The Chant of Savant

Wednesday 4 May 2016

Kijiwe chamchimba Makufuli

Baada ya kuona mikwara, vimbwanga, mbinyo na hekaheka za Dokta Kanywaji Makufuli na kukunwa navyo, Kijiwe sasa kimeamua kumtonya kama si kumchokonoa. Kinashangaa–baada ya kuongoja bila majibu–ni kwanini majambazi ya Escrew bado yako uraiani yakitanua wakati wachovu wanatanuliwa na matatizo hasa ukapuku uliosababishwa na zali kama hivi chini ya Njaa Kaya ambaye kingependa naye anyee debe.
            Mpemba ndiye analianzisha tena kwa methali na nahau. Anaingia akiwa amewekea tarabushi yake na kanzu mardadi kweli kweli. Anakula mic baada ya kuamkua, “Yakhe mie nina hoja leeeo. Nataka Kijiwe hichi kitukufu kitoa hoja kwa rahis Joni Kanywaji Makomeo atie makomeo kwenye kashfa ya Escrew. Sijui wenzangu mwaonaje?”
            Kapende hangoji. Anaramba mic, “Ami hapo umepiga panapopaswa haswa. Hata mie nashangaa. Sioni makeke ya Kanywaji kwenye zali hili linalotusababishia mateso na matatizo lukuki kana kwamba kaya inaendelea kuwa Shamba la Bibi wakati Dk Kanywaji amejitolea kuirejesha kwenye mstari.”
            Msomi Mkatatamaa leo hangoji kuja mwishomwisho. Anakula mic kama hana akili nzuri, “Ami lazima nikupongeze kwa kuleta mada hii. Morally, we must make a stand. Hata nami nashangaa hivi vimbweka vyote vya kutumbua majipu wakati majipu sugu tena yaliyo wazi hayaguswi. Lazima tumbane Dk mwenzangu Kanywaji atoe msimamo wake kuhusiana na ujambazi wa Escrew. Bila kufanya hivyo, hakuna atakayemuelewa.”
            Kabla ya kuendelea kuneme mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu, “Jamani tunamuonea Kanywaji wa watu. Hivi mnategemea aguse uoza wa chama wakati hakijakabidhiwa mikononi mwake? Ngojeni wampe rungu uone atakavyobonda nalo hata wale usiotegemea. Japo ngoja ngoja huumiza matumbo, haraka haraka pia haina Baraka. Subira yavuta heri au vipi? Nawaamba walo juu walo chini wasikie au vipi? Leo twaronga kwa methali msoipata mtajijuu au vipi?”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua naye kutia timu mapema, “Ama kweli Bwege leo umefika wakati wa farasi kufingiana nyama na nyangwa! Leo twaamba kwa mithali mafumbo na nahau au vipi? Nami nakuunga mkono mheshimiwa kwa kutaka subra ifanyike ile tusifanye haraka tukaula wa chuya japo twataka kumaizi kutosubiri kupita kiasi tukaishia kula mbovu badala ya mbivu. Mwanakwetu nakuunga mkono. Tungoje. Kwani mambo mazuri hayataki haraka.”
            “Bengh’we, mnanikumbusha nahau na mwalimu wa Kiswahili zama zile za mwaka arobaini na saba. Sijui kama mwenzangu Kanji anaipata hii. Hata hivyo, niseme wazi, Escrew si jipu bali kansa. Na bila shaka ndilo litaamua hatima ya Dk Kanywaji atake asitake.” Anazoza Mipawa.
            Mgosi Machungi anaamua kula mic, “Wae wanaoona kama afiki yangu Kanji anaachwa Soemba hawajui. Hawa jamaa wanajua kiswahii kuiko wengi kama akina Mua. Sema hujifanya hwakikijui ii waonekane tofauti.”
            Kanji naye anaamua kutoka mafichoni. “Veve acha chezo na mimi. Iko jua Swahili sana kuliko veve nakuja kwa gari na jicho moja. Hata kama lafuzi yangu Hindi, bado iko jua Swahili sana. Mimi zaliwa taa ya India pale nakutana na Indira Gandhi house no 11. Iko jua veve hiyo?”
            “Ama kweli gabacholi ni gaba kweli. Mimi nakutetea ili usiachwe nyuma kumbe unanikandia na kunizodoa. Nenda kawazodoe akina Escrew na akina Karasinga, Muongo na Njaa Kaya wanaofumbiwa macho wakati walikwapua njuluku ya Escrew,” anajitetea Mipawa.
            Msomi anarejea tena, “Kwa vile leo tumeamua kumtwangia–na si kumbeep–Dk Kanywaji, lazima tutoe ya moyoni. Ukiachia mbali kashfa ya Escrew, kuna jipu jingine tena lilolgeuka kansa. Hili si jingine bali kashfa ya UDa. Lazima nayo aitumbue hasa ikizingatiwa kuwa baada ya Chama cha Mafisadi kuchapwa kwenye uchaguzi wa meya wa Bongo, kila kitu kimefunguka–kiko wazi–tayari kufaidiwa. Asiishie kwa Escrew. Atumbue hata UDa. Maana juzi nilimsikia mstahiki Meya akisema kuwa UDa ni mali ya wachovu na si mali ya mafisi na mafisadi na Masimba na Marizi au vipi?”
            Mzee Meneno anaamua kuchomekea, “Kumbe nyie hamjui! Dk Kanywaji ana nia na mipango mizuri na kaya yetu sema wenzake chamani wanataka kumkwamisha kwa kuhofia watapoteza ulaji na wengine kuozea lupango. Kuna ninaowajua ambao ni mazungu ya unga ukiachia mbali wale walioko nyuma ya hizi kashfa zote mnazoshuhudia. Inataka subra na uvumilivu vinginevyo atashindwa. Mie namuunga si mkono bali mikono na miguu. Tumpe muda tutakuja kuambiana, “yako wapi sasa mliolewa madaraka mkasahau kesho? UDa nina imani itarejeshwa.  Wale walioiiba na kuitwaa kwa kutumia madaraka yao au ya wazazi wao wakae mkao wa kuliwa usawa huu. Nadhani wengi mmesahau kuwa bila Dk Kanywaji kuamuru CCM wasichakachue tusingekuwa na meya wa upingaji au vipi?” Walimwengu ni rahisi kusahau hasa usawa huu wa kukata tamaa na ngoa. Tuvuteni subira ndugu zangu.”
            Mijjinga aliyekuwa akisiliza kimya kwa muda mrefu anaamua kutia guu, “Waheshimiwa nakubaliana nanyi. Lazima tumchokonoe Dk Kanywaji ajue kuwa nasi tuna mawazo ya kuweza kuendesha kaya yetu. Mie simwambii mengi. Ninachotaka sasa ni Katiba Mpya ili kuweza kusaidia katika mapambano haya ya kurejesha kaya kwenye mstari. Escrew, UDa na majipu mengine yanayojulikana lazima yatumbuliwe kwanza. Hapa ndipo nitakapoamini kuwa Dk Kanywaji hamuogopi gendaeka yeyote na wala hafanyi usanii.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Kariuki aliyekataa mshahara kwa vile anapata marupurupu ya kutupwa. Acha tulitoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: