The Chant of Savant

Sunday 6 September 2015

Magufuli anapoanza kutetea uoza kabla ya kuingia ikulu







     

       Kusema ule ukweli, miaka kama mitatu kabla ya uchaguzi nilimwambia mwanafunzi wangu aishie Toronto kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kilikuwa na mgombea mmoja wa maana na anayeuzika, Dk John Pombe Magufuli. Tarehe 26 Agosti 2015 majira ya saa kumi hivi za huku alinipigia simu akitaka nimwambie nilijuaje siri hii. Sitaki kujifanya mtabiri au waganga njaa wanosema walioteshwa. Sikuoteshwa zaidi ya kusoma uoza wa CCM. Hivyo, nilimjibu mwanafunzi wangu kuwa kama ningekuwa mbunge au waziri, basi ingekuwa mimi au Magufuli. Mwanafunzi wangu wa zamani alicheka sana na tukaachia hapo.
            Japo sishabikii siasa za Tanzania kutokana kuwa mbali, hakuna mtu niliykuwa namwanimi kama Magufuli. Hata siku chache kabla ya CCM kuteua na kupitisha mgombea wake, niliandika makala kwenye gazeti la Dira yenye kichwa cha “Wapinzani wamuangalie sana Magufuli” Nakumbuka nilituma makala hiyo Julai 11. Nataka kuonyesha ni jinsi gani Magufuli alikuwa amejijengea umaarufu kutokana na uchapakazi wake na kutokwa na makundi wala kutumia fedha kutafuta madaraka. Kwangu huu ulikuwa ni ushahidi kuwa Magufuli si mwenye tamaa ya madaraka na anaweza kuwafaa wananchi.
Pamoja na kusema yote hapo juu, matamshi ya Magufuli –kama alivyokaririwa na vyombo vya habari siku moja baada ya kuongea na mwanafunzi wangu –yameanza kufanya nibadili mwelekeo. Je baada ya kuaminiwa na CCM Magufuli ameanza kubadilishwa na mfumo hata kabla ya kuingia madarakani ambapo tulitegemea angeubadili huu mfumo? Sitaki niulize maswali mengi. Ninachotaka kusema hapa ni kumshauri Magufuli aangalie aendako na kufahamu kuwa safari ya kisiasa inaweza kuwa ndefu hata kama inagharimu masaa kama ilivyotokea kwa mpinzani wake mkuu Edward Lowassa ambaye aliingia kwenye ukumbi wa kuteua na kupitisha mgombea wa CCM akiamini kuwa hakuwapo mwingi isipokuwa yeye akaishia kutimkia upinzani.
             Nitatoa nukuu mbili za Magufuli ambazo zinaweza kumuonyesha kama rais asiyefaa hivyo kuwashawishi wananchi wasimchague. Akiwa mkoani Katavi alikaririwa mara mbili akisema, “Naowaombeni jamani, hatuchagui malaika, kila mtu ana Tatizo Lake. Inawezekana wengine tumechoka hata kumwangalia, lakini mkitaka nifanye kazi vizuri nileteeni bwana huyu,”
            Magufuli alikuwa akimtetea Joseph Kandege aliyeonekana kuchokwa na kuchukiwa na wananchi wa jimbo la Kalambo mkoani Katavi. Je hapa tunajifunza nini? Je inakuwaje Magufuli akatetea watu wabovu kama kweli naye si mbovu?
            Hebu angalia nukuu nyingine, “Wewe nenda hata kama humpendi fumba macho lakini umpigie nani?” Wananchi walijibu, “Malochaa.” Magufuli aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Laela. Magufuli alikaririwa akimtetea Ignas Malocha, mbunge mwingine aliyeonekana wazi kuchukiwa na wale waliomchagua akaishia kuwasaliti na kuwaangusha. Kwanini Magufuli anawashauri wapiga kura vitu visivyoingia akilini? Akiwa Mkoani Sumbawanga alimtetea mbunge mwingine ambaye amebanwa Hilary Aeshi.
             Kwanini anawashauri watu wawachague watu wanaowachukia kutokana na uoza wao kama siyo kuwahujumu? Cha msingi hapa ni wahusika kujua kuwa huo mzigo na gamba anavyotetea Magufuli vitakapoanza kuwaumiza, watakaoumia ni wao na si Magufuli. Kimsingi anachobainisha Magufuli ni kwamba hata hiyo mizigo itakapoanza kuvuruga na kuvurunda atailinda kwa kutumia rungu lake la urais. Je wananchi wapewe ishara gani kuwa wanahujumiwa na wale waliowategemea; hivyo wachukue hatua? Anachobainisha Magufuli ni kufuata nyayo za Jakaya Kikwete ambaye aliwakingia kifua watu kama Benjamin Mkapa, familia yake na marafiki zake hata walipobainika kujitwalia na kuiba mali za umma kama vile Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira na wale wote walioghushi. Mtu wa namna hii ni kwa kuogopwa kama ukimwi kama siyo ukoma.
            Tunapenda kuhitimisha makala hii tukimshauri Magufuli asichafue rekodi yake kwenye majukwaa. Oktoba siyo mbali na wananchi watakuwa bado wanakumbuka maneno yake. Hata hivyo, ashukuru Mungu kuwa wapinzani hawachambui vilivyo kauli zake na za wana CCM wenzake kama upupu wa juzi aliomwanga rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alijivua nguo hadharani huku akitoa matusi yanayoweza kumharibia Magufuli. Kweli binadamu si malaika. Makosa aliyotenda Katavi asiyarudie vinginevyo ataanza kujionyesha tofauti na tulivyomdhania. Mchapakazi wa kweli anapaswa awatake wananchi wampe wachapakazi hata kama wanatoka kwenye upinzani. Hii itamuonyesha kama mtu anayetaka maendeleo na si siasa za kipuuzi za kulindana kama tulivyozishuhudia.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 6, 2015.

2 comments:

Mbele said...

Taarifa nyingine niliyosoma jana inasema kuwa Magufuli katika kuhutubia "mafuriko" mahali fulani amesema kuwa akishika nchi, atakuwa mwenye bahati kwa sababu atakuwa na wazee wa kuwafuata ili kupata ushauri. Kwa mujibu wa taarifa niliyosoma, wazee hao ni marais wastaafu.

Sasa hapo nilipata mshangao. Magufuli huyu huyu amekuwa akilalamikia na kuyashangaa mapungufu mbali mbali yaliyomo nchini, huku akisema atayarekebisha. Papo hapo anasema kuwa akishika nchi, atatafuta ushauri kutoka kwa hao hao waliosababisha haya mapungufu anayoyalalamikia.

Kwa mtazamo wangu, hata kama Magufuli ataacha kujikanyaga, ukweli ni kuwa hataweza kwenda kinyume na matakwa ya kamati kuu ya CCM. Atakuwa anatii maelekezo ya kamati, ambayo ina nguvu isiyo kifani. Ona jinsi kamati ilivyowafungia vigogo mbali mbali wa CCM kwa kile kilichosemwa kuanza kampeni kabla ya wakati, nao wakatii amri kwa unyenyekevu.

Magufuli akichaguliwa, ni ushindi kwa kamati kuu ya CCM. Tutabaki na mfumo ule ule ambao umetufikisha hapa tulipo. Siwalaumu wa-Tanzania wanaopigania kuing'oa CCM huku wakisema wazi kuwa mengine yatashughulikiwa baadaye.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele usemayo ni ya kweli. Hata ukisikiliza baadhi ya madai yake unapata shaka hata na huo udaktari wake. Juzi alikaririwa akiwa Songea akisema kuwa wampe kura. Kwa sababu akiwa waziri wa ujenzi hakuwasahau. Aliwajengea barabara. Cha kushangaza ni kwanini Magufuli anashindwa kuelewa kuwa hakujenga hizo barabara kwa fedha yake au kwa utashi wake bali kutekeleza wajibu wake kama mtumishi wa umma.
Kimsingi kinachoendelea ni siasa zile zile sa kisanii na kibabaishaji. Hawa wastaafu watatu wana nini zaidi ya kuwa mafisadi? Nadhani Magufuli amejibainisha kuwa ni kibaraka cha hawa wastaafu wenye madhambi yao. Hatakuwa na tofauti na Mkapa aliyelinda uoza wa Mwinyi na Kikwete akalinda wake sawa na ambavyo Magufuli atalinda uoza wa Kikwete. Ndiyo maana imani yangu ni kwamba hakuna anayefaa kati ya hawa wawili. Je umeisoma ya Lowassa kwenda kuhutubia akifungua na CCM OYEEE au Msindai kusema kura zote za urais, ubunge, udiwani wapewe CCM wakati akiwa kwenye jukwaa la UKAWA?