The Chant of Savant

Friday 6 February 2015

TAKUKURU chunguzeni wizi wa UDA


         
          Hakuna ubishi kuwa sakata la unyakuzi wa Shirika la Usafiri Dar Es Salaam (UDA) bado ni bichi ingawa waliojiridhisha kufanya hivyo wanadhani yamekwisha. Ingawa waliofanya hivyo pamoja na mamlaka yanayoendelea kuwafumbia macho wanaweza kudhani watanzania wamesahau dhuluma waliyotendewa, ukweli ni kwamba wanakumbuka. Baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza kuwafikisha mahakamani waneemeka na watuhumiwa wa kashfa ya escrow, wananchi wameanza kurejesha imani nayo kwa kiasi fulani.
          Kama inachofanya TAKUKURU si danganya toto au bora liende, basi ni wakati muafaka kuitaka ichunguze hata huu utwaliwaji wa UDA. Kama TAKUKURU itasita kufanya hivyo, kwa vile haijaagizwa na bunge, itakuwa inashindwa kutekeleza mamalaka ya kuchunguza eneo lolote inalodhani au kuhisi kuna rushwa. Inaweza kufanya hivyo kwa kusikiliza vilio vya wananchi, kama hiki tunachotoa kupitia gazetini, au kuhisi kuwa kuna kila dalili za rushwa au ufisadi mahali popote nchini.
          Ni jambo la aibu kuona taifa letu linageuka shamba la bibi kwa kila aina ya wezi na matapeli kuja kujinyakulia mali za umma. Hatuwezi kuendelea hivi na tukajidanganya kuwa tutasonga mbele kimaendeleo kitaifa. Nasema hivi, kutokana na tabia ya wizi wa fedha na mali za umma kuanza kuota mizizi kiasi cha kuonekana kama kitu halali wakati ni jinai.
          Inatia aibu kuona kuwa hatukujifunza tokana na unyakuzi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira uliokuwa umenyakuliwa na familia na marafiki wa rais mstaafu Benjamin Mkapa. Japo tuliambiwa kuwa mradi huu wa umma ulirejeshwa, kuna maswali mengi kuliko majibu. Maana rais Jakaya Kikwete alimkingia kifua Mkapa akisema tumuache apumzike pamoja na kutenda jinai.
          Achovyae asali hachovyi mara moja. Baada ya Mkapa na marafiki zake kufanikiwa kujitwalia Kiwira kinyume cha sheria, walikwenda mbele zaidi na kushirikiana na wenzao wakiwamo mawaziri na wabunge ku jitwalia nyumba za umma wakati wafanyakazi wa umma wakihangaika na mahali pa kuishi. Ni bahati mbaya sana kuwa serikali iliridhia wizi wote huu.
          Baada ya utwaliwaji wa Kiwira na wizi wa nyumba za umma, sasa upo huu wizi wa wazi wazi wa UDA ambapo anayejiita mwekezaji mzawa anaonyesha kila dalili za kukwapua shirika hili la umma huku serikali ikitoa majibu hata yasiyoingia akilini ukiachia mbali kupingana na kujikanganya.
          Watanzania wengi bado hawaoni kama haki imetendeka kwenye uuzaji, au tuseme ugawaji, wa UDA. Kuna shaka kuwa nyuma ya UDA kunaweza kuwapo vigogo, ndugu au marafiki zao hata watoto wao. Maana kwa namna serikali inavyojifanya kutojali wala kujua kinachoendelea, lazima kuna namna. Kwanini tumejiruhusu hivi kuwa taifa la kuchezewa? Kama matapeli na wezi wengine wakishirikiana na wakubwa wanaweza kujiibia watakavyo, usalama wa taifa uko wapi? Na hiyo taasisi ya usalama wa taifa isiyojua kuwa usalama wa raia ni pamoja na mali zao kama watu binafsi na taifa ni ya kazi gani?
          Kwa vile TAKUKURU imeonyesha angalau kustuka, tunaitaka ifumue kashfa ya wizi wa UDA haraka sana iwezekanavyo.
          Na kwenye kashfa hii, TAKURURU isiangalia wala kujali kama waliotenda jinai hii ni wazawa au wageni. Mwizi ni mwizi hana cha ugeni au uzawa. Najua watetezi wa UDA wanaotumia kisingizio cha uzawa watakuja na wimbo ule ule wa jogoo kuwa anaonewa gere mzawa. Hakuna cha gere bali kutaka haki itendeke. Hata hawa watuhumiwa wa escrow wengi wao ni wazawa. Kweli mbomoa nchi ni mwananchi!
          Pamoja na kutopewa majibu ya kutosha, wengi wangependa kujua mtaji wa huyu anayeitwa mwekezaji kwenye UDA ambaye ameibuka ghafla bin vu. Hii ni kutaka kujua kama mtaji wake unatokana na wizi wa fedha za umma, ujambazi hata mihadarati ukiachia mbali kuweza kutolewa na wakubwa na washirika zao wasiotaka kujulikana.  Haiwezekani mtu anaamka tena kijana mdogo asiye na hata historia ya ujasiriamali anakuwa bilionea na kununua taasisi ya umma bila kuchunguza kujua, kwanza, ni mtu wa namna gani na pili amepatawa wapi huu ukwasi wa ghafla. Nani mara hii amesahau kisa cha tapeli wa kimarekani Bernard Madoff aliyewaibia wamarekani kwa kisingizio cha uwekezaji wakati alikuwa tapeli na mcheza upata? Tunaweza kuwa na akina Madoff wetu hapa lakini kwa uzembe na kuabudia wenye nazo bila kujali wamezipataje wakatuumiza badala ya kujifunza toka Marekani na kwingineko ambako matapeli wa namna hii wameumiza watu wengi.
          Hata wachambuzi wa Marekani walipoanza kumstukia Madoff waliitwa majina mbali mbali kama ambavyo uzawa unatumika kwenye kashfa ya wizi wa UDA. Hakuna cha wivu wala chuki bali kutaka, kama watanzania, tutendewe haki.
          Kama tulivyosema hapo juu, kama TAKUKURU itashikwa kigugumizi kama serikali basi waheshimiwa wabunge waingilie kati baada ya kugundua kuna ufisadi kwenye uuzwaji wa UDA.
          Mwezi Mei mwaka jana Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali mstaafu, Lodovick Utoh alikaririwa akisema, “Bodi ya wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hisa bila kupata kibali cha Serikali na hata CHC.” Taarifa kama hizi zinapaswa ziwe chachu kwa TAKUKURU na Bunge kuigilia kati kuokoa mali ya umma.
          Tunaweza kuuliza swali lile lile alilouliza bungeni mbunge wa Ubungo Mheshimiwa John Mnyika aliyekaririwa akisema, “Ni kwa nini watuhumiwa wameachiwa? Mheshimiwa Spika, haya yasipojibiwa tutaamini kuwa jambo hili linawahusu vigogo wa CCM na mnawalinda katika ufisadi huu.” Waziri Malima alijibu swali la Mnyika na kukiri kuwa suala la UDA lina mazingira yenye utata mkubwa.
Tumalizie kwa kuwataka wahusika waje na jibu mara moja ili mali ya umma iondoke mikononi mwa wezi na mafisadi wanaotaka kutuingiza mjini.
Chanzo: Dira.

No comments: