The Chant of Savant

Tuesday 5 May 2015

Hongera Takukuru kuiumbua CCM


          Hivi karibuni Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iliamua kujivua gamba kwa kusema wazi nani ni gamba na mhimili wa rushwa na ufisadi nchini. Baada ya kushambuliwa kuwa haifanyi kazi vilivyo, Takukuru iliamua kuweka mambo hadharani. Vyombo vya habari hivi karibuni vilimkariri Daniel Mtuka, Kamanda wa Takukuru wa Dar es Salaam akisema, “Taasisi iko tayari hata kama viongozi au wanachama watatuletea malalamiko hayo leo (jana). Bila ushirikiano wa viongozi inakuwa vigumu kufuatilia.”  Kumbe kutofanya kazi vizuri kwa Takukuru siyo lengo lao bali wale wanaowaamuru? Je Takukuru inaweza kuwakamata wala rushwa na mafisadi ima waliomo madarakani au marafiki na wana familia zao wakati iko chini ya rais?
Tokana na madai kuwa Takukuru inanyimwa “ushirikiano” na mamlaka za juu, tunapata jibu ni kwanini ufisadi na rushwa vimetamalaki. Huu ni ushahidi kuwa wahusika wananufaika na jinai hii. Je hii ndiyo sababu ya kuiweka Takukuru chini ya ofisi ya rais ili kuifunga gavana isiwaguse wasioguswa kama Mtuka anavyoeleza hapa? Anasema, “Kwa kesi ya rushwa kwa wagombea hao, ni vigumu kwani tuliwahi kukutana na changamoto ya kushindwa kufanya kazi yetu miaka iliyopita tulipomnasa mgombea fulani wa ubunge CCM ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama. Sisi tulidhani ni tatizo, lakini hali hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo, akasema ni sahihi na ataingia kutekeleza ilani ya chama.” Huu ni ushahidi wa wazi kuwa CCM ndiyo mhimili mkuu wa rushwa kutokana na kunufaika nayo. Je ni wabunge wangapi wanaomaliza muda wao walioingia madarakani ima kwa kutoa rushwa, kutangazwa kwa mabavu tofauti na ukweli halisi wa matokeo? Ni wengi na wanafahamika. Je baada ya wananchi kupata ukweli huu, wataruhusu jinai hii iendelee hata kwenye uchaguzi ujao? Nadhani Mtuka amewarahisishia kazi wapiga kura. Kimsingi, amewaonya kuwa wasipojiandaa kulinda kura zao na kugomea washindi wa kimabavu mchezo utaendelea.
Mtuka wala hafichi. Anaonyesha wazi nani ni kikwazo na nini kifanyike. Aliongeza kusema, “(Iwapo watatoa ushirikiano) Itakuwa rahisi kuona tunaanzia wapi, pia (kwa kuangalia) mfumo wa chama, taratibu zake, katiba na ilani yake wanafanyaje kazi.” Kuthibitisha ukweli wa madai haya, wahusika wala hawakujihangaisha kujibu wala kukanusha. Je watu wa namna hii wanaotegemea rushwa na uchakachuaji kuwa madarakani wanaweza kuandaa uchaguzi wa maana ambao kwa kiingereza huitwa free and fair au huru na wa haki?
Nadhani kuna kitu Takukuru walichelea kukisemea ambacho ni ukweli kuwa hawa watoa rushwa wakubwa walioko madarakani, pia hupata fedha za kuhongea kupitia rushwa hiyo hiyo. Wanapewa rushwa ili wapate fedha ya kutoa rushwa kwa wapiga kura. Ni mchezo wa mduara ambaye mlaji naye huliwa. Ni kulana kwa kwenda mbele. Wazito wanahongwa na wawekezaji na matajiri wenye maslahi binafsi kama vile kupewa misamaha ya kodi, kuingiza bidhaa tata na mazabe mengine. Nao wanatumia fedha hiyo hiyo waliyohongwa kuwahonga wapiga kura. Hivi ndivyo mfumo fisadi ulivyojengeka. Mgombea ubunge ambaye alikuwa mbunge anatumia muda wake bungeni kupata fedha toka kwenye mashirika yawe ya umma au ya binafsi, wawekezaji wanaojipatia mikataba tata ya kuliumiza taifa ili atumie fedha hiyo kuwahonga wapiga kura na Takukuru ikija juu inaambiwa hiyo sivyo.
Kwa wale wenye nyadhifa serikali ambao si wabunge tayari, wanaiba mahali pao pa kazi na kupata mtaji wa kununulia ubunge kwa njia ya hongo. Urais nao kadhalika. Rejea taarifa za hivi karibuni kuwa rais ajae atapata urais kwa kutumia shilingi bilioni 20. Na aliyekadiria hivi alipatia hasa ikikumbukwa jinsi urais unaokwisha ulivyopatikana kwa fedha za EPA ambazo wahusika hawajawahi kutolea maelezo wala utetezi zaidi ya kujifanya hayawahusu wala hawahusiki.
Kimsingi, tokana na haya yaliyofichukiwa na Takukuru ni kwamba bila kuiondoa CCM watanzania wasitegee mabadiliko yoyote. Kama umma hautaamka na kuanza kuchukua hatua kuzuia jinai hii, wataendelea kulalamika na kugeuzwa shamba la bibi. Tumezidiwa na mataifa madogo kama Burundi na Burkina Faso! Kinachoendelea nchini Burundi ambapo rais anayemaliza muda wake anataka agombee kipindi kingine kinyume cha sheria ni ushahidi na somo tosha kwa watanzania kuwa wasipoanza kujenga tabia ya kukataa upuuzi wataendelea kufanyiwa upuuzi.
Kama Takukuru imenyima makali na mazingira mazuri ya kufanya kazi zake, waajiriwa wake wanalipwa kwa lipi wakati hawana la kufanya? Je kuna haja ya kuendelea kuiweka Takukuru chini ya ofisi ya rais ili aitumie kulinda watu wake na uoza wao? Je kuna haja ya kuendelea kuiamini CCM wakati imetuhumiwa kushiriki ufisadi kila aina? Nadhani hapa tunapata jibu ni kwanini watuhimiwa wa kuficha fedha nje ya nchi au wezi wa escrow hawakamatwi na kufikishwa mahakamani wala mabilioni ambayo mamlaka za Uswisi ziliamua kutoa ushirikiano yarejeshe hayarejeshwi. Kumbe tatizo si jingine bali utawala wa CCM! Japo hamfai, hongera Takukuru kwa kuisuta CCM kwa kuweka mambo hadharani.
Tunadhani hata wafanya biashara ya unga na majambazi wanaendelea na jinai zao bila wasi wasi kutokana na kujua kuwa kumbe watawala wanahitaji fedha kwa njia yoyote ilmradi waendelee kuwa madarakani.

Tumalizie kwa kuita CCM ijibu hoja za Takukuru na ijirekebishe kabla ya kuandaa uchaguzi ambao utaishia kuwa mchezo wa kutembeza hongo.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 6, 2015.

No comments: