The Chant of Savant

Monday 28 March 2016

Barua ya wazi kwa waziri mkuu Majaliwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.             Mheshimiwa waziri mkuu,
Kwanza nakupongeza kwa kuteuliwa kuwa waziri mkuu. Pili, nakupongeza kwa juhudi unazofanya kupambana na uovu kuanzia bandarini hadi kwenye sekta ya ardhi.
Ndugu waziri mkuu, hivi karibuni ukiwa mkoani Kagera, ulifanya maamuzi magumu ambayo ni kuwanyang’anya ardhi mafisadi wa ardhi walioipata na kuihodhi kinyume cha sheria na wasiiendeleze katika wilaya ya Ngara. Hili ni jambo la kupigiwa mfano kama juhudi zako zitalenga kuwabaini na kuwashughulikia wote waliojilimbikizia ardhi.
Ndugu waziri mkuu, hivi karibuni waziri wa Ardhi, William Lukuvi alitoa madai kuwa kuna wafanyabiashara wawili waliohodhi ardhi kwenye eneo la Kigamboni waliotaka kumhonga shilingi bilioni tano ili awawezesha kuiuzia serikali ardhi waliyoipata kwa bei ya kutupwa baada ya kuwarubuni na kuwadhulumu wananchi. Lukuvi alikaririwa akisema kuwa wafanyabiashara wakubwa wawili walikuwa na jumla ya ekari 700 walizonunua kwa shilingi milioni tano kwa heka huku wakitaka kuiuzia serikali kwa shilingi 141 kwa heka.
            Ndugu waziri mkuu, baada ya Lukuvi kutoa madai haya –ambayo bila shaka yaliacha mashaka na maswali mengi bila majibu–wengi tulishangaa ni kwanini hakuwataarifu Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) au polisi ili kuweka mtego na kuwakamata wahalifu hawa. Kama haitoshi, Lukuvi alificha majina ya wahusika kiasi cha kujenga shaka juu ya ukweli wa madai na usafi wake. Kwa kuonyeza uzembe wa wazi, wengi wanamuona Lukuvi kama jipu linalopaswa kutumbuliwa na kuondolewa kwenye serikali ya awamu ya tano. Maana, ameonyesha uzembe wa wazi wazi na kutojua wajibu wake kama waziri na mtanzania kwa kushindwa kuripoti tukio la jinai. Wengi walidhani kwa mtu wa kada ya Lukuvi, angechukua hatua mujarabu na kuonyesha kwa vitendo anavyochukia na kupiga vita rushwa. Sijui kama hata rais ameuona huu udhaifu wa Lukuvi ambao tungetaka nawe uupige darubini na kumshauri rais nini cha kufanya dhidi ya waziri kama huyu ili liwe somo kwa wengine wanaofanyia kazi mazoea badala ya kufuata taratibu na kanuni.
             Ndugu waziri mkuu, tukirejea kwenye maamuzi yako ya wilayani Ngara ambapo hati za kumilki jumla ya ekari 7,700 zilifutwa, tunakutaka uchukue hatua hiyo dhidi ya wamilki aliowataja Lukuvi huku ukibaini wengine ambao wameishafanya mchezo huo au wanapanga kuufanya. Pia tungeshauri sheria ya uuzaji na umilkishaji ardhi wawekezaji irejewe na kurekebishwa ili kuziba mianya ambayo waroho wachache wenye madaraka na fedha wamekuwa wakitumia kuhujumu taifa huku wao wakitajirika wakati taifa linazidi kuwa maskini wakati lina raslimali lukuki. Kwa mfano, tunashangaa serikali–ambayo kisheria ndiyo mmilki wa ardhi nchini–kulanguliwa ardhi yake wakati ina mamlaka ya kufuta hati milki husika na kuchunguza namna hawa walanguzi wa ardhi walivyopata hodhi ya ardhi husika. Hili halitasaidia tu kupambana na hawa wanaojulikana. Pia, litasaidia kubaini mitandao yao iliyojazana kwenye ofisi za umma. Waziri Lukuvi alisema kuwa kumekuwapo wafanyabiashara hasa wawekezaji kuja Tanzania na kununua ardhi bila kuiendeleza huku wakienda kwenye mabenki na kuchukua mikopo kwenda kuanzisha miradi kwenye miji ya Dubai na London jambo ambalo licha ya kuhujumu taifa linawanyima watanzania ajira na huduma. Tungeomba umuite Lukuvi kwenye ofisi yako na kumtaka atoe maelezo ya kufanikisha kuwakamata wahalifu hawa pia ukimtaka aeleze kwanini–kama ni kweli alitaka kuhongwa–hakutaarifu vyombo husika viweke mtego wa kuwanasa? Pia umtake waziri Lukuvi akupe majina ya wahusika ili kubaini ukubwa wa tatizo na kulishughulikia.
            Ndugu waziri mkuu, pia tunakushauri uchunguze kujua hawa wawekezaji, wawe wa ndani au wa kigeni walipataje kununua na kuhodhi ardhi husika na nani aliwaambia kuwa Kigamboni ingekuwa na soko kubwa baadaye wakati miradi ya serikali ni siri?  Hili litasaidia kubaini watumishi wasio waaminifu wa serikali wanaovujisha siri za serikali na kuzitumia kuhujumu watanzania bila sababu zaidi ya uroho na ufisadi.
             Ndugu waziri mkuu, Lukuvi alikwenda mbele na kudai kuwa kuna baadhi ya viongozi waliojilimbikizia ardhi. Tungeshauri na hili Lukuvi aitwe na kulitolea maelezo ili uchunguzi ufanyike na kubaini wahusika walipataje ardhi husika na hatua zichukuliwe ilil kukomesha mchezo huu unaotokana na ubinafsi na ufisadi wa kutumia madaraka ya umma kwa kujinufaisha binafsi kwa baadhi ya maafisa wa serikali.
            Kwa vile umeonyesha umakini na juhudi kubwa katika kutatua matatizo ya wananchi, tunategemea hutaacha tuhuma na kashfa kama hizi zifutikwe chini ya busati jambo ambalo litaionyesha serikali yako kama yenye kupendelea na kugwaya baadhi ya wahalifu. Tusingependa dhana potufu kama hii iruhusiwe kujengeka ingawa kuizuia kutatokana na namna utakavyofanyia kazi madai kama haya.
            Tumalizie kwa kusema wazi kuwa tunaitikia wito wa rais John Pombe Magufuli wa kutaka watanzania wamsaidie kubaini na kupambana na ufisadi mambo ambayo yameikwamisha nchi yetu kimaendeleo ukiachia mbali kuigeuz shamba la bibi na kuiletea hasara na aibu. Wakati wa kufanya kazi kwa mazoea unapaswa kukomeshwa na kujenga uchapakazi unazingatia sheria, taaluma na maadili.
Ndugu waziri mkuu, tunaomba tuishie hapa kwa kutoa hoja.
Wasalaam.
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 27, 2016.

No comments: