwanza nashangaa. Huyu babie amesomea sharia gani au PhD yake ni ya kugushi? Haiwezekani wapingaji wawatetee wasomi walioonewa halafu muishiwa anayeitwa msomi atie ngumu. I am going to lunge at the lady without any excuse. Kama ni PhD nami ninayo hata kama ni ya kilevi. Kwanini msomi anashindwa kuelewa somo dogo na utawala bora wa sheria unaotegemea mgawanyo wa madaraka?
            Unapowatimua wawakilishi wa walevi, unakuwa umewatimua walevi ambao kimsingi ndiyo wanaolipa marupurupu yako. Tumechoka na watendaji wanaotutumia badala ya kututumikia. Hivyo basi, simung’unyi wala kuzungusha maneno. Huyu hajaTulia; na apaswa kutulizwa kwa kutumbuliwa; na siyo kupepewa kama yalivyokuwa mazoea chini ya Njaa Kaya aliyefuga kila aina ya ujambazi. Kwani naye ni jipu tena linalonuka. Hatuwezi kuendesha mjengo kwa mapenzi ya watu binafsi badala ya sharia tulizojiwekea. Nawapongeza wapingaji kumsusa kidhabu huyu anayeonyesha ulimbukeni kwenye ofisi ya walevi.
            Kwa vile sisi ni wapenda amani, tunamtumia shinikizo. Asipoomba msamaha na kurejea kwenye mstari, tutamtokea na michupa ya gongo ajue tulivyochukia kichizi. Hata njiwa akishambuliwa anaweza kujitetea pamoja na kusifika kwa upenzi wake wa amani. Nasi kadhalika, tukiendelea kuchokozwa kwa kufukuziwa wawakilishi wetu, tutatia timu mjengoni na patachimbika bila jembe ukiachia mbali kutokalika.
            Huyu bibie kama anataka ukada basi aende makao makuu ya chama na kutafuta ulaji huko lakini si kwenye mjengo ambao ni taasisi inayopaswa kuwa huru na yenye kujitegemea. Inakuwa aibu kuliko hata unavyoweza kueleza kwa mtu kihiyo kutumika. Kwa sasa, kusema ukweli; sioni tofauti ya kihiyo Makidamakida na hyu ambaye hajaTulia. Kwanini hataki kwenda kumuuliza mwenzie Makidamakida jinsi Mlevi alivyomshukia hadi akatia adabu? Au anadhani mlevi ni wa jana kama yeye? Na kama ni kubukua, mlevi si haba; amepiga vitabu tena ughaibuni kwa sana tu. Mbukuzi gani asiyejua kuwa wakati umebadilika au anayeshindwa kusoma alama za nyakati wakati maandishi yake yako bold pale ukutani?
            Kutokana na uhuni na undavandava unaotembezwa mjengoni tena bila sababu ya msingi zaidi ya ujinga na unazi wa kitoto, nitakwenda kule kutoa somo kwa wahishimiwa wasirudie kosa la kukubali muishiwa yeyote wa kuteuliwa kugombea U-microphone au unaibu wake. Muishiwa wa namna hii asiyejua adha na kazi ngumu ya kuwashawishi wapika kura ya kula wakupe ulaji, anaweza kuchukulia nafasi hii kama ya kufanya majaribio kama ilivyotokea hivi karibuni kiasi cha kuniudhi na kunilazimisha kwenda kuweka mambo sawa mjengoni. Kukubali mtu asiyewakilisha yeyote isipokuwa tumbo lake ni kujihujumu hasa ikizingatiwa kuwa muishiwa kama huyu wa sasa hawezi kuwaheshimu wahishimiwa kwa vile yeye si mhishimiwa bali muishiwa hadi akaingia mjengoni kwa kubebwa. Sijui kwanini fyatu Mlingaji hatajamtolea uvivu na kumuita baby ili naye audhike tuone kama ataususa mjengo kama wale walioitwa babies kikawashuka hadi kususa mjengo?
            Kitendo cha kuugeuza mjengo sehemu ya kulindana kivyama ni jambo la kizamani. Ni kinyume na demokrasia hata kama ni ya maigizo na kilevi. Usawa huu utamburuza nani wakati kinachotakiwa ni kujadiliana na kukubali kutokubaliana? Upuuzi unazidi kuchusha, kuudhi na kutapisha sana hasa unapofanywa na yule anayeitwa mbukuzi. Heri kihiyo anayefanya ukihiyo wake kuliko mbukuzi anayefanya ukihiyo kama kihiyo. Mbukuzi anayefanya ukihiyo ni kihiyo hata angeitwa daktari au porofwesa kama akina J4 Majembe na Shcool Kawa-dog walioua elimu. Huyu hana tofauti na Dokta Kamanda wa Zenj zama zile akitembeza undavandava asijue kila jambo lina mwisho. Huyu hana tofauti na akina Profwesa Anae Kajuamlo aliyeingizwa mkenge na tapeli la Escrew. Wala hana tofauti na maprofesa waganga wa kienyeji na matapeli wengine wanaojiita madaktari wakati udaktari wao ni wa kughushi kama akina Emmy Nchimvi, Merry Nyagu, Makorongo Muhanga, Diddie Makalio aka Masssaburiii, Dororos Kamara na wengine wengi waliotuhumiwa kughushi Njaa Kaya akawanusuru kwa ukihiyo wake.
            Namalizia kwa kumuonya huyu dogo asingoje nimshughulikie hadi apepewe ili atulie. Awaheshimu wahishimiwa walioko mjengoni kwa kutumwa na walevi. Message sent.
Chanzo: Nipashe.

No comments: