The Chant of Savant

Saturday 25 July 2015

Mlevi achonga na Joni Kanywaji Makufuli

Mpendwa Mheshimiwa Dk Joni Kanywaji Makufuli
Kwa mara ya kwanza anawasiliana naw kwa niaba ya walevi na wachovu wote kayani. Kwanza, nakupongeza kwa kutokatwa jina na kupitishwa kumrithi bwana mkubwa, rafiki yangu Njaa Kaya. Hongera sana mheshimiwa sana na aliyepakwa mafuta na wateule wakuu ili ufanye mambo makuu ila si makufuru.
Sitaki nizungushe japo nipeishaupiga mma na tubangi kidogo. Nachukua fursa hii–kama mzee na msomi mtukuka wa walevi–kukupa wosia kama utafanikiwa kuula.
Kitu ya kwanza nataka ushughulikie vibaka na majambazi ya EPA, Escrow na Richmonduli hata kabla hujakaa kwenye kiti. Maana kitu waliyotufanyia ni mbaya sana kustahiki nao kufanyiwa kitu mbaya zaidi. Walevi wanataka kuona mijambazi kama Jimmy Rugemalayer na Singasinga wakipigwa mawe hadi kufa au kuchomwa moto kama siyo kupelekwa kwa ISIS iwachinje kigaidi ili wanaodhani kaya yetu ni shamba la bibi wakome na kukomaa. Inapendeza? Au siyo?
Pili, walevi wamenituma wakikutaka –si kukuomba –usiteue vihiyo, mafisadi, vibaka na mipaka kwenye baraza lako la mawaziri. Vihiyo –hasa wale walioghushi, japo walikingiwa kifua–wanajulikana. Hata wale waliopewa ubalozi, ukuu wa wilaya na mkoa, ujaji na makandokando mengine watimliwe haraka ili kujenga heshima kwa lisirikali lako tukutu chini ya Chama cha Mizengwe (CcM).
Tatu, walevi wanakutaka ufumue mikataba yote ya uchukuaji unaoitwa uwekezaji. Waliokutangulia walituingiza mkenge na kutufanyia usanii. Si waliahidi wangefumua na kusuka upya mikataba hii wakaishia kuingia mingine ya kishenzi na kijambazi ikiwamo Richmonduli. Hatutaki urudie makosa haya ya kichovu na kipumbavu.
Nne, usiwasahau walevi. Maana bila kukupata wewe huwa hawalali. Sisi ni watu wako –yaani watu wa kanywaji kama jina lako. Hivyo, lazima tukukumbukane hasa ikizingitiwa kuwa kama utawaahidi kanywaji na bangi zaidi watakupa kura za kula kama hawana akili nzuri. Hivyo tukiwa na rahis kanywaji na kanywaji na tubangi kama kawaida nadhani furaha itarejea
Tano, ukiachia mbali kuwakumbuka walevi, hakikisha kwenye ulaji wako hakuna kujuana wala kufadhiliana. Ulipita bila mfadhili. Hivyo, uhitaji kulipa fadhili wala kupendelea.
Sita, tunataka kukuletea ufagio wa chelewa ili uifagie na kuisafisha kaya inayonuka vibaya sana. Tutataka uanzie ikulu ukiwatimua wale wote walioajiriwa kulipwa fadhila kama wale makanjanja wanaojifanya vipaza sauti vya ikulu waliowachafua wenzao kwenye mchakato wa 2005. Siku nyingine tutakupa majina yao. Hata hivyo, unawajua vizuri akina Rweyependekezamo. Hata wale waliopewa ukuu wa wilaya timua kama huna akili nzuri. Mchonga alionya kuwa ikulu hakuna biashara na ni patakatifu pa patakatifu. Kwa vile paligeuzwa patakakitu pa patakitu au pachafu pa pachafu, tunakutaka usafishe kila kitu pale.
Saba, epuka uzururaji wa kupenda kwenda kutanua Ulaya na Amerika. Walevi wanasema kuwa wanachukia jina la Vasco da Gama sana. Hivyo, wanategemea utakaa ofisini na kutatua matatizo yao badala ya kuzurura kwa kisingizo cha kuombaomba. Usikubali kuwa Vasco da Gama Matonya.
Nane, walevi wamenituma nikupe laivu kuwa usimruhusu Bi mkubwa wako aanzishe kampuni almaaruf NGO. Kwa walevi hizi NGO ni vichaka vya wizi wa fedha za umma na matumizi mabaya ya ikulu. Hivyo, ogopa NGO kama ukoma au ukimwi. Kwani mwisho wa siku hukuacha mchafu, asiyeheshimika wala kuaminika. Guess what. Mzee Mchonga wa Musa hakumruhusu Maria wake kuwa na kampuni hii aina ya NGO na bado bi mkubwa huyu anaheshimika kuliko wote waliomfuatia.  Walevi wanataka bi mkubwa wake awe wa pili baada ya Maria Mchonga. Nadhani unajua ninachomaanisha. Pia usiruhusu mashoga zake wapewe vyeo tena wasivyoweza.
Tisa, usiruhusu kitegemezi chako au ndugu yako kuchukua nafasi yako Chato. Cheo si urithi binafsi. Maana, tulizoea kuona uongozi ukigeuzwa private estate. Hii–kwa mtu aliyepiga shule kama wewe –inaweza kukuonyesha ima kama mtu aliyeghushi au ambaye alisoma lakini hakuelimika.  Nakuaminia bro. tunataka ujenga kaya kama barabara.
Sipigi chuku wala kujigonga ili unikumbuke japo si vibaya ukinikumbuka. Kuna mlevi mmoja aliyekuzimia hadi akasema sasa anaona Mchonga na Muringe wakifufuka kupitia kwao kama hutatupiga chini au kutuangusha.
Kumi, walevi wanasema usianze kupiga kampeni kabla ya kipenga kupulizwa. Hata huu upuuzi wa kujitambulisha achana nao. Nani asiyekujua hapa kayani bro? Hivyo, epuka njama za wabaya wako kukuchafua kwa kukushauri upuuzi. Pia usikubali kutumia raslimali za umma kufanyia kampeni. Walevi wanasema kuwa kama hutakuwa na means ongea nao wakupe tafu kuliko kuaibishwa na matumizi mabaya ya raslimali za umma. Pia wanakuonya kuwachunga sana magabacholi wanaopenda kujifanya wanakupenda ili wakutumie na kukuchafulia sifa yako nzuri. Si wema hao. Sana sana uwabane walipe kodi na kuzuia kuchukua nafasi za wamachinga wetu.
Kumi na moja, walevi wanasema wazi kuwa lazima uanzishe upya mchakato wa katiba ili wapate katiba isiyo ya kifisadi na kijambazi. Wanaamini kuwa nawe hukupendezwa na uhuni uliofanywa hadi katiba ya walevi ikauawa huku njuluku zao zikiliwa na muda wao kupotezwa. Tena kabla sijasahau, wale wahuni waliopewa ukuu wa wilaya kwa kumnyanyasa mzee Sinde ambaye ameonyesha kukubali sana lazima uwapige chini. Lazima ofisi zetu za wilaya na mikoa ziheshimike badala ya kuwa chaka la kujaza wahuni na wababaishaji kwa vile wanajuana au kula na wakubwa. Najua sasa wengine matumbo joto kweli kweli hasa wakijua kuwa wewe si mhuni wala mbabaishaji.
Mwisho, soma sana sera za mzee Mchonga unaweza kumaliza muda wako ukiwa baba wa pili wa kaya baada ya wenzio watatu kutoka kapa tokana na upogo, tamaa na uvivu wa kufikiri.
Kwa vile nasikia kanywaji na tubangi vinazidi kupanda upstairs, acha niachie hapa nikingoja kupokea email yako ya majibu ili niwarejeshee walevi waheshimiwa walionituma kwako.
Ubarikiwe sana bro.
Kanywaji hoyeee! Makufuli hoyeee!
Nahene ngosha.
Chanzo: Nipashe Julai 25, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

Tukuwaga hutujui asanteni
Kura zetu oacober hawapati ngo
Pamoja na kuharibu mitambo ya bhv