The Chant of Savant

Sunday 31 May 2015

Lowassa anamtishia nani na kwanini?

  • LOWASSA CAN YET STEP TO CANAAN: BY NOVA KAMBOTA.
          Hivi karibuni mmojawapo wa wanaotaka kuwania urais kwa tiketi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, waziri mkuu wa zamani aliyeondolewa na kashfa ya Richmond Edward Lowassa alitoa la moyoni ingawa hakujibu tuhuma za ufisadi dhidi yake. Alikaririwa akisema kuwa mambo mengi wanayomtuhumu kwayo ni uzushi hata yanayoonekana au kujulikana kuwa ya kweli. Wengi wanahoji ni kwanini Lowassa amechukua miaka mingi kujibu au kuongelea tuhuma dhidi yake.
Moja ya kauli iliyofanya wengi wakune vichwa na kuanza kumuogopa Lowassa ni pale aliposema, “Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.” Je Lowassa anamaanisha kuwa hata kama atanyimwa fursa –kama maneno ya rafiki yake yanavyoonyesha –atanywea na kuendelea kuuguza maumivu akiwa ndani ya CCM? Je CCM ni mali yake binafsi au yametimia yale aliyosema Nyerere kuwa CCM imo mifukoni mwa mafisadi? Je atafanya nini iwapo watanzania au wanaCCM wengi wakimkataa?  Mara hii amesahau alivyotishia kutojiuzulu wakati wa kashfa iliyomng’oa madarakani ya Richmond punde tu akajipiga mtama na kuufyata akatimka? Je Lowassa anampiga nani mkwara zaidi ya rafiki yake rais Jakaya Kikwete aliyeanzisha mjadala wa nani anafaa kuwa rais huku akionyesha wazi kuwa hana nafasi ya urafiki kwenye kumsaka mrithi wake? Je ubavu anao? Na hii jeuri anaipata wapi?
Nyerere pamoja na kuanzisha CCM hakuthubutu kukufuru na kutishia kama anavyofanya Lowassa. Nyerere alisema CCM si baba wala mama yake akimaanisha kama ingeendelea kutomridhisha, angejiondoa. Je Lowassa –kwa kuzingatia uzoefu wa mkwara wake wakati wa Richmond –ana mpango wa kukihama CCM hasa ikizingatiwa kuwa husema hili na kutenda lile?
Kuhusiana na tetesi kuwa afya yake imedhoofu, Lowassa alikuwa na haya ya kusema,“Twendeni tukapime tuone nani mgonjwa. Tuonane kwenye uwanja wa mapambano katika mchakamchaka wa maendeleo, ninajua nitawashinda kwa mbali.” Japo napping vitisho vyake, kwa hili la kupima afya naungana na Lowassa kuwa wagombea urais wapime afya zao ili kuepuka kupoteza fedha nyingi kuuguza rais hata kumpoteza rais kama ilivyotokea nchi ya jirani ya Zambia ambapo walimchagua mtu mgonjwa akafa miaka mitatu baada ya kuwa madarakani. Na wafanye hivyo si kwa kukomoana bali mujibu wa sheria ambapo vipimo husika vitafanyika kwa njia halali na si kughushi na kificho.
Akiongelea kashfa iliyomg’oa madaakani kwanza alisema kuwa serikali haikupoteza hata senti moja kabla ya kujipinga na kusema,“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni kutaka kuvunja mkataba wa Richmond nikaita wataalamu…..nao wakakutana chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa uamuzi ambao sina haja ya kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola 120 milioni.” Kama anayosema ni kweli kuwa hakuhusika na kashfa ya Richmond, kwanini haya anayosema sasa hakuyasema alipoitwa kujitetea mbele ya Tume Teule ya Bunge almaarufu kama Tume ya Dk Harrison Mwakyembe hadi akapewa kitanzi apime na kuamua na akaamua kuachia ngazi kwa vile alijiona mkosefu? Kama hakuwa na kosa kweli, kwanini aliamua kujiuzulu badala ya kutaka ukweli ujulikane ili umma ujue nani alileta Richmond na kwanini sheria zilipindwa? Na kwanini sasa si wakati ule?
Hakuna sehemu alipowaacha wengi hoi Lowassa kama kutolea mifano ya watu matajiri huku akimtaja mmoja wapo aliyepata utajiri wake kwa njia ya ufisadi hadi akafukuzwa uwaziri. Alisema, “Nataka watu wawe matajiri, tuache kuwabeza matajiri, matajiri wawe ni mfano kwa wengine, watu kama (Reginald) Mengi, (Said) Bakhressa na (Nazir) Karamagi wanatakiwa kuwa mfano kwa wengine.” Je Lowassa akiwa rais atatengeneza matajiri wangapi wa namna ya huyu mmojawapo kwa kuruhusu waibie umma ili wawe matajiri?
Sehemu alipowaacha wengi hoi ni pale alipokanusha kuwa hajawahi kukataliwa na marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Alikaririwa akisema, “Jambo hili si la kweli, sijawahi kukataliwa.” Je Lowassa amesahau au anafanya makusudi au kudhani kuwa watanzania wote ni wasahaulifi kirahisi hasa kuhusiana na maneno na matendo ya kipenzi chao Mwl Nyerere ambaye hakumkataa yeye peke yake bali na rafiki na mshirika wake Kikwete baada ya kuuliza pesa ya kukodisha ndege kwenda na kurudi kuchukua fomu za kugombea urais waliipata wapi wasijibu? Tunajua, Lowassa anaweza kumwonyesha Nyerere kama muongo kwa vile hayupo tena ila wengi wanajua Nyerere alivyochefuliwa na kuchukizwa na utajiri wa Lowassa ambao hadi sasa hajawahi kuutolea maelezo.
Huyu kama amefikia kuwatishia wanachama wenzake wajiondoe kwenye chama asicho nacho mamlaka akipata urais si atawaamuru wale wasiompenda kuihama nchi? Je rais wa namna hii anafaa kweli?
Hata hivyo, kwa wanaoujua jinsi siasa za Tanzania zinavyoendeshwa ambapo ndoa mpya hufungwa na za zamani kuvunjwa, Lowassa ameishajua hatima yake kuwa tiketi ya CCM haipati. Kwa vile akipewa tiketi ile CCM itaangushwa kirahisi kutokana na historia ya mhusika na hasa ikizingatiwa legacy anayoacha rafiki na mshirika wake Kikwete.
Tumalizie kwa maneno ya Kikwete yanayomkaanga Lowassa, “Hivyo ni lazima tupate wagombea wanaochagulika na wananchi ambao niwengi kuliko wanaCCM. Hatuwezi kupeleka kwa wananchi watwasiokubalika, watu waliopungukiwa sifa, tukadhani Watanzania watamchagua tu kwa sababu ni mgombea wa CCM.”
Chanzo: Tanzania Daima Mei 31, 2015.

No comments: