The Chant of Savant

Tuesday 10 February 2015

Kikwete “usilinde” sheria kwa kuivunja


          Tukio la kudhalilishwa na kupigwa mwenyekiti wa Chama Cha Wananachi Profesa Ibrahim Lipumba limevuta hisia za watu wengi wakubwa na wadogo.  Kwanza tunalaani kitendo hiki cha hovyo na kinyama kinachokinzana na misingi ya utawala bora na wa sheria. Kitendo alichofanyiwa Lipumba ni cha kishenzi hata kama waliofanya hivyo wana amri toka juu. Tunakilaani kwa nguvu zote kitendo hiki cha kihayawani. Wapo walioliona kama dalili za utawala msonge wa chama kimoja wenye kujawa na ukandamizaji wa demokrasia na mawazo pinzani. Wapo walioshangilia hasa wale wanazi wasiopenda mabadiliko. Katika wote aliyestua wengi ni rais Jakaya Kikwete kuonekana kushangilia na kuunga mkono udhalilishaji, ukandamizaji na matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Kikwete alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano mingi kuliko chama tawala, ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja sheria.” Inasikitisha sana. Ni bahati mbaya Kikwete hakusema ni sheria gani ilivunjwa na kama adhabu yake ni kudhalilishwa na kupigwa. Kimsingi, Kikwete alishindwa kuficha furaha yake huku akitetea wazi wazi uvunjaji wa sheria kwa kisingizio cha kuilinda sheria.
          Haiingii akilini kwa polisi kugeuka wapelelezi, wakamataji na mwisho mahakimu. Huu si utawala wa sheria anaoongelea Kikwete vinginevyo uwe na maana tofauti na ile sahihi na inayoingia akilini. Sijui kama Kikwete ndiye ambaye angepata kipigo alichopata Lipumba kama angeyasema haya anayosema. Hata hivyo haishangazi kusikia maneno yanayoshabikia uvunjaji wa sheria na haki za binadamu kutoka midomoni mwa kiongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na rais wa Jamhuri. Nani mara hii kasahau maneno ya kichochezi ya waziri wake mkuu Mizengo Pinda aliyewachagiza polisi kuwapiga wapinzani na wakafanya kweli hadi kwenda mbali wakaua? Huu ndiyo utawala wa sheria anaomaanisha Kikwete?
          Wahenga wana msemo kuwa ukimpiga mzazi wako nawe utapigwa na mwanao. Ipo siku CCM watajikuta kwenye upinzani na legacy hii ya ukandamizaji waliyoasisi na kuenzi itawarudiwa wao wenyewe. Ni bahati mbaya kuwa tumefika hapa ambapo viongozi wetu hawapimi maneno yao kabla ya kuyatamka. Hawajali athari za matamshi yao. Wanaangalia ulaji wao bila kujali kuwa nchi hii ni mali yetu sote na kufanya mikutano au maandamano ni haki ya kikatiba.
          Kama tukiweka makosa ya Lipumba na ya Kikwete kwenye mizania, uwezekano ni kwamba Kikwete ametenda kosa kubwa kuliko Lipumba. Maana alichofanya Lipumba na waandamanaji wenzake ni kufaidi haki yao ya kikatiba ya kuandamana. Ajabu ya maajabu hata katiba inapovunjwa kwa kukandamizwa akatokea mtu tena kiongozi wa juu akasema maneno ya ajabu kama haya, unapata shaka na busara ya kufanya hivyo.
          Japo Kikwete yuko kwenye ngwe yake ya lala salama, anaacha legacy chafu hasa uvunjaji wa sheria na matumizi ya vyombo vya dola. Inashangaza ni wapi serikali inapata askari wa kuwapiga wapinzani wakati polisi hawa hawa hawatoshi hata kujilinda ukiachia mbali kuwatelekeza wananchi. Rejea kuvamiwa kwa vituo vya polisi na kuuawa kwa baadhi ya polisi ukiachia mbali kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na uharifu. Hii maana yake ni kwamba polisi wameshindwa. Serikali pia imeshindwa. Na hawa wanaounga mkono ukandamizaji wa demokrasia na haki za kikatiba wameshindwa tena vibaya sana.
          Kama Kikwete hakuwa na la kusema heri angejinyamazia kuliko kumwaga upupu na kuchochea mtafaruko.  Heri Kikwete angetumia jeshi lake kupambana na uharifu na ufisadi badala ya kuhangaishwa na wapinzani wanaofaidi haki zao za kikatiba.  Rais anayevunja katiba hafai hata kama anaweza kutumia maguvu ya serikali yake na vyombo vya dola kuendelea kuwa madarakani. Watanzania wote – bila kujali itikadi zao za kisiasa na mafungamano – wana haki ya kufaidi haki zao za kikatiba mojawapo zikiwa ni zile za kukutana, kuandamana na kueleza mawazo yao bila kuathiriwa na sheria wala mtu au kikundi chochote. Inashangaza ni wapi Kikwete anapopata mshipa wa kuunga mkono jinai wakati serikali yake inanuka uovu na ufisadi kuanzia mauaji ya raia wasio na hatia hadi wizi wa fedha za umma ukiachia mbali uvujaji wa raslimali na uzembe.
          Kwa muda mchache aliobakiza madarakani, Kikwete angejikita kwenye kusafisha maovu aliyoacha yakazaliana kiasi cha nchi kujiendea kama haina serikali. Hili ni la msingi sana kwa mtu ambaye serikali yake ina sifa hasi hasa kulinda na kushiriki ufisadi. Laiti Kikwete angejua kuna maisha baada ya ikulu, asingeunga mkono uvunjwaji wa wazi wazi wa katiba. Japo tunamheshimu sana Kikwete, kwa hili amenoa au tuseme amekosea na aombe msamaha. Haiwezekani tuendelee kuwa nchi ya kipolisi huku tukiuhadaa umma kuwa huu ndiyo utawala wa sheria. Utawala gani wa sheria inayobagua ambapo majizi yanaendelea kutesa huku umma ukiangamia kwa kusikinishwa na kuteswa hata unapodai kutendewa haki. Hatutaki sheria za mwitu ambapo mwenye nguvu ndiye mfalme. Tunataka utawala wa kweli wa sheria na si matumizi ya sheria kibaguzi kwa kulinda kikundi kidogo cha walaji na wezi.
Tumalizie kwa kumtaka Kikwete asilinde sheria kwa kuvunja katiba na sheria. Alichofanyiwa Lipumba ni kitendo cha hovyo na cha kinyama na kidhalilishaji kwa aliyetendewa na waliotenda na hata waliotoa amri na wanaoshangilia.
 Chanzo: Tanzania Daima Feb., 11, 2015.

No comments: