The Chant of Savant

Saturday 28 February 2015

Mnaua elimu wasomi wametosha eeh!

Kaya yetu inasifika duniani kuwa ya wasomi. Rais wetu ni profesa. Wengi wa mawaziri na wabunge ni madaktari wasiotibu.Usiniulize kama wameghushi au la. Kaya ina wasomi kila tabaka.Wapo wa ukweli, wa kughushi, kubaingaiza,kuungauga hata feki, kujipachika vyeo vya kisomi. 
Yote ni matokeo ya marehemu Mwalimu Mchonga kutoa elimu ya bure. Je alifanya hivi kwa vile alikuwa ticha? Ngurumbili ni viumbe wa ajabu na tatanishi. Wakikosa wanalaumu, wakipata wanakufuru. 
Baada ya “watalaumu” wetu wa ‘taalauma’ kugundua kuwa kaya ina wasomi kiasi cha kazi kuadimika, wengine kushinda baa, kula msosi mzito wa viroba na kuvuta mibangi kama mimi, wamekuja na ubunifu wa hali ya juu. 
Wameamua kuanza kujaza ujinga kisera ili kupunguza tatizo la kuwa na wasomi wengi wafanyao kaya isilike wala kutawalika kiulani. Hivyo, wamekuja na mbinu ya kutukuza ujinga na kulaani usomi. Wameruhusu watu –tena wazito –waghushi taaluma huku wengine wakizawadiwa vyeo vizito vizito kitaaluma bila kujua hata mlango wa darasa la kusomea vyeo hivyo ulipo! 
Kutokana na kuwa na wasomi wengi –tena wanaoongea Kiswa-Kinge hata mjengoni –wataalamu wamekuja na gia ya kuwakata kilimilimi. Wanapendekeza Kiswaa kiwe lugha ya kufundishia kunzia vidudu hata vyoo vikuu. Upo hapo mshirika? Tuache utani. Hiki kinachoitwa sera mpya ya ilimu si chochote wala lolote bali mauti ya vizazi vijavyo. 
Hivi, uliposoma wakati wa mzee Mchonga –tena bure –ukasoma vitabu kibao kuanzia Adili na Nduguze, Kusadikika, Hamkani si Shwari Tena, Mfanyabiashara wa Venice, African Child, Things Fall Apart, No Longer at Ease, The Great Ponds, The River Between, New life in Kyierefaso na Songs of Lawino ukaamua watoto wetu wasome kitabu kimoja unamaanisha nini kama si kuwajaza ujinga? Let’s face it folks. 
Juzi nilisikia daktari mmoja feki akisema kuwa kwa kufundisha kwa Kiswaa wanagezi wataelewa sana tofauti na sasa ambapo kimombo eti kinawafanya wasiambulie kitu. Uongo. Mnaua ilimu kwa kusingizia lugha? Basi kafundishe kwa Kimakonde au Kisambaa au Kitumbuka muone balaa lake. Hakuna cha lugha wala nini bali sanaa na kukosa ubunifu. Wekezeni kwenye ilimu. 
Wape maticha motisha na marupurupu mnayopotezea kwa wanasiasa muone kama haitapaa. 
Sikubaliani na upuuzi wa kusoma kitabu kimoja. Hata hizo dini, pamoja na kuwa na kitabu kimoja kimoja, ndanimwe kuna vitabu vingi.Hamjui kuwa kutumia kitabu kimoja ni kuua vipaji vya wanafunzi ukiachia mbali kuwamaliza watunzi na wachapishaji? 
Naona hili limefanyika ili wavivu fulani wanaoandika vitabu vya hovyo wapate soko. Kama si hivyo mbona vitabu vyangu havifundishwi maskulini wakati ni vya kisomi na vimekwenda shule ile mbaya.Tena, vingine vimechapishwa nje kuonyesha vilivyo bomba. Hata hivyo, nani atatumia vitabu vyangu wakati vinawasuta? 
Watu wameendekeza usanii na ufisadi hadi kwenye ilimu.Huu ni ushahidi wa kutoona mbali na kushindwa vibaya sana.Vijana siku hizi hawana motisha wa kusoma kwa vile hakuna ajira ukiachia mbali kuhalalishwa kwa usanii,uhalifu na mazabe mengine.Kwa sasa vijana wanatamani kuwa wasanii wawe wa kweli au kisiasa, au ikizidi ikapungua, majambazi ili waukate kama mafisadi na majambazi wakubwa wa kalamu wanaowaona wakiwaongoza njia ya kuelekea kwenye utwahuti. Huwezi kubariki jinai ukategemea watu wawe na motisha wa kufanya kazi kwa bidii au kusoma. 
Wahangaike na kusoma ili iweje wakati mtu ananyaka silaha ya SmG usiku mmoja na kuamka tajiri na hakuna anayemhoji? Rejesheni sheria ya maadili na kuondokana na madili muone kama ilmu haitapaa.Wahangaishwe na kusoma ili iweje iwapo ajira nyingi zinaangalia udugu na rushwa badala ya elimu? Mara hii mmesahau skandali ya uhamishaji ndani ya Wizara ya Mambo ya Uani ya Nchi, ambapo waajiriwa wote walikuwa ‘dugu’ za mabosi wa idara siyo? 
Nenda bandarini, uhamiaji, viwanja vya ndege, undata, TrA, mizani, mipakani, Benki Kubwa aka Belly of Tembo (BoT) iliyojaa watoto wa vigogo ambao wamefoji midigilii na kwingineko kwenye njuluku ya chapchap. Sijui ile kashfa ya BoT kujaa watoto wa vigogo iliishia wapi? Nani anakumbuka iwapo walevi na wachovu wana sifa kuu ya kusahau kirahisi wanaposahauliswa kwa movies mbali mbali?  
Nani anaongelea tena escrow au kurejesha mshiko kutoka Uswisi? Kila kitu kimesahaulika. Mambo shwari kwa wenyewe kula kaya.
Tukirejea kwenye ilimu wakubwa wana shida gani iwapo wanapeleka vitegemezi vyao ughaibuni kupata elimu ya nguvu ili waje vitawale walevi?   Tena wanafanya hivyo kwa kutumia mshiko wa walevi na wachovu waupatao toka kwenye kodi. Nani anajali iwapo wenye kaya wana namna ya kuwajaza ujinga walevi ili waendelee kuwaibia? Ndiyo maana hata hawakuona aibu kuja na mauzauza haya wakayaita nyenzo ya maendeleo bila kufafanua kuwa maendeleo yenyewe ni ya kwenda nyuma au shimoni. 
 Mara hii mmesahau tambo za mgosi Jose Makambale kuwa mwanae amesoma, tena, ughaibuni. Hivyo, angepewa uwaziri na kweli akaupata kiasi cha kutaka hata urahisi? Unadhani angekuwa amesomea kwenye shule za “shule za kata elimu” angekuwa na ubavu wa kumwaga nyodo hadharani asihofie wachovu wangemtolea uvivu? Alisema akijua wengi wa walengwa ni hamnazo wasioweza kumstukia na kuzuia jinai yake.  
Unafikiri  tambo hizi angemtolea mzee Mchonga mwanae angapata huo uwaziri?  Thubutu. Nani anajali iwapo mambo yamebadilika kiasi cha makaburi ya watakatifu kusafishwa na wenye dhambi?  
 Kwa vile wanaopaswa kufaidi kaya wanahisi wasomi wametosha, lazima waongeze ujinga ili kutawala kiulani. Mara hii mmesahau maneno ya mzee Mchonga aliposema kuwa wajinga hutawaliwa kirahisi kuliko wasomi. Hata hivyo, mzee hakuwa na mtima nyongo.  
Aliendelea kutoa elimu ya bure kwa kila kitegemezi bila kujali mbari wala kipato. 
 Matokeo yake wale waliofaidi elimu hii wameisahau na kuanza kufanyia majaribio vichwa vya vitegemezi vyetu. Mwenzenu hawanipati nitahamishia changu baa lau kifyatuke kama mimi na kunena:Ueni elimu wasomi wametosha. 
Mtajijuu.
Chanzo: Nipashe Feb., 28, 2015.

No comments: