The Chant of Savant

Friday 12 February 2016

Laiti watanzania wanamwelewa Dk Magufuli




            Wachambuzi wengi wamekwisha kuandika mengi kuhusiana na rais John Pombe Magufuli. Kila mmoja anamuelezea kwa kadri amjuavyo au ajuavyo hata kama si sahihi. Wapo wanaosema eti amekataa kwenda nje. Hii –nadhani –inatokana nay ale mazoea ya kuwaona watawala wetu waliopita wakipoteza fedha na muda mwingi –kila siku –kiguu na njia kwenda kuomba na kutanua. Hata  hivyo, binadamu hatuna wema. Akisafiri sana tunamwita Vasco da Gama. Asiposafiri tunaanza kuzua kuwa amegoma kwenda ughaibuni. Aende kufanya nini kama ana kazi nyingi za kufanya ofisini kwako? Azurure hovyo wakati alichaguliwa kuwahudumia na si kuzurura na kupoteza muda na fedha. Sijui kama ni kweli kuwa Dk Magufuli hataki kwenda nje au anaepuka safari zisizo na tija kwa taifa ambazo–mara nyingi–licha ya kulihujumu taifa hulidhalilisha. Lazima tubadilike na kujifunza kufanya mambo kwa namna mpya kama alivyowahi kusema rais wa zamani wa Burkina Faso, marehemu Thomas Sankara kuwa huwezi kutumia kanuni za zamani zilizoshindwa kutafuta majibu mapya ili hali unajua zilivyoshindwa.
Tokana na kuwa madarakani kwa takribani miezi mitatu bila kusafiri nje, wengine wamechorea vibonzo vya kuonyesha kuwa amegoma kwenda nje. Kimsingi, Magufuli anachofanya ni kuongoza kwa mfano badala ya maneno. Kwa wanaojua hali ilivyokuwa chini ya awamu za tatu na nne zilizooongozwa na marais waliokuwa mawaziri wa mambo ya nje kabla ya kuukwaa urais, walizoea kuzurura dunia nzima wakiombaomba misaada ya uongo na ukweli hata pasipo ulazima bila sababu za msingi. Wenye kufikiri wanaona mantiki ya rais kutozurura wakati akifuja fedha ya walipa kodi ilhali, kuna fedha nyingi ilikuwa ikipotea kwenye kukwepa kulipa kodi na misamaha ya kifisadi ya kodi. Magufuli ameamua kukataa kujidhalilisha kwenda ughaibuni kuombaomba na kujikomba wakati fedha ipo nchini ikiliwa na wahalifu wanaoshirikiana na maafisa wa seriakali wasio waaminifu na mafisadi. Hivyo, ameamua hizo fedha ambazo waliomtangulia walikuwa wakifuata nje wakati nyingi zinaibiwa nchini, akae ofisi na nchini azisimamie kikamilifu ili kujitosheleza na kuepuka laana na aibu ya kuomba wakati taifa limejaliwa kila aina ya raslimali.
Kitu kingine, huwezi kuwazuia wenzako wasiende kuzurura ughaibuni wakati wewe ukiwa ndiyo kinara. Vasco da Gama hawezi kuwa na udhu wa kuwazuia wadandizi na wazururaji wengine wasifanye kama yeye. Wahenga walisema kuwa jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Kimsingi, anachoonyesha Magufuli ni uongozi wa mfano wa kuigwa na walio chini yake. Ana mapenzi na mipango mikubwa kwa taifa. Tumpe nafasi na kumuunga mkono ili tuondokane na laana ya uombaomba usio na sababu. Wengi hupenda kwenda nje ili walipwe per diem hata kama safari zao hazina msingi wowote wala maslahi kwa taifa. Akihutumbia hafla ya kufungua mwaka mpya wa mahakama, rais Magufuli alisema kuwa nchi ilikuwa imefikia pabaya kiasi cha watu kuamua kwenda ughaibuni eti kufanya mikutano ya bodi.  Ni ajabu hata utawala uliopita ulikuwa ukifumbia macho ufisadi huu wa kijinga na kiroho.
Kimsingi, ujio wa Magufuli umeonyesha kuwa nchi yetu–tangu alipong’atuka baba wa taifa marehemu mwalimu Julius Nyerere–ilikuwa ima kwenye outpilot au ilikuwa ikitawaliwa na watu wenye akili za kutia shaka ukiachia mbali uzalendo wao. Magufuli amethibitisha kuwa si mbinafsi wala limbukeni wa kupwakia safari za nje huku akikwepa majukumu mazito aliyoapa kuyatimiza. Kilichobaki sasa ni kwa Magufuli kufumua mfumo wa sasa wa kijambazi na kuusuka upya ili uwe endelevu na wenye kujiendesha na kujitegemea hata akimaliza muda wake.
Hivyo, badala ya kumbeza na kumlaumu Magufuli kwa kuukataa uomba omba, tumsaidie na kumpongeza badala ya kumkatisha tamaa na kumuona kama mshamba.  Nadhani hii inasababishwa na ile hali ya kubariki ufisadi wa kimfumo kiasi cha maovu kushabikiwa kuliko mema. Hata viongozi wa nchi tajiri hawazururi hovyo pamoja na uchumi wao kuwa mzuri tu. Wanakaa ofisini na kuwatumikia wapiga kura na wananchi wao waliowaamini dhamana ya uongozi sawa na anavyofanya Magufuli. Badala ya kumuona kama mshamba, tumpongeze na kumpa moyo ashikilie uzi ule ule ili taifa liondokane na tabia ya uombaomba ijitegemee na kuheshimika.
Tumalizie kwa kumpa moyo na kumpogeza rais Magufuli. Tunawaomba watanzania wamuunge mkono kwenye jitihada zake za kulikomboa taifa ambalo liliangushwa na utawala wa kishikiaji na kijinga wa muda mrefu ambapo urais uligeuzwa chaka la maovu kama vile uzururaji ulioandamana na misafara mikubwa ya walaji wasio na sababu yoyote ya kuwa kwenye misafara ya rais. Watanzania walishazoea kufichwa hata majina ya waliokuwa wakiandamana na rais kutokana na kutofaa kwao kufanya hivyo. Kimsingi–pamoja na nia nzuri yake–wengi hawajamuelewa rais Magufuli na wakimuelewa, bila shaka, taifa letu litasonga mbele na kuanza kujenga utamaduni wa kuwajibika na matumizi mazuri ya fedha na raslimali za umma.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 14, 2016.

No comments: