The Chant of Savant

Friday 18 March 2016

Makufuli mtumbue jipu Lukuviii


            
Baada ya muishiwa waziri wa Udongo Bill Lukuviii kuja na mpya kiasi cha kumlewesha Mlevi hata bila kanywaji na tubangi, imebidi lau niseme ili wote na yeye wajue kuwa sikuingizwa mkenge. Hii itasaidia na wengine wasiingizwe mkenge katika msako huu wa umaarufu wa shilingi mbili.
            Bila hata chembe ya aibu, Bill alikaririwa na wambea akijisifu kuwa alikataa mshiko wa bilioni tano. Hebu nirudie. Five billions doughs! Ngai, Zumbe na Ambuye! Kwa vile mlevi ni mtaalamu wa masuala ya jinai hasa kusema uongo, ilibidi nirejee kwenye maktaba yangu na kufungua makabrasha na shajala zote lau nipate pa kuweka uongo huu. Kwa lugha ya kisambaa hii huitwa cheap popularity ambapo mhusika hujitahidi kujipigia debe kama yule jamaa mbaguzi wa kwa Joji Kichaka aitwaye Don Drumpf. Mhusika hujikweza hata kujikweza kwenyewe kukiishia kwenye maanguko kama ilivyotokea kwa Bill ambaye leo namrarua bila huruma.
            Kwa vile mlevi ni bonge la gwiji la sheria, nitajaribu kutoa sababu za kutokubaliana na madai ya Lukuvii.
            Mosi, Lukuviii alificha majina ya wahalifu–aliowataja kama wafanyabiashara wakubwa–waliotaka kumshikisha mabilioni haya. Hawa ni wafanyabiashara wakubwa au wezi na wahalifu wakubwa tu? Je ni kwanini alificha majina ya majambazi kama hana lolote la kuficha? Je kuficha kwake na kutoboa vinatusaidia nini iwapi watuhumiwa wamefanywa kuwa top secret?
            Pili, kwanini hakuitaarifu ile kampuni ya umma ya kulinda na kupamba–sorry–kupambana na rushua (Takokuru) kama hakuna namna. Ina maana–pamoja na nafasi yake kubwa na nyeti kama hiyo–Lukuviii hajui kuwa sheria inamtaka kila mwanakaya anayekuta mtu anatenda au kujaribu kutenda kosa la jinai anapaswa–kisheria–kutoa taarifa kwa vyombo husika? Je Bill hakuwa na imani na Takokuru? Kama ni hivyo, kwanini hakuwatonya ndata lau wakaweka mtego na kuwanyaka hawa wanahizaya wanaoharibu kaya yetu?
            Tatu, Lukuviii alidai kuwa kuna mtandao wa matapeli tena aliwaowaita wawekezaji wanaolangua ardhi yetu na kwenda kufungua mabiashara makubwa Dubai na London. Je hawa ni wabongo au maabsii na makalu? Je hawa ni wawekezaji au wachukuaji? Je walipataje taarifa za siri ya sirikali kuwa Kigamboni kungekuwa dili kama nao siyo kuwa na sirikali yao ndani ya sirikali na siri kali ambayo Bill amejitahidi kuitunza? Pia, Lukuviii alidai kuwa kuna wakubwa waliojilimbikizia ardhi. Je Bill kama waziri mhusika, kwanini hakutaja majina yao na kueleza mikakati aliyo nayo ya kuhakikisha wanatumbuliwa jipu na kurejesha ardhi yetu? Je sheria ya kuzuia kuuzia wageni ardhi ilibatilishwa au kubadilishwa lini? Je kwa uzembe wote huu hapa Bill kajijenga au kujibomoa na kuonekana muongo na mzembe?
            Nne, Lukuviii–wa uzembe na habari zisizo na ukweli kama hizi–hajawa jipu linalopaswa kutumbuliwa mapema na Dk John Kanywaji Makufuli? Katika maajabu ninayongojea ni mawili. Mosi, Lukuviii kuendelea kuwa kwenye ulaji bila kutumbuliwa jipu na kutupwa nje kama Sifui. Na pili, kama Lukuviii hatajibu maswali yangu tena kwa majibu yanayoingia akilini. Asipofanya hivyo, nitatia guu ikulu mwenyewe kushinikiza atumbuliwe jipu na kuwataja hao waliotaka kumhonga. Atafichaje majina ya wahalifu waliotaka kutuibia walevi? Anadhani hii kaya ni mali yake peke yake kiasi cha kufanya jinai kama hii suala la binafsi?
            Tano, kwanini Lukuviii hakueleza uhusiano wake na hawa “wafanyabiashara wakubwa” ambao hadi sasa ni kitendawili anachoweza kutegua yeye mwenyewe?
            Sita, kama mtu mzima na kiongozi, je Lukuviii anaona alichofanya ni haki na sawa sawa? Je hawa jamaa wangekuwa wanapanga kuvunja nyumba yake au kumkaba bi nkubwa angeficha majina yao bila kuita ndata kuwashikisha adabu?
            Saba, je kwa kuwaficha, Lukuviii haoni kuwa amewasaidia na kuwapa hifadhi kiasi cha kusaidia uhalifu uendelee kutendeka? Je uhusiano na biashara ya Lukuviii na hao wenzake inaishia hapo au kuna mengi yamefichwa na kwanini na ili iweje na kwa faida ya nani?
            Nane, je Lukuviii–kuondoa ubishi na shaka–yuko tayari kutaja majina ya hao wezi wakubwa aliowapa sifa ya ufanyabiashara mkubwa?
            Tisa, je Lukuviii yuko tayari kueleza ni kwanini asitumbuliwe jipu kutokana na kushirikiana na wahalifu kwa kuficha majina yao?
            Je Lukuviii anajua madhara atakayoisababishia kaya kwa kushindwa kuwaitia Takokuru au ndata wakawatia mbaroni? Je anafahamu kuwa na Dk Kanywaji–licha ya kuaibishwa na kutiwa majaribuni–amechukia uzembe huu wa mchana tena bila sababu na kama zipo ziko nyuma ya pazia?
            Tumalizie kwa kumpongeza Lukuviii kwa angalau kusema. Maana, alipotuhumiwa kughushi sifa za kitaaluma na yule gwiji wa kuwaumbua vihiyo Keinerugaba Msematruth. Kwa nondo ninazomwaga hapa wala Lukuviii asipoteze muda kutishia watu. Kwani ninalo tabu lote la Keinerugaba liitwalo Orodha ya Mafisadi wa Elimu. Ni bahati nzuri, wote waliotajwa humo akiwamo Bill tena wakati ule akiwa mkuu wa mkoa wa Bongo walifyata bila kwenda mahakamani. Sambamba na kumpongeza, ningetaka ajitokeze lau kimasomaso akanushe madai ya Msematruth ambayo ameyaweka kwenye maandishi. Ama kweli madai ya Lukuviii yanaacha maswali mengi kuliko majibu! Kazi kwa Dk Makufuli kumsefue ili liwe onyo kwa wengine.
Chanzo: Nipashe, Machi 19, 2016.

No comments: