The Chant of Savant

Tuesday 16 September 2014

Wanakijiwe wavaa magunia na kujipaka majivu

Baada ya wakubwa wenye ajenda zao za siri za kutajirishana na kutubambikizia katiba wakiitumia kama kisingizio cha kuiba njuluku zetu kuja na maigizo yao, kijiwe kimekaa kulaani na kuomboleza kwa msiba wa njuluku za wachovu na makapuka wa kaya hii.
Baada ya mkuu kutangaza alichoamua ambacho, kimsingi, si uamuzi kitu bali kubariki wizi wa njuluku za walevi na sanaa tupu, kama kijiwe cha watu wanaoona mbali tunalaani na kupinga mchezo mzima ambao ni mauti kwa kaya yetu. Hivyo, tumekubaliana kuvaa magunia na kujipaka majivu na kuombolezea kaya yetu ya Danganyika.
Mijjinga analianzisha, “Jamani mmepokeaje huu uamuzi angamizi wa kuendelea kuibiwa njuluku zetu huku rasimu ya Waryuba ikiendelea kubunguliwa na kuchakachuliwa chini ya shinikizo la Sam Sixx na Njaa Kaya na wenzao?”
“Namsikitikia Njaa Kaya kwa kupoteza fursa ya kuandika katiba na historia kwa pamoja.” Anachomkea Kapende huku akijifuta majivu usoni na kuweka gunia lake vizuri.
Mgosi ambaye kweli gunia limemkaa huku uso wake ukijaa ndita, anakula mic, “Jamani tinapaswa kuomboeza kwei kwei. Tiomboeze kwa vie timeshindwa kuingia mitaani na kudai haki yetu. Hakika timerogwa na kuaaniwa hakuna mfano!”
Mpemba anakwanyua mic, “Hakika yasikitisha sana kuona tuliotegemea wangekuwa mihimili ya ustawi wa kaya wanakuwa ndiyo wabomoaji wa kila kitu hasa kubariki BMK kinyumenyume.”
 Mipawa anachangamkia mic na kuronga, “Wanatumia mabilioni yote haya kwa nini iwapo wanachofanya, licha ya kutotambuliwa kisheria, ni jinai tupu? Wanajitahidi kumhadaa nani wakati kila kitu kiko wazi kuwa kinachoendelea ni wizi na ufisadi wa kutisha? Kwa mwenye kufikiri sawa sawa hawezi kuruhusu bilioni 200 ziibiwe na wasaka tonge na bado akajipiga kifua kuwa amefanya maamuzi magumu.”
          Mzee Maneno anachomekea, “Ninawashangaa wapingaji wanaojivua nguo na kukubali kutumiwa. Je hawa viranja wa upingaji nao wanajiona wamefanikisha kitu au ni kusifiana upuuzi?”
Msomi, huku akiweka vizuri gunia lake lisimbane nyeti anakula mic, “Tumelaumu sana hawa wanasiasia. Kwanini tusiangalie upande wa pili ambao ni wa waathirika? Je fikra zao ndiyo mwisho wa kufikiri au kigezo cha kila maamuzi? Wao wamefanikisha walichotaka au wameweka msingi wa kufanikisha wanachotaka.  Je wachovu wamefanya nini kupinga na kuzuia jinai hii inayofanyika mchana wakati wao wakishuhudia? Washikwe wapi ndipo wastuke?”Anajifuta majivu kwenye mstachi na kuendelea, “Wachovu nao wako wapi kiasi cha kila siku kuwa mashahidi wa maangamizi yao? Je hizi njuluku wanazohongana kwa mambo ya kipuuzi zingesaidia wachovu wangapi lau kupata mitaji kuanzisha shughuli za kimaisha ukiachia mbali kuchangia huduma za kijamii? Nani anajali iwapo kila mtu anajifanya hamnazo na haya hayamhusu?”
Sofia Lion aka Kanungaembe hangoji. Akapoka mic, “Mie sioni ubaya mkuu kuruhusu BMK liendelee ikizingatiwa kuwa bado hatujapata katiba mpya. Naona amefanya uamuzi mgumu.”
          Mhe. Bwege hangoji. Anakula mic, “Dada yangu Sofi umeingiliwa na nini? Yaani unaona kuruhusu njuluku za wachovu ziendelee kuibiwa ni maamuzi magumu! Kweli ni maamuzi magumu yatakayo roho na akili ya mwendawazi. Sioni mantiki katika hili hata kidogo.”
          Kanji, kama kawaida yake lazima ampige tafu mshirika wake. Anakatua mic, “Kuu fanya wema. Yeye angalia sheria. Ile nalalamika juluku napoteza muda. Juluku ya umma haiko umma bwana.”
          Mpemba anarejea huku akiweka vizuri kigunia lake kiasi cha kuwa kichekesho kwa linavyomhangaisha. Anasema, “Yakhe nashukuru sana kwa wazo la kuvaa magunia na kujipaka majivu. Natamani hata Njaa Kaya au Sam Sixx hata wanasiasa wangevishwa magunia na kupakwa majivu lau waone yanivyokera na kusulubu. Hakika ujumbe huu umefika mwake.”
          Mbwamwitu aliyekuwa kimya akiangalia jinsi magunia na majivu vinavyotusulubu aliamua kuchangia, “Mie naona hapa mada si kutamani wangevishwa  magunia na kupakwa majivu. Kwanini tusiende huko waliko tukawapake majivu na kuwavisha magunia lau watie akilini?”
          Mijjinga hakubaliani na hoja hii, “Let’s try to be a little bit realistic. Tutawafikiaje wavujaji wa njuluku zetu iwapo wana walinzi? Naona njia ya kuwapaka majivu na kuwavisha magunia ni kupitia kwenye sanduku la kura mwakani. Tuwapige chini ili wapinzani wachukue waje waandike katiba inayoingia akilini kuliko huu upuuzi na uchakachuaji.”
          Pwenti za Mijjinga zimemshawishi Msomi. Anakwanyua mic na kusema, “Usemacho Dk. Mijjinga ni kweli. Tuepuke ndoto na kuweza kujiingiza kwenye fujo kiasi cha kupoteza hoja. Sanduku la kura linaweza kuwa muarobaini wa kuleta ukombozi wetu hapo baadaye.”
Kabla ya kuendelea, Mgosi anachomekea, “Tinaweza kuwabwaga kwenye sanduku la kura wakachakachukua kama waivyozoea kufanya tikajikuta pae pae. Naona tifanye mpango tiwapige zongo kwanza au tiombe dua mbaya wapukutike. Tifanye mageuzi ya kwei kwa kugomea uchaguzi mwakani ii tipate katiba muafaka itakayolinda na kuheshimu kura zetu.”
Kila mtu anatikisa kichwa kuunga mkono hoja nzito za Mgosi isipokuwa Sofi anayebeua midomo huku akimtazama Kanji.
Kijiwe kikiwa kinanoga si Mbwamwitu akachomoa majibu na gunia ili kuwapaka na kuwavisha akina Kanji na bi Sofi. Acha watimke mbio nasi tuwakimbize tukizomea!
Chanzo: Tanzania Daima Sept, 17, 2014.

No comments: