The Chant of Savant

Wednesday 30 December 2015

Kijiwe chastukia wanaojitia kuombea kaya


            Baada ya kunyaka matangazo kuwa kuna wachunaji wana mpango wa kuiombea kaya, kijiwe kimekaa kama kamati kulaani upuuzi huu.
            Mgosi Machungi –kama kawa –ndiye analikoleza. Anaingia na kuamkua na kusema, “Jamani mmesikia wae matapei wanaotaka eti kuombea kaya kana kwamba kaya yetu ni maiti? Watatiombeaje kana kwamba sisi timekufa?”
            “Kwana hamjafa hadi kuhitaji Dk Kanywaji awafufue?” anauliza Mchunguliaji huku akichukua gazeti toka kwa Msomi Mkatatamaa.
            Msomi anakatua mic, “Mada yako Mgosi imekuja wakati wake ambapo rais Kanywaji anajitahidi kuwafundisha wachovu namna ya kujikomboa na kuondokana na uombaomba alioendekeza Njaa Kaya na Ben Tunituni Makapu. Tunaweza kujikomboa bila kuomba dua wala njuluku ughaibuni. Nadhani hawa wanaojifanya wanataka kutuombea kuna wanachotafuta kama si kutaka kuwa karibu na lisirikali ili wapate ulaji. Ila kwa Dk Kanywaji wamenoa. Wataomba lakini hawatapewa kibali cha kuwaibua waumini au kufanya biashara za siri kama ilivyokuwa.”
Kapende anakatua mic, “Usemayo Msomi ni kweli tupu. Kaya yetu ahitaji maombi bali maadili. Niliposoma tangazo hili,” anatoa gazeti linaloonyesha kuwa kuna mchungaji wa kibongo akishirikiana na wachungaji toka Ghana na Nigeria walikuwa na mpango wa kumuomba Dk Kanywaji na Kaya na kuendelea, “Eti hata wanigeria nao wanataka kutuombea. Si waombee kaya yao inayosumbuliwa na magaidi wa Boko Haram ukiachia mbali vibaka, mibaka, mafisadi na majambazi yenye madaraka?”
            Mijjinga naye anaamua kula mic, “Nadhani hawa wanaotaka kutuombea wanapaswa waache unafiki. Kwani ukitaka kumuombea mtu lazima utangaze? Mbona wanapoombea waumini wao wanaowatapeli hawatangazi magazetini? Kama kuombea ni big deal basi hawa wanaotaka kutuombea wanapaswa kuombewa kama si kuambiwa kuwa kinachoweza kuendeleza kaya yetu si maombi bali hapa kazi tu. Wamezoea kuwahadaa wajinga kuwa wanatenda miujiza wakati ni utapeli mtupu.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kukamua mic, “Jamani usiwanyime haki yao. Hawa jamaa kweli wanafanya miujiza kama vile kuwanyonya maskini kwa kuwatapeli kuwa wanaweza kubadili maisha yao. Pili wanafanya miujiza ya kutajirika bila kufanya kazi. Unadhani ni mchezo kuwa bilionea hadi wengine wakanunua vyopa bila kufanya kazi? Nadhani kama miujiza wanayosema, si mingine bali hii.”
            “Yakhe hapa nkupata sasa. Kumbe hata kuibia watu nako muujiza?” Mpemba anauliza.
            Mheshimiwa Bwege anajibu, “Ulikuwa hujui! Usingekuwa muujiza si wale wanaoibiwa au mamlaka zingehoji wanapataje ukwasi bila kuchapa kazi? Unadhani bila kuja Dk Kanywaji utapeli huu ungeisha?”
            “Sasa nimekuelewa. Hata hivo, nafurahi kuwa sasa mwisho wa miuya yao wawadia. Lazima wabanwe waeleze wanivyotengeza huo ukwasi wao wakati waendelea kuwaibia makapuku.” Mpemba anajibu.
            Mipawa aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kula mic, “Mwenzenu nadhani hawa jamaa walitumia mwanya wa kuwa na lisirikali zembe na fisadi nao kuiba kama wakubwa wake walivyokuwa wakifanya. Hamkuona yaliyojiri bandarini, TRA, Reli na kwingineko ambapo Dk Kanywaji na waziri mkubwa Katelephone waliposhupaa? Naungana na wanaotaka hawa wachunaji wanaojiita wachungaji kubanwa waeleze walivyopata ukwasi wao wakati hawatii mzigo. Bila kuwabana tutaendelea kutapeliwa.”
            Kapende anarejea, “Hakuna aliyenikuna kama Hamis Kigwaragwara aliyepiga marufuku utangazaji wa upuuzi uitwao tiba mbadala wakati nao umegeuka utapeli mtupu. Mijitu isiyo na elimu wakati mwingine ni sumu na jahiri. Ilifikia kutangaza eti inatibu ukimwi wakati mingi inajulikana kuueneza kwa kutembea na wagonjwa wapumbavu hasa akina mama walioshindwa kwenye ndoa zao au kukosa kizazi.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe kaguswa pabaya. Anaamua kutia buti kwa kasi. Anakwapua mic, “Kapende unaweza kutupa ushahidi wa unayosema au unaamua kutugeuza majuha? Unaweza kutwambia ni akina mama wangapi unawafahamu waliobakwa na waganga wa kienyeji kama unavyodai?”
            Kapende anajibu huku akicheka, “Mbona wengi tu. Hata nikutajia majina yao unadhani utawajua wakati ni watu wa mtaani kwangu? Isitoshe, kuna siri juu ya ushenzi huu? Hivi unategemea nini unapokuta tapeli limeandika eti lina dawa ya mapenzi au utajiri wakati jitu lenyewe halina mke au ni maskini na jingine kama lina mke ni matatizo matupu? Unataka kusema nisemayo ni uongo kuwa akina mama hawabakwi wakidanganywa eti ni namna ya tiba? Ama kweli ujinga na kukata tamaa ni ugonjwa mbaya kuliko ugonjwa wenyewe. Wengine unakuta wanajiita wasomi wakati ni wapumbavu wa kutupwa.”
            Kanji naye anaamua kula mic, “Hata mimi iko ona ganga njaa naita yeye ganga. Kama nataka jua ganga nabaka mama tazama teja nakwenda dukani yake. Kama yote iko vanavake jua hii nabaka yeye. Iko rahisi jua tapeli hii nabaka vanavake jinga jinga.”
            Baada ya kugundua kuwa maongezi yanaanza kuelekea kwenye uganga njaa tu, Msomi anaamua kuyarejesha kwenye mstari. Anakwapua mic toka kwa Kanji na kudema, “Nadhani tukubali kuwa kaya yetu ilikuwa imefikia pabaya sana. Kila tapeli kutoka kila mahali alikuwa akija na kujifanyia atakavyo. Mnaongelea wachunaji wanaojiita wachungaji au mashehena yanayojiita mashehe, mbona hamgusii matapeliwa wanaowatumia dada zetu kwa kisingizio cha kuoa na kuendelea kuishi kayani mwetu wakati ni wakimbizi wa kiuchumi? Mbona hamuongelei magabacholi wanaotorosha tanzanite yetu kila uchao? Kuna mengi ya kubadili kwenye kaya yetu. Hivyo badala ya kumuombea Dk Kanywaji tumwambie akaze buti kupambana na utapeli hata kwa wale wanaotumia neno la God.”
Naona shangingi la mama mchunaji Rwakatarehe linakuja.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 30, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

Mwalimu shukrani kwa kutujulisha kuwa hawa wadudu mafisa wanataka kuingia kwenye mlango ma-padlocks na kilaji kirahisi kwa unafiki waaambie hapa mageti yote yamefungwa kazi tuu sasa

Mafisadi wanapomwombea ili kujenga ukaribu na tabia zao kifasadi kwa kivuli cha Imani....waambie hao wanakweenda waeenda kwa mwenzao kule kule kijijini kwake maana hawa ndiyo ilikuwa tabia yao wakatengenezewa ulaji kutoka kwa awafikiria kutoka tumboni angalia hii link http://www.tanzaniatoday.co.tz/news/petition-ya-watanzania-uk-kupinga-vikali-utaratibu-mpya-wa-ukaguzi-magari

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon nashukuru kwa mchango wako. Utashangaa hawa wanaotaka kuombea nchi na rais hata marehemu wazazi wao hawawaombei. Ni mbwa mwitu wanaojivika ngozi ya kondoo ili kurarua kaya. Nadhani walipoona yule tapeli wa kinigeria TB Jushua amekaribishwa kwenye sherehe za kuapa makufuli wakajua udhaifu wake hivyo nao wakataka wawe karibu nao ili kuendeleza ushirikina na ujambazi wao. Walaaaniwe weanaotaka kutuombea wakati hawafanyi kazi zaidi ya kuibia waumini wao maskini na wajinga.