The Chant of Savant

Tuesday 28 April 2015

Kijiwe chaasa wachovu kuchukia na kufanya mabadiliko


          Tukiwa tunahuzunika tokana na ajali za barabarani zilizosababishwa na ufisadi na utawala mbovu si tukazinyaka kuwa kuna majambazi makubwa yameingia kaya mkengeni kwa kupiga mabilioni. Inshu yenyewe ni kwamba washenzi hawa wenye roho za kinyama waliagiza mabehewa mabovu wakapandisha bei yake na kudai ni mapya wakati si kweli. Tulistuka kusikia kuwa waziri Sam Sixx amewasimamisha kazi badala ya kuwatupa lupango wakingojea kunyongwa.
Mgosi Machungi anaingia akiwa amekunja ndita kana kwamba atapiga mtu zongo. Anafungua moyo na kuronga, “Jamani mimesikia huu ujambazi wa bandaiini ambapo majambazi yamepiga njuuku kwa kununua mabehewa mikangafu na kudai ni mapya?” Kabla ya kuendelea anachomoa gazeti mkobani na kutupa tusome wenyewe nyuzi zenyewe.
Mipawa anadakia hata bila kusoma gazeti, “Huyu Sixx naye ni msanii. Kwanini asiwatupe lupango kwanza huku mali zao zote zikikamatwa ili kuchunguzwa wakiwa wanapoa lupango?”
Kapende anadakia, “Lupango ni kwa wezi wa kuku na vidokozi wadogo wadogo na vidagaa lakini si kwa mapapa.”
Msomi Mkatatamaa anadakia, “Ni kweli kaya imeibiwa jumla ya madafu bilioni 230 ukiachia mbali mabehewa husika kuletwa kutupwa kayani ambayo licha ya kupata hasara imegeuzwa dampo la taka hizi hatari. Nakubaliana na wachangiaji wanaotaka wahusika watupe lupango hata kunyongwa bila kungoja kupoteza muda kwa ndata kufungua kesi potofu na kuwapa mwanya majambazi hawa kushinda na kudai fidia.”
Kabla ya kuendelea, mheshimiwa Bwege anakatua mic, “Usemayo Msomi ni kweli. Kesho utasikia wamefikishwa mahakamani kama akina Idd Lion waliofilisi UdA na kuitwaa kwa kuwaweka vidhabi wachovu kujifanya ndiyo wamilki wakati wamilki wanajulikana kuwa ni akina Riz na wanene wengine.”
Anakoho kidogo baada ya kashata kumkwama na kuendelea, “Hapa hafungwi wala kushitakiwa mtu hasa ikizingatiwa kuwa ujambazi huu unawahusisha wakubwa wenyewe wanaojifanya kuushupalia.”
“Yakhe nasikia presha yanpanda Wallahi. Yaani wajalaana wajiibia kana kwamba hii kaya haina mwenyewe! Waleta mabehewa 150 kudampu hapa huku wakituibia na njuluku kana kwamba sie vichaa!” Mpemba analalama
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kukwanyua mic, “Jamani nyie mmeingiliwa na nini? Yaani hamngoji sheria ichukue mkondo wake? Kwanza, mna ushahidi gani kuwa hayo mabehewa ni mikangafu kama si kuzuazua?”
Kabla ya kuendelea Mgosi anamchomekea Sofi, “Da Sofi ngoja nikuchomekee. Kwei wewe ni wa kutiambia kuwa timeiingiwa na nini?”
Sofi hangoji, anakatua mic, “Halo Halo! Mmesahau ambavyo mmekuwa mkiniambia nimeingiliwa na nini siyo? Ama kweli mkuki kwa nguruwe!” anaangua kicheko huku akimtazama Mgosi anayeonekana kuudhika dhahiri.
Kanji anaamua kutia guu, “Kwanini Swahili penda tafsiri witu tofauti?  Mimi siku yote sikia ingiliwa ingiliwa. Sasa tatizo nini?”
“Kweli Kanji huwezi kuona ubaya hasa ikizingatiwa kuwa hii mikangafu imenunuliwa toka Bombei. Yaani kaya hii imegeuka shamba la bibi la magabacholi kupiga njuluku watakavyo.” Analalamika Mchunguliaji anayesoma gazeti kwa makini utadhani anatafuta majibu.
Mpemba anarejea, “Yakhe mie nshangaa sana. Yaani kaya imegeuzwa dampo la India. Mabehewa feki India. Madawa feki, India. Wawekezaji feki, India, vyangudoa wa kuja kwa kisingizio cha kucheza nziki bhangra na banjan nao watoka huko huko. Hata kunguru nao watoka huko huko kunani jamani?”
Kanji anastuka kusika Mpemba anavyotaja mitindo ya miziki ya kigabacholi. Anauliza, “Kumbe veve Pemba jua myuziki ya India! Iko veve ongea hindi?”
 Mpemba anajibu kwa kihindi, “Tame mari sathe dance karso yaani unataka kucheza muziki nami?”
Kanji anajibu, “dhanvaad yaani asante.”
Mpemba anajibu tena, “Tamaarūṃ svaagata cha yaani shukrani nawe.”
Kijiwe chote kimepigwa butwaa na jinsi Mpemba anavyokirudi kigujaraati.
Msomi baada ya kuona lugha gongana zinataka kupoteza mada anaamua kula mic,, “ Ami na Kanji tunawashukuru kwa kugonganisha lugha ingawa bado hamjaleta suluhu ya mada iliyoko mezani.” Anamgeukia Kanji na kusema kwa kigabacholi, “manne maaf karo yaani samahani na kuendelea. Nami nakimanya japo si sana ila hili si muhimu kwa leo. Turejee kwenye mada kwa kutoa shinikizo kwa lisirikali jizi liwashughulikie hawa majambazi wake vinginevyo tuingia mitaani au vipi?
Mipawa anakula mic, “Mie sidhani kama hawa mapapa watafungwa. Nani awafunge wakati wote lao moja? Jiulize akina Rugemalaya na Seti Singasinga wa wa escrew wako wapi zaidi ya kuwa mitaani wakipiga dili nyingine za kuiba kutumia bandari ya kule kwa akina waja leo waondoka leo?”
Mgosi anadandia, “Usiniumize ndugu yangu. Hata mimi sitegemei wezi wa HEPA wawashughuikie wenzao wa escrew. Nakubaina nawe lao moja.”
Mzee Maneno anachomekea, “Mie bado namuamini mzee Sam Sixx kwa vile ni mtu wa viwango.”
“Viwango ilikuwa zamani. Leo naye keshaingia kwenye maji taka. Mara hii umesahau alivyoua katiba ya mzee Jose Waryuba ya wachovu? Naye ni fisadi kama wenzake kwenye genge lao. Kwangu mle hakuna msafi hata mmoja bali unafiki na usanii mtupu.” Anajibu Kapende huku akikamua kahawa yake.

Kijiwe kikiwa kinaendelea si tukasikia king’ora cha treni ya kuelekea bara. Tuliamua kwenda kusimama relini kupinga hiyo mikangafu isitumike hadi kieleweke.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 29, 2015.

No comments: