The Chant of Savant

Tuesday 27 October 2015

Kijiwe chatabiri ushindi kwa wadanganyika wote


            Baada ya wadanganyika kutumbukiza kura zao za kula kwa walaji wao, Kijiwe leo kinakaa kutafakari na kutathmini mambo yatakavyokuwa huku kikija na utabiri wa aina yake ambao utawashangaza wengi.
            Kapende ndiye anafungua dimba kwa kusema, “Wazee kwanza nawapongezeni wote kwa kufanya uchakachuaji wenye amani na utulivu.”
            Mipawa anamchomekea, “Mbona kuna sehemu hiyo amani hawakuiona achilia mbali kuiona? Mara hii umesahau kuwa poti kule Mwanza watu wametembezewa mikong’oto na kulipuliwa mibomu ya michozi?”
            “Hayo huwa hayakosekani kwenye kaya za kipuuzi. Mara hii umesahau kuwa ndata huwa wanawashwawashwa kuwamwagia watu maji ya washawasha na mibomu ya michozi ili kuonyesha kuwa nao wamo?” anajibu Mchunguliaji huku akiendelea kubukua gazeti la Danganyika Daima.
            Mpemba anakula mic, “Yakhe hata mie hiyo amani mnosifia sijaiona hasa ikizingatiwa kuwa kule Pemba watu walipigwa kwa kutaka kulinda kura zao.”
Mgosi Machungi anakula mic, “Taifa niizopata ni kwamba kue Ushoto mambo yaikwenda shwai sana na hakuna aiyepigwa waa kumwagiwa mimaji ya kuwasha waa mibomu ya michozi. Ndata wanaijua Ushoto. Wamwage upupu wapigwe zongo.”
            Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Kwa ujumla zoezi limekwenda vizuri sana. Sema  hatujatoka nyikani. Ngoja tungoje matokeo ingawa yanaonyesha kuwa wote watashinda kwa kishindo kuanzia wapiga kura hata wagombea wote.”
            “Una maanisha nini Msomi mbona umeniacha kizani? Watashindaje wote wakati lazima wawepo wa kushinda na kushindwa? Itakuwaje wakati wengine wameishaanza kukiri kudondoshwa kwa kusema kuwa watakwenda kuchunga ng’ombe kule kwa aina Laibon?” Mzee Maneno anauliza huku akibwia kahawa yake.
            “Umeuliza  swali zuri sana mzee wangu. Nitatoa ufafanuzi ili kila mtu anielewe wakiwamo wahusika wakuu. Kwanza, nianze na Eddie Luwasha. Huyu bwana alishinda hata kabla ya kuanza kampeni. Unadhani ni ushindi kidogo kukimbia chata lake na kupewa kijiti aviue vyama vinne vilivyokuwa tishio kwa nambari wahedi? Kwangu, huu ni ushindi wa kwanza. Pili, ushindi wa pili ni ile hali ya Eddie kuwalazimisha mahasidi wake waliomwita fisadi kwenda kumsafisha kaya nzima huku wakijivua nguo na kujidhalilisha ingawa si wote.”
            Mbwamwitu anachomekea, “Una maanisha nini kuwa si wote wakati wote waliandamana naye kumsafafisha ingawa kwa wapiga kura kama sisi hakusafishika?
            “Swali zuri hili. Namaanisha akina Dk Silaha na Profwesa Pumba ambao walikataa kuramba matapishi yao.”
“Hapo nimekupata vizuri sana,” anajibu Mbwamwitu huku akitabasamu.
            “Msomi naye anajibu. Nami nimekupata ten asana. Tuendelee,” anakohoa kidogo na kuendelea, “Mshindi wa pili na Dk Kanywaji Makufuli ambaye –kwa taarifa nilizo nazo –ni kwamba anaongoza kwa mbali sana. Hivyo, tegemea lisirikali la Makufuli. Je atawafunga mafwisadi kama alivyoahadi? Je ataanza na akina Escrow, EPA au Richmond?”
            Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Kwa njia moja au nyingine nakubaliana na uchambuzi wako wa kisomi hasa kuhusiana na Eddie ambaye kwa sasa yuko anachekelea akingoja kwenda kuchunga ng’ombe baada ya kuwazika wapingaji. Mie nadhani alitumwa na Nambari wahedi kwenda kuwarahisishia kazi ya ushindi.”
            Msomi anarejea, “Washindi wa mwisho hapa ni wapiga kura ambao walifanya kweli kukwepa kuingiza kaya kwenye matatizo zaidi ingawa hawajaleta ukombozi kwa kuondoa balaa lenyewe. Kimsingi, naweza kusema hapa waliopoteza ni UKAUA ambao –baada ya matokeo kutoka na kugundua changa la macho walilopigwa na Nambari wahedi watajilaumu maisha yao yote. Wengine waliopoteza ni akina Sumuye, Kimdunge Ngumbaru Mwehu na wale viranja wa nambari wani waliomfuata Eddie kula njuluku zake.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kukamua mic, “Yako wapi na kiko wapi? Wengi hapa niliwaambia kuwa wapingaji hawakuwa na sera mkaniona hamnazo. Wengine mlinishutumu kuwa na mapenzi ya kibubusa msijue nayamanya haya mambo. Sasa kiko wapi? Uko wapi ukombozi mliokuwa mkihanikizia na kushangililia msijue tutachukua ngoma?”
            Kanji naye hataki kuachwa nyuma, “Mimi ikosangaa sana vatu ya kaya hii. Iko nazugwa na Eddie kuwa iko pinzani na pinzani kwa jinga na pofu yao naingia kenge. Sasa tajua kama suka au nyoa iko rahisi dugu zangu.”
            Mijjinga aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kutia timu, “Kanji nakubaliana nawe. Siasa za kaya hii ni miradi ya wajanja wachache waliogeuza vyama kuwa kama NGO zao. Mimi ni mwanachama hai wa CHAKUDAME. Nilipinga sana movie hii lakini hawakunielewa. Sasa ngoja matokeo yatoke uone watakavyotoka nduki kuelekea kusikojulikana. Inasikitisha kuwa vyama vilikuwa vimejijengea umaarufu mkubwa na imani kubwa kwa wachovu lakini wakaharibu mwishoni kwa tamaa na ubinafsi na upogo wao. Lazima hapa watazomewa sana.”
            Kapende anarejea, “Mie wazomewe wasizomewe au kupigwa wasipigwe hanisikitishi. Kinachonisikitisha ni ile hali ya kuwa kila baada ya miaka mitano, tumaini linafutika kutokana na kutokuwa na vyama huru na vyenye lengo la kukomboa kaya. Hawa, kimsingi wameonyesha walivyoweka mbele maslahi binafsi wakatutelekeza. Sijui watatwambia nini baada ya Nambari wani kuchukua na kuweke waa ikachukua tena?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si ukaja msafara wa wakota wa Nambari wani wakishangilia ushindi hata kabla ya matokeo rasmi kutoka! Kwa hasira kila mmoja alijikata kivyake kupinga kushuhudia shamra shamra hizi ambazo ni maudhi kwa Kijiwe.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 28, 2015.

No comments: