The Chant of Savant

Tuesday 7 October 2014

Kijiwe chawapongeza walokataa utwahuti

Baada ya wahishimiwa wenye akili kuliko Abunwasi kuwaliza matwahuti wanaohangaika kuchakachua katiba yetu kwenye Bunge Maalum la Kuula kule Dom, kijiwe kimeamua kuwatumia salamu za pongezi kwa kitendo hiki cha kizalendo na kishujaa.
 Mijiinga anaingia akiwa amebeba gazeti la Wameipata Leo anaamkua na kusema, “Mmesikia jinsi Njaa Kaya na Sam Sixx walivyoingizwa mjini na wahhishimiwa waliotaka kuwaingiza mjini wasijue nao wana akili tena zaidi yao?”
“Kwa furaha nilo nayo kwa baadhi ya waja wenye taamuli kuanza onyesha njia, natoa ofa kwa yeyote atayekuja kijiweni hapa wallahi.” Mpemba anasema huku akitabasamu.
Mbwamwitu anadaka mic, “Wote wamenifurahisha isipokuwa Ali Kesi ambaye ameonyesha uzabazabina kama Joni Chibuda buda la kutupwa. Sijui kama akili zake ni sawa sawa. Maana ukiangalia alivyokuwa akijonyesha mzalendo kumbe hovyo.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia daruga, “Nyinyi inaonekana hamuwajui wataka sifa na wachumia tumbo. Kwa ninavyojua visasi vya baadhi ya wanasiasa, nilitegemea Kesi angepiga kikesikesi kama alivyofanya.”
Kabla ya kuendelea Kapende anakwanyua mic, “Kwanini unasema ulijua atakavyopiga kura au mshirika mna uhusiano na ngurumbiri huyu?”
Msomi abwia kombe lake na kujibu, “Ni rahisi kujua ni kwanini alipiga kura hivyo.  Kwa vile waliotishia kumnyuka walipiga kura ya kupinga, yeye badala ya kuangalia mstakabali wa kaya aliamua kupiga kupingana nao bila hata kujua kuwa suala lenyewe si la binafsi bali kikaya.”
“Hapo nimekupata.” Anajibu Kapende.
Mbwamwitu anamuuliza , “Umetosheka?”
Kapende anajibu, “Unaonaje? Unataka zaidi?”
Baada ya kuona utani unaanza kuharibu mada Mgosi Machungi anaamua kuokoa jahazi, “Sasa tinaweza kuanza kupumua kuwa huu upuuzi hautaruuusiwa upite kwa ajili ya kuhujumu sisi na vizazi vyetu. Sijawahi kuona mijitu inayofikii kwa matumbo kama hii. Mungu kweli si Asumani! Hawa waioamua kupiga kura ya hapana wamerejesha heshima ya uhishimiwa uliokuwa umeanza kugeuka uishiwa.”
“Tuanze kupumua! Unadhani hawa manyang’au na matwahuti wataacha mizengwe yao kutubambika mkenge ili waweze kujinusuru na vifungo huko tuendako kama tutapitisha chate letu wenyewe?” Anauliza Mipawa huku akiwa anamuangalia Sofia Lion Kanungaembe ambaye mara nyingi huwa ana bifu naye sambamba na Kapende na Mijjinga.
Kana kwamba walipeana ishara kuwa akiongea atajibiwa na Sofi. Sofi anakwanyua mic. “Uwe na adabu. Msipende kuita watu na heshima zao majina ya ajabu ajabu. Hivi twahuti kati yako na hao unaowatukana matwahuti nani? Shika adabu na adabu ikushike.”
Mipawa hangoji Kapende aliyekuwa akijanaa kujibu afanye hivyo. Anakula mic, “Watu na heshima zao ukiwaona utawajua au unaota mchana dadangu? Heshima na ukubwa wa mtu si cheo alicho nacho bali matendo yake. Kuna watu wadogo sana wasio na vyeo wala kazi lakini wana heshima kuliko hao wezi wanaotapanya njuluku zetu huku umaskini ukizidi kutumaliza. Kwangu mwizi hata hawe mkubwa kama tembo au awe na cheo kikubwa kama Sam Sixx ni mwizi tu.”
Kanji hakubaliana na mawazo ya Mipawa . Anaamua kula mic kumhami mshirika wake Sofia. Anasema, “Hata mimi pana taka tukana vatu howo howo. Hata kama kuba nafanya kosa dogo hapana tukana tusi kubakuba hiwo.”
“Kanji matusi unayajua au unayasikia. Hata hivyo, wewe una kosa gani wakati una uraia mia na moja?” Kapende anachomekea huku akigonganisha mkono na Mipawa.
“Nadhani kumjibu Kanji na Sofi mnapoteza majibu na muda wenu. Laiti ingekuwa kwao Bombay sijui kama Swahili iko pewa nafasi toa vazo kama Kanji pewa hapa kwa Swahili.” Mbwamwitu anabukanya Kiswahili cha Kigabacholi huku akimwangilia Kanji kwa dharau. Kanji anachekacheka japo moyoni anatukuta.
Mchunguliaji aliyekuwa bize akisoma gazeti anaamua kula mic, “Mimi pamoja na kuwapongeza hawa mashujaa wa ukombozi wa wachovu nasema. Laki tatu kuleni na kura wanyimeni ati! Yote tisa. Kumi namuonea huruma kiherehere Sam Sixx ambaye anajitia kuendesha show hii wakati mwenyewe yuko majukuu kwa mzee Joji Kichaka akitanua na vimwana, waramba viatu hata makalio na marafiki zake wakitanua.”
“Nadhani wanasharia waandae kesi dhidi ya hawa wafujaji walioruhusu njuluku za wachovu kuvunjwa kwenye upuuzi ambao sasa unapigwa chini na kuthibitisha uhalali wa umma. Kuna haja ya kupiga chini hiki kiini macho na kuonyesha ulimwengu kuwa wachovu wakijitambua na kuungana wanaweza kufanya lolote walitakalo kama jamii. Ni somo kwa walevi wa maulaji na madaraka wanaodhani kuwa walipo ni ujanja kiasi cha kupatumia kutetea uoza na upuuzi mwingine.” Anaongea Msomi huku akibofya ki-tablet chake.
Anabwia kahawa na kuendelea, “Kilichotokea kinapaswa kuungwa mkono na kuendelezwa hadi mwisho wa mapambano. Tukatae hii hujuma ya mafisi na mafisadi.  Hawa mashujaa tuwaenzi, kuwahehshimu na kuwaunga mkono kuzuia kula ya maoni. Bila kuwazuia hawa matwahuti, wataendelea kuchezea njuluku zetu kwenye hujuma yao. How can a cabal of criminals enact a document of the people? Who authorized them to do so? Oh! Samahani nimepandisha mori kiasi cha kuongea ukameruni.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Sam Sixx. Kwa hasira na usongo si tuliamua kulikimbiza huku tukizomea tukitafuta kumnyofoa na kumtia adabu!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 8, 2014.

No comments: