The Chant of Savant

Tuesday 3 February 2015

Msemaji wa Rais Anapokuwa Bingwa wa Matusi

 
          Bado watanzania wengi wanakumbuka jinsi Salva Rweyemamu, mwandishi wa habari wa zamani na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, alivyotumiwa na rais Jakaya Kikwete kuwachafua wapinzani wake mwaka 2005. Bado watanzania wanajua kuwa Rweyemamu alipewa kazi ya ukurugenzi wa Mawasiliano ikulu kama kulipwa fadhila kwa mchango wake ambao si haba ulimwezesha Kikwete kuupata urais. Wananchi wanajua kuwa Rweyemamu aliteuliwa si kwa sifa zinahohitajika bali kazi chafu aliyofanya.
          Pamoja na udhaifu huu, wengi walitegemea Rweyemamu lau angefanya kazi tena kwa umakini na staha ili kurejesha imani kwa wananchi. Ni bahati mbaya haikuwa hivyo tangia akae kwenye ofisi ambayo ataiacha chafu pale atakapoondoka.
          Hivi karibuni, Rweyemamu aliendelea kujisahau na kuwaita watu wapumbavu bila sababu. Alikaririwa akiwaambia waandishi wa habari walipomuuliza kuhusiana na waziri wa zamani wa Madini na Nishati Profesa Sospeter Muhongo kumfuata Rais Kikwete Uswizi. Bila aibu wala woga, Rweyemamu alijibu, “Acha habari zenu za kipumbavu hizo.” Je hapa upumbavu wa mwandishi ni upi? Hivi kweli kutafuta habari tena toka kwa mtu ambaye anaitwa mkurugenzi wa mawasiliano ikulu ni upumbavu au upumbavu ni mhusika kutojua wajibu wake? Hivi kati ya huyu mwandishi aliyevurumishiwa mitusi na Rweyemamu nani mpumbavu wa kweli asiyejua hata ukubwa wa hadhi ya ofisi anayoitumikia? Nini kimemkumba Rweyemamu hadi akajisahau hivi wakati akijua fika kuwa cheo ni dhamana?
          Baada ya kunogewa kutukana Rweyemamu wala hakuishia hapo. Kwani aliendelea kuvurumisha mitusi hata bila sababu. Alipoulizwa nini maana ya habari za kipumbavu na ni zipi alijibu, “Nimekwambia acha upumbavu, kama unataka habari nipigie na kama hutaki usinipigie, siyo kila kitu mnachoandika tu lazima nizungumzie.” Huyo ndiye mtu anayeitwa mtumishi wa umma anayeweza kuwadhalilisha watu tena wakiwa kazini.Huyu ndiye mtu eti anayeidaiwa kuwa mchambuzi mahiri na nguli katika fani anayoidhalilisha ukiachia mbali kuitumia kufanya unepi na kufika hapo alipo. Kama Rweyemamu na Kikwete wasingekuwa wameajiriana kwa kujuana, Rweyemamu alikuwa ni mtu wa kubanwa mbavu hadi naye akitoe maana ameonyesha kuimudu kazi ukiachia mbali kuwa kongwa shingoni mwa Kikwete. Nafasi aliyopewa ni kubwa kuliko uwezo wake. Na hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kwa Rweyemamu kujiropokea. Amekuwa akitoa majibu ambayo hata kenge hawezi kuyakubali kuhusiana na masuala mbali mbali.
           Wapo wanaoona kama Rweyemamu alikuwa ameajiriwa na Muhongo kama alivyowahi kuajiriwa na wezi wa Richmond ili kusafisha uchafu wao akashindwa. Kama si hivyo basi alikuwa anajenga mazingira ya kutaka amtumie kama alivyowahi kutumia kufanya kazi chafu ambayo kimsingi ndiyo iliyomfikisha hapo alipo. Maana kabla ya hapo aliwahi kutoa majibu ya hovyo alipowaambia waandishi wa habari kuwa Muhongo asingeweza kufukuzwa kwa vile ni mwanasiasa huku akisahau kuwa profesa Anna Tibaijuka alifukuzwa pamoja na kuwa mbunge tena wa kuchaguliwa ikilinganishwa na Muhongo wa kuteuliwa.
          Kwa kiwango cha elimu anachodaiwa kuwa nacho Rweyemamu kama hakughushi, umri na cheo alichoshikilia, alipaswa lau kuwa amewahi kufundishwa kama si kufikiri basi angalau baadhi ya mbinu za mawasilano hasa katika ofisi kubwa kama hiyo tena inayoshughulikia mawasiliano. Ofisi ya rais si ofisi ndogo hata kama ni kitengo chake. Inahitaji watu makini, wasiojiona wala kujivuna wala wasioongea bila mdomo kuwasiliana na kichwa. Ni ofisi takatifu kama alivyowahi kusema baba wa taifa kuwa Ikulu ni patakatifu pa patakatifu. Ni hatari kiasi gani mahali patakatifu pa patakatifu wanapojaa wezi na mabingwa wa matusi?
          Ni bahati mbaya kuwa Rweyemamu, tunda la uovu na dhambi ya kuchafuana, ameuendeleza kwa kuonyesha kiburi na majivuno. Wakati mwingine huongea kwa majivuno utadhani yeye ndiye rais. Kuna maisha baada ya bosi wake kuondoka madarakani. Laiti vyombo vya habari vingekuwa na ushirikiano, vingesusia kuandika habari zozote za ikulu ili tuone huyu mjivuni kama angeendelea kuwa ofisini anayoidhalilisha. Laiti angejua kuwa yeye kama msemaji wa rais anapotukana, rais ndiye anaathirika. Hata hivyo, Kikwete anapaswa kujiulaumu kwa kuteua mtu asiyefaa kwenye wadhifa huu. Hata kama alimtumia kuwazushia na kuwatukana washindani wake, huo wakati ulishapita. Alipaswa ampe chake na aachane na Rweyemamu. Kwa kufanya hivyo, hii aibu inayoikumba ofisi ya rais isingekuwapo. Maana, inavyoonekana, Rweyemamu hajasahu asili yake ya kutukana. Aliwatukana washindani wa Kikwete. Sasa amewageukia waandishi wa habari asijue wakiamua kumshughulikia ataachia ngazi ndani ya muda mfupi.    Tumalizie kwa kumtaka Rweyemamu aombe msamaha. Kama ataendelea kujifanya mwamba na bingwa wa matusi basi waandishi wa habari na vyombo vya habari wamshughulikie kwa kumsusia na kushinikiza aondolewe kwenye Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ili ateuliwe mtu mwenye uwezo na staha anayejua anachofanya na anayeheshimu kazi na hadhi ya wenzake. Haiingii akilini Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu igeuke kijiwe cha makuli na mabingwa wa matusi huku wakionyesha wazi kupwaya na kutokuwa na uwezo wa kutoa majibu ya maswali wanayoulizwa na kujenga mahusiano mema na sekta nyingine. Ikulu ni mali ya watanzania wote. Hata rais hana uwezo wala mamlaka ya kudhalilisha watu eti kwa sababu ni rais.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 4, 2015.

No comments: