The Chant of Savant

Saturday 19 September 2015

Gwajumaa: Si uunde chama cha kisiasa?

Baada ya mchunaji, sorry, mchungaji mwenye cheo cha kujipa cha askofu Jose Gwajumaa kutawala majukwaa ya siasa, Mlevi ameamua kumtolea uvivu.
          Kila mchovu, mdanganyika na mbongolalalander ana haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa ingawa si wote. Ndata, wasoja na viongozi wa kiroho wasio na uroho wanaweza kuwa na vyama wanavyopenda japo hawapaswi kuonyesha hadharani. Hii ni kutokana na kuepusha kuwagawa na kuwakwaza waumini. Hata hivyo, siku hizi mambo yamebadilika. Wapo viongozi wa kiroho wanaotia shaka wanaounga mkono vyama fulani tena hadhani. Wengine wamegeuka wasemaji wasio rasmi wa vyama husika. Waambiwe wachague moja joho au gwanda.
          Pamoja na bangi na ulevi wangu, huwa nashangaa mantiki ya ngurumbili hawa kufanya wanayofanya wasijue ni kinyume cha sheria na maadili. Inakuwa noma pale anayejiita kiongozi wa kiroho kujiingiza kwenye siasa za majitaka kama vile kuwa “mshenga” wa mgombea fulani kiasi kujiingiza kwenye vita vya kisiasa. Je huyu tumueleweje usawa huu?
          Hivi karibuni, Gwajumaa alisikika “akimvua nguo” Dk Willy Silaha, katibu wa zamani wa Chakudema aliyeachia ngazi baada ya kutokubaliana na chata lake kuweka mfukoni na wale anaowaita mafisadi mapapa tena wa kunuka. Alisikika akitoboa siri za ndani za Dk Silaha kinyume cha sheria na maadili. Je huyu ana mke; na kama anaye atafurahi kusikia mambo ya chumbani kwake kwenye mikutano ya waandishi wa umbea? Ama kweli mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu!
          Gwajumaa aliyetajwa na Dk Silaha kuwa mshenga wa Eddy Luwasa, alipagawa pale Dk Silaha alipoanika siri zake na undumilakuwili wake.   Kujibu mapigo, alinyofoa tuhuma kiduchu kwenye nyingi alizofyatua Dk Silaha. Gwajumaa alidandia lile dai kuwa alimwambia Dk Silaha kuwa Luwasa angechomoka toka Nambari Wani akiwa na waishiwa kibao huku akiungwa nkono na mabishop kama 30 waliokatiwa uchache. Gwajumaa anasema kitendo cha Dk Silaha kuwatuhumu watu wa God ni chakulaaniwa. Tumuulize swali dogo. Je watu wa God hawahongwi? Mbona Yuda Iskarioti alihongwa vipande 30 akamsaliti mwana wa Adamu sawa na viongozi wa kiroho wanavyomsaliti kwa kujiingiza kwenye mambo ya madili na kiuroho badala ya maadili na ya kiroho?
          Swali la nyongeza: Mbona hivi karibuni askofu mmoja wa kweli alikiri kuwekewa njuluku zipatazo milioni 40 kwenye akaunti yake na fisadi wa Escrow Jimmy Rugemalayer?  Je Gwajumaa anawaongelea maaskofu wapi wakati siku hizi wapo wengi wa kweli na wa kujipachika? Anayejipachika cheo kikubwa kama hiki atashindwa nini kuhongwa ukiachia mbali kuwa na maaskofu ni binadamu? Nani angeamini kuwa watu wa God wangewatafuna kondoo wao kama ilivyotokea kwa kanisa moja kubwa ulimwenguni ambapo makasisi wake walipatikana na hatia za kulawiti na kunajisi watoto na waumini wao tena kwa miongo kibao?
          Pamoja na bangi zangu, nakumbuka kuwa Yesu alisema kuwa mbinguni ni kwa maskini na si kwa matajiri. Rejea mfano wa Zakayo. Leo hii kuna wachunaji sorry, wachungaji ni matajiri wa kutisha hadi kununua vyopa au helkopta kwa kimakonde. Namshauri Dk Kanywaji Makomeo awashughulikie wakwasi hawa waeleze walivyoupata.  Pia nawashauri wakwasi hawa wanaowaibia waumini wajinga na wenye matatizo lukuki wasome Matayo 19:24 isemayo, “Heri ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko wakwasi kuingia kwenye ufalme wa Mungu.”
          Kama Gwajumaa na wengine kama yeye wanapenda siasa si wa waunde vyama badala ya kuwa mguu mmoja kwenye dini na mwingine kwenye siasa? Hata hivyo, hawatafanikiwa. Maana ukiwa kiongozi wa kiroho mwenye uroho ukataka kufanya siasa nje ya chama twawala hufiki popote.
Zumbe atogolwe sana na mbarikiweni sana wasomaji wa pumba hizi za mlevi bingwa wa bangi na ulabu. Wachanganya siasa na dini walaaniwe kama wale wachuuzi waliokuwa wamegeuza sinagogi kuwa genge la biashara.
Chanzo: Nipashe Sept., 19, 2015.

No comments: