The Chant of Savant

Monday 6 July 2015

Tuhuma za ufisadi: Mchawi wa Lowassa ni Lowassa


Ingawa mtia nia waziri mkuu wa zamani aliyeondoka madarakani kwa kashfa ya Richmond Edward Lowassa mbunge wa Monduli analaumu wanaomtuhumu ufisadi, anapaswa kujilaumu mwenyewe. Ndiyo maana tunasema kuwa mchawi wa Lowassa ni Lowassa mwenyewe na uchawi utakaommaliza si mwingine bali ukimya na kujipa matumaini hata pasipohitajika kufanya hivyo.
“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo.” Utetezi wa namna hii licha ya kuwa mwepesi unaonyesha mwoga wa mhusika. Kwa wepesi na ukosefu wa mashiko wa utetezi wake, Lowassa licha ya kuwachochea waseme sana, amejionyesha kama mtu mwoga ambaye hana ubavu wa kuwashughulikia wahusika. Wengi walitegemea wasikie akisema kwenda mahakama kuwashitaki wahusika. Kusema kuwa waache tu hakuna uzito wowote hasa ikizingatiwa kuwa yumo kwenye mbio za kisiasa.
 Kama wanaomtuhumu wanasema uongo basi yeye angekuja na ukweli badala ya jibu la mkato kuwa hakuna ukweli bila kuonyesha uongo wa wanaomtuhumu. Lowassa alisema kuwa amechoshwa na majungu asijue majungu haya anayosema anayasababisha yeye kwa kukalia kimya shutuma zinazomkabili.
“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?” Anachopaswa kufundishwa Lowassa ni ukweli kuwa mahakama ya kisiasa si sawa na ya kisheria. Na isitoshe, watu wanaweza wasiwe na ushahidi kama anavyoutaka lakini mazingira yakawa ushahidi wa kutosha. Kwanza, kwanini azushiwe yeye? Jibu ni jepesi kuwa lisemwalo lipo kama halipo laja. Ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa –kama anavyokiri Lowassa mwenyewe–alianza kutuhumiwa zamani. Hivyo, madai ya ufisadi wa Lowassa si suala la siasa za kuchafuana au mbinu ya wapinzani wake kummaliza kisiasa. Kama anakiri kuwa ametuhumiwa kwa miaka mingi hata kabla hajaingia kwenye kinyang’anyiro anategemea nini sasa? Mbona hili jambo ni jepesi kuelewa?
Pili, Lowassa ni mtu mwenye bahati ingawa bahati haiji mara nyingi. Kama ametuhumiwa miaka mingi iliyopita, hata kupewa uwaziri mkuu ilikuwa ni bahati. Wengi wanajua jinsi marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alivyokatiza mbio za Lowassa na Jakaya Kikwete mwaka 1995 baada ya kudai walikuwa wamepata wapi pesa ya kukodisha ndege kwenda na kurudi Dodoma kuchukua fomu. Nyerere wala hakuzungusha. Alikaririwa akisema kuwa wengine wamejilimbikizia utajiri ambao wasingeweza kuutolea maelezo. Tangu Nyerere afyatue kimondo hiki kiligeuka kongwa kwenye shingo ya Lowassa. Anachopaswa kujiuliza Lowassa ni kwanini maneno ya Nyerere yalitafsiriwa kuwa yalimlenga yeye wakati walikuwa wawili kama hakuna namna? Jibu ni simpo kuwa Nyerere aliwalea akina Kikwete na Lowassa. Hivyo, alikuwa anawafahamu vizuri sawa na wanachama wenzake Lowassa wanaosema wazi wazi kuwa hana udhu.
Hivyo, lazima tusema kuwa utetezi wa Lowassa ni dhaifu na unaonyesha kama kuna kitu anaogopa kukigusia kwa sababu ajuazo mwenyewe. Kimsingi, asipofanya maamuzi magumu atazidi kuandamwa.  Aige mfano wa Barack Obama. Alipotuhumiwa kuwa aliwahi kuvuta bangi alikiri na kuomba msamaha na mambo yakaisha akaendelea kuwa rais.
Japo hakuwataja wanaomsema, wapo wanajulikana kuwa wengine ni wanachama wenzake na watia nia wenzake wanaomfahamu fika. Sikumbuki kama ameishakwenda Butiama kutafuta kuungwa mkono na familia ya Nyerere kama wenzake walivyofanya. Nadhani wengi wanajua sababu ya Lowassa kutofanya hivyo.
Lowassa ameshindwa kujitofautisha na watu kama Nazir Karamagi, Andrew Chenge na Ramadhani Madabida ambao mazabe yao yanajulikana kwa watanzania walio wengi! Je anajenga picha gani? Je kwanin Lowassa hataki kuongelea kashfa iliyomtoa madarakani tena kwa hiari yake baada ya kupewa kitanzi ajimalize naye akachagua kujitundika kuliko kutundikwa? Je anadhani kuwa doa la Richmond anaweza kulifuta? Sidhani kama waathirika wa ujambazi wa Richmond walishasahau migao na kulanguliwa umeme. Je Lowassa anashindwa kuelewa kuwa kujitokeza kwa watia nia wengi chamani mwake tena wasio na doa ni ushahidi kuwa CCM ina wigo mpana wa kuchagua mbeba bendera yake? Sijui wanaomshauri Lowassa ni akina nani wasiomuonea huruma. Maana, kwa wataalamu wa mikakati, anachofanya Lowassa ni kuzidi kutumia fedha zake kwenye mradi ambao matokeo yake yanajulikana kuwa hauna faida.
Lowassa anahangaika na wanaomtuhumu ufisadi chamani mwake wakati wapinzani wanaojua kila kitu hawajafungua midomo. Sijui hata kama anaweza kuwazidi kete CCM akapita kwenye chujio, atafanya nini atakapokutana uso kwa uso na wapinzani ambao kimsingi ndiyo walioibua kashfa nzima ya Richmond na wakaisimamia pamoja na vitisho vyote walivyowekewa? Nadhani hata CCM nao hawawezi kuwa wazembe kiasi hiki wakaja na mtu ambaye atakuwa soft target ya wapinzani kutokana na kujua madudu yake. Hapa ndipo mchawi wa Lowassa anapozidi kuwa Lowassa.
Tumalizie kwa kumpa ushauri wa bure Lowassa kuwa kama anataka wanaomwandama kwa uongo wakome basi aanike ukweli ili wananchi waamue wenyewe badala ya yeye kukaa kimya akisema wasemayo si ukweli wakati ukweli wenyewe hauweki wazi. Kama hatafanya hivyo, basi Lowassa afahamu kuwa mchawi wa Lowassa si mwingine bali Lowassa mwenyewe.
Chanzo: Dira Julai 6, 2015.

4 comments:

Anonymous said...

LOWASSA KASEMA KWELI "kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo."KAMA KUNA USHAHIDI UTOLEWE SIO KUROPOKWA TUU FULANI HIVI NA VILE
MNA USHAHIDI JAJI ANASEMA TOA USHAHIDI LAKINI NYIE HAMNA USHAHIDI NI CHUKI ZENU BINAFSI
HUYO NDIE LAIS WA WATANZANIA MKITAKA NDIE HUYO NA IKIWA HAMUTAKI NDIE HUYO

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umesikika japo rais wa Tanzania hajajulikana. Kama Lowassa ni lais wa Tanzania hakuna anayepingana na hilo na aendelee na ulais wake japo urais hatapata kwa maneno makali ya vibaraka au wapenzi wake.

Anonymous said...

Kutokana na maoni ya anon...hapo juu. Sasa naamini na nimekubali kweli sisi wananchi ni majuha na tunasahili kupata malais majuha na siyo marais makini na wazalendo wasiohitajika kupakwa rangi ili kuondoa alama za makovu ya uhalifu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon 10:32 umenena vyema. Naamini wahusika wameipata na wamesikia. Shurani sana.