The Chant of Savant

Friday 10 April 2015

Rais ameanzisha vurugu za ardhi nchini

 
          Kitendo cha rais Jakaya Kikwete kutwaa shamba la Galapo mkoani Manyara kimechochea sintofahamu nchini kuhusiana na sera ya ardhi. Baada ya rais kutoa amri ya kugawiwa kwa wananchi shamba husika baada ya kufuta hati ya umilki wa shamba toka kwa mwekezaji ambaye hakutajwa, wananchi wa wilaya ya Arumeru walimpa siku saba mwekezaji mwingine wa shamba la Karamu Cofee Estate kuwa ameachia shamba vinginevyo watalivamia na kugawana. Huu si ujumebe mzuri. Wananchi wameamshwa na kugundua kuwa kumbe hawana haja ya kuteseka na kuishi bila ardhi kwenye nchi yao huku watu wachache waroho wakijilimbikizia ardhi bila kujali wengine. Tunatamani hatua hii isiishie kwa wawekezaji tu. Iguse hata ardhi ya viongozi waroho waliojilimbikizia ardhi nchini mahali popote zilipo. Kwanini kutwaa mashamba ya wawekezaji wakati yapo mengine ya viongozi? Kama ni kutenda haki basi itendeke kwa wote bila ubaguzi. Hata ardhi zinazomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi sehemu mbali mbali nchini zitwaliwe na wananchi wasio na ardhi au wenye ardhi pungufu.
Hii maana yake ni kwamba rais amekurupuka. Ili kuepuka vurugu na hata maafa yanayoweza kutokea wakati wa utwaaji wa mashamba – ambao bila shaka utarudufiwa nchini –alipaswa kufanya utafiti wa kina na kuchukua hatua. Mfano, alipaswa kuanisha ni mashamba mangapi yako wapi na yana ukubwa kiasi gani. Pia angefanya utafiti kuhusiana na hali ya mashamba na wapi sheria ilikiukwa pamoja na kujua idadi ya watu wasio na ardhi ndipo atangaze. Sasa kwa kukurupuka huku, atapata kibarua kingine cha kutumia nguvu ya dola kuzuia utwaliwaji wa mashamba husika.
 Inasikitisha kuona rais anafanya mambo bila kufanya utafiti kiasi cha kuweza kuwa chanzo cha vurugu huko tuendako. Pia rais, angepaswa ajue waliovunja sheria na kutoa mashamba husika au walioyatwaa, kuyanunua au kuyamilki bila kuyaendeleza. Bila kufanya hivyo –tutake tusitake –rais ataanzisha vurugu bila sababu na hiyo vurugu hataikomesha bila kuleta madhara kwa wananchi husika.
Pia tungeshauri itungwe sera maalumu na madhubuti ya kuepusha kurudiwa kwa vitendo vya uporaji na umilki wa ardhi kinyume cha sheria. Bila kuwa na sera maalumu, vurugu zitaongezeka. Kisa cha Arumeru kinatukumbusha kisa kingine kilichotokea tarehe 17 Desemba 2013 katika eneo la mlima wa Kanyama, Kisesa huko Mwanza ambapo mwenyekiti wa zamani wa CCM wa mkoa wa Mwanza, Clement Mabina aliuawa kwa kupigwa mawe baada ya kumjeruhi kumpiga risasi mwananchi wakati wa kugombea eneo alilokuwa ametwaa Mabina. Je kuna Mabina wangapi waliojimilkisha ardhi ya umma nchini?
Mwaka juzi wananchi wa wilaya moja mkoani Kagera walikuwa wakilalamikia mbunge wao kujitwalia eneo kubwa la ardhi wilayani humo. Je wananchi hawa wakiona wenzao wa mikoa mingine wanavyofanya, watashindwa kujitwalia ardhi husika hasa ikizingatiwa ukweli kuwa wanajua walidhulumiwa ardhi yao?
Pamoja na hatua nzuri ya rais, kunatakiwa kuwepo mipango mizuri na ya kudumu si kwa ajili ya kuzuia kurudiwa kwa makosa husika bali kuwezesha ardhi husika kugawiwa kwa wananchi bila kuwepo vurugu, vitisho wala uvunjaji sheria. Japo tunaweza kulichukulia suala hili kama jambo la kawaida, si la kawaida hasa ikizingatiwa watu wetu wanavyoishi kama wakimbizi kwenye nchi yao huku wenye fedha na madaraka wakiwadhulumu mchana kweupe.
Uwepo wa sera madhubuti ya ardhi licha ya kutenda haki, utaepusha maafa yatokanayo na ugomvi wa ardhi nchini. Inashangaza kuwa wakati wa awamu ya kwanza ambapo kujitwalia mali ya umma ilikuwa mwiko na aliyefanya hivyo alichukuliwa hatua za kisheria hapo hapo hatukuwa na matukio kama haya. Kwanini tusirejeshe utaratibu uliotumika wakati huo kuepusha vurugu na migogoro ya ardhi.
Kwa sasa yamekuwa yakiripotiwa matukio mengi ya uvunjaji amani na hata kusababisha mauti yatokanayo na migogoro ya ardhi.  Hatuwezi kuendelea hivi. Inapotokea migogoro, licha ya kuruga amani, inasababisha kusimama kwa uzalishaji jambo ambalo linaathiri taifa kiuchumi hata kijamii ingawa wengi hawalioni hivi. Inapotekea mwananchi akauawa au kuua kutokana na ugomvi wa ardhi, si taifa tu linaloathirika tu, hata familia za wahusika zinaathirika kiasi kikubwa.
Zamani tulikuwa tukiwacheka majirani zetu wa Kenya na Malawi kwa kuishi bila ardhi kwenye nchi zao bila kujua kuwa kumbe hili litatufika siku si nyingi. Sasa hivi, hatuna cha kuwacheka. Kwani kuna watanzania wengi wanaishi bila ardhi na kama wanayo basi haitoshi. Kwa nchi kubwa yenye ardhi ya kutosha kinachogomba si ukosefu wa ardhi bali sera madhubuti ya uthibiti na ugawaji ardhi. Hivyo, kama tutakuwa makini, uwezekano wa kila mtanzania kupata ardhi inayomtosha ni mkubwa. Haiwezekani tukaribishe wakimbizi kwa malaki toka nchi jirani na kuwapa ardhi wakati watu wetu hawana ardhi ya kutosha. Fadhila huanzia nyumbani. Hatumaanishi kuwa tusiwape wakimbizi ardhi. Tunapaswa kuwapa watu wetu kwanza na kitakachobaki basi wafikiriwe hao wakimbizi. Pia tusiishie hapa. Tuwe na mipango ya kuwa na ardhi ya akiba kwa wengine watakaozaliwa ili kuepuka kuwa na watu wasiozalisha wala kujitegemea kwa vile hawana ardhi. Nchi yetu bado inategemea kilimo kama uti wa mgongo wa taifa. Je huu uti wa mgongo utafanyeje kazi bila wananchi kuwa na ardhi ya kutosha?
Chonde chonde rais na serikali yako, unda sera ya ardhi na mhakikishe kila mwananchi anapata ardhi ili aweza kuzalisha chakula cha kujikimu na kuuza kwa faida yake binafsi na taifa kwa ujumla. Chonde rais usianzishe vurugu hata kama hukukusudia kufanya hivyo.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

No comments: