The Chant of Savant

Wednesday 22 June 2016

Kijiwe chamkaribisha Pumba kijiweni

Baada ya kuisha na kuishiwa kiasi cha kujirahisi, Kijiwe kimemuonea huruma Profwedheha Ibra Pumba kuja kujiunga nacho na kupiga kahawa badala ya kuendelea kujivua nguo.
Mpemba analianzisha, “Yakhe mmensikia yule porofedheha alokikimbia chama cha Kafu halafu eti ajirudisha ataka aendelee kuwa mwenyekiti? Wallahi mie kama atakubaliwa kurejea hiko cheo naregesha kadi yangu. Itakuwaje chama kigeuzwe choo ambapo yeyote ajisikiaye haja ya kuingia huingia humo?”
Mgosi Machungi anachomekea, “Huyu waa isitipe tabu. Kama aitaka taaka akapewa anaudi kufanya nini wakati wameishamchezea na kumtupa kama ganda? Uzui nimesikia Kafu wakisema kuwa huwa hawana taala rejea. Abaki huku huko na hao hao waiomdanganya na kumchezea haafu wakamtema. Nani anataka mabaki jamani?”
Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Wahenga walisema; adui yako muombee njaa. Ama kweli njaa kitu kibaya. Yaani prof mzima unaamua kujivua nguo hadharani bila hata kufikiri japo kidogo! Sijui nani walimdanganya huyu ndugu yetu kiasi cha kujigeuza pumba kirahisi hivi? Ama kweli kuchamba kwingi kuondoka na  mavi! Kwanini hakutumia usomi wake lau kuangalia mbele hata kama ni meta moja? Nijuavyo mimi, huyu jamaa hatafanikiwa.”
Anapiga chafya mara mbili na kuendelea, “Ushauri wangu wa bure ni kwamba arejee shule akapige chaki kama bado anahitajika; kama hakuna anayemhitaji basi arejee kijijini kwake akalime tumbaku au mahindi mchezo uishe.”
Dada Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Ama kweli hujafa hujaumbika; usipoangalia unaweza kuumbuka. Nikikumbuka nyodo za jamaa yetu akijiondoa kwenye ulaji sina hata hamu wala la kusema zaidi ya kumshauri atafute shughuli nyingine ya kufanya.”
Mbwamwitu anachomoa mic, “Mie namshauri aje hapa awe akitupa somo la jinsi ya kunywa kahawa kiuchumi.”
Mzee Maneno anamnyang’nya mic Mbwamwitu, “Jamaa yangu shushu alinitonya kuwa jamaa aliahadiwa uwaziri wa njuluku kama angejitoa Kafu wakati ule asijue alikuwa akiukwaa mkenge mchana kweupe. Sijui kwanini baadhi ya wasomi wetu wanaonyesha ukilaza hata kwenye mambo madogo? Ama kweli tamaa mbele mauti nyuma,” anamalizia akimpa kikombe muuza kahawa amuongezee kahawa.
Mijjinga anaamua kutia guu, “Mie nadhani mnaomshangaa profwedheha Pumba mnakosea. Kwani, najua kinachomsukuma ni kudhani kuwa kile chama ni mali ya wakubwa wake wanaoweza kukitumia kama NGO kujipatia ulaji. Sioni tofauti kati yake na wale walioingia ndoa ya mkeka na wabaya wao wakaisha kutumika kwa muda na kubwagwa; na sasa wanalialia wasijue mustakabali wao. Kumbuka hii Bongo jamani.”
Mheshimiwa Bwege naye anatia guu, “Japo wengi wanadhani mwenye jina la Bwege ni mimi peke yangu wasijue ni kinyume chake, wapo mabwege wa kweli kweli kweli. Huwezi kujiuzulu kwa hiari yako ukatagemea kurejea kwa hiari yako. Huu ndiyo ubwege wa kweli achia huu wa jina. Kwanza, siamini kama Kafu wameisha na kuishiwa kiasi hiki kiasi cha kupwakia matapishi ukiachia mbali mabaki. Pili, anataka kurejea kufanya nini wakati yeye, kama kamanda wa vita, alijiuzulu wakati majeshi yakielekea vitani? Sasa vita imekwisha eti anataka ukamanda tena. Hii akili au matope au wehu tena wa mchana?”
Kapende aliyekuwa akibofya kijisimu chake anaamua kula mic, “Hata mimi simshangai huyu nyanda. Nadhani ameshindwa kutofautisha vyama vya mfukoni na vyama vya wananchi. Kwanini msomi aliyekubuhu kama huyu hajitofautishi na kina Joni Cheo, Gus Mlemavu na Fahamu Duvutwa? Alidhani Kafu ni NGO kama zile za wake wa marahis kutumia kujitengenezea ulaji kirahisi hivi? Kwa alivyoishiwa hata akina Mlemavu na wababaishaji wengine hawamtaki.”
Kanji anaamua kukamua, “Sasa hii pumba kwanini napoteza muda. Kama nataka laji kwa chama basi unda chama yake. Sasa kama Kafu nasema hapana regea yeye, yeye iko gangania nini? Kama veve nauzuru chamani na vatu haiko taka veve tena nenda unda chamani yako tumia kama dukani yake chezo kwisha.”
Mipawa aliyekuwa akitabasamu muda wote anaamua kula mic, “Mimi nitachukua mrengo tofauti. Badala ya kumlaumu Pumba kwa masahibu yaliyomkumba tokana na upumba wake, namshauri atulie kwanza. Aje hapa kijiweni tumpe michoro ya kuweza ku-survive katika hali hii. Hata hivyo, kwa muda wa miaka mingi aliyokuwa mwenyekiti bila kuleta mabadiliko yoyote, anapaswa kukubali kuwa zake zimekwisha; na lazima wengine waje wajaribu. Nadhani hili halimhusu Pumba pekee. Hata maalimu Madevu naye anapaswa kuwapisha wenye nguvu na mawazo mapya kukwamua chama kama kweli wanalenga kushika dola. Hata hivyo, kama wanataka kutengeneza dola kwa mgongo wa chama, wawili hawa wanaweza kuendelea na biashara yao ya siku zote.”
Msomi anakula mic,”Dk Mipawa umetoa pwenti kubwa sana. Umeingia ndani zaidi kwa kukangalia mfumo mzima wa ulaji wa kisiasa kwenye vyama. Kama vipindi vya urahis ni viwili tu, inakuwaje mtu aongoze chama kwa zaidi ya vipindi viwili yaani miaka kumi? Hata Chama Cha mafisadi (CCm) kimewapiku katika hili. Nadhani wakati wa kuandaa benchi ya Pumba hapa kijiweni umewadia.”
Kabla ya kuendelea simu ya Msomi ililia. Anapokea na kusema, “Halo profedheha Pumba, unasema eti unataka kujiunga na kijiwe chetu? Basi wakaribishwa hata sasa.” Msomi anakata simu na kutupa taarifa kuwa Pumba ameamua kujiunga na kijiwe lau kujadili yanayoendela kayani.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: