The Chant of Savant

Wednesday 3 September 2014

Tubinafsishe Bonge la Mchongo wa Kukwapua

Baada ya kuchoshwa kuchefuliwa na kuchukizwa na wizi unaoendelea Mjengoni chini ya kinachoitwa Mjengo Maalum wa Katiba au Kuhomola (MMKK) aka Bonge la Mzengwe wa Kukwapua (BMK), Kijiwe kimesukuti na kuja na suluhisho la kuuzuia, kubinafsisha ilipo nguvu ya Bonge ya Mshiko Kirahisi.
          Mgosi Machungi, kama kawa, hakosi vituko na vibweka. Akiwa amemaliza kuagiza kahawa yake na kubwia kidogo na kupata stimu anakwanyua mic, “Waheshimiwa kwanza nipeni makiwa kwa kufiwa na shemeji yangu Coltide huko Keko kwa pressure.”
          “Du pole sana Mgosi. Huyu kwini namdeku sana. Ni jana tu niliongea naye. Alikuwa mchangamfu hakuna! Kweli amekufa! Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.” anasema Kapende huku akimpa mkono wa makiwa Mgosi.
“Kufa hakuna saa wala sekunde. Hata kama ungekuwa umepiga mbonji naye: Kullu Nafsin Zaikatul Maut.” Anasema Mbwamwitu akijfanya shehe anayeujua umanga.
          Kama mila na desturi ya wastaarabu, tunamchangia uchache Mgosi lau aende akauguze majonzi ya kuondokewa na shem wake.
          Baada ya kupokea mchango Mgosi anaendelea, “Nawashukuu sana waheshimiwa kwa michango yenu. Muhimu nataka niseme kuwa huu msiba wa shemeji yangu si mkubwa kama huu wa njuuku zetu zinazoibiwa kue kwenye Mjengo Maalum wa Kuiba sorry Mjengo Maalum wa Katiba. Hivyo, nawaomba tikubaiane kutafuta suluhu ya wizi huu wa mchana.”
          Mpemba akiwa anajiweka vizuri kwenye benchi, anapoka mic, “Yakhe mie nkubaliana nawe. Lazima tusake suluhu ya kukomesha huu ujambazi mbuzi wa kusaliti kaya kwa vipande thelathini vye fedha Wallahi. Napendekeza tuondoe shilingi ili wasipate hiyo laki tatu ya kupeana kwa siku kwa kufanya madudu.”
          Msomi Mkatatamaa akiwa anampa gazeti Mchunguliaji anadandia mic, “Ami tuondoe shilingi wapi wakati malipo haya ya haramu hayatokani na bajeti bali hazina iliyogeuzwa shamba la bibi?”
          Mipawa akiwa anaweka vizuri shati lake jipya anakwanyua mic, “Kwa vile wiki jana tulipokwenda kulifunga tuliletewa ndata tukachelea kuwaumiza na kuzushiwa tumeanzisha vurugu, napendekeza tutafute mwekezaji ili aendeshe zoezi la kuandika katiba mpya. Maana, kama wahusika wameonyesha wazi walivyo hamnazo, tutafute mwekezaji mwenye akili lau afanye kazi hii.”
          “Napendekeza mwekezaji mwenyewe awe Kijiwe hiki kitukufu chenye watu wenye akili zinazochaji na kucheka kama jiko la mchina.  Au vipi?” anajibu Kapende huku akiendelea kubwia kahawa yake.
          Mgosi Machungi anadakia, “Dk Kapende ni kama umesoma mawazo yangu. Sema nina tofauti kidogo. Kwani, napendekeza tibinafsishe ikuu kwanza. Maana ndiyo chanzo cha wizi huu. Bia kubinafsisha ikuu kwanza yote ni bure. Tihakikishe tinakata mzizi wa fitina kwa kubinafsisha ikuu. Ikiwezekane tiichukue sisi wenyewe na kuendesha kaya.”
          Kabla ya Mgosi Kumaliza, Mbwamwitu anamchomekea, “Unadhani mkuu aliyeko ikulu akifaidi na kutanua na watu wake tena bila kufanya lolote zaidi ya madudu atakubaliana na hatua hii?”
          “Akatae kwani ikuu ni mai ya mama yake? Ikuu ni mai yetu bwana tisimuogope hana nguvu yoyote. Kama yeye anatibinafsisha kwa wezi kia aina kwanini nasi tisibinafsishe ulaji wake ili wote titoke droo?”
          Mijjinga aliyekuwa amekaa kimya muda mrefu huku akibofya ki-Surface chake anaamua kutia guu, “Mgosi mawazo yako ni endelevu, adhimu na ya kimapinduzi. Lazima tufikie mahali tuamue. Kama mbaya mbaya! Tena ni heri tuibinafsishe mapema kabla Chama cha Mizengwe (CcM) hakijaibinafsisha kwa fisadi mwingine. Hamkusikia kuwa hata mzee Mizengwe Pinder naye eti anautaka huku akipigiwa upatu na Denjaman Makapi?”
          Msomi anaamua kurejea tena, “Mkuu Mijjinga usinivunje mbavu. Jitu lililoshindwa kulhali eti nalo linataka urahisi ili lile kwa urahisi. Nadhani hili balaa lililopo linatosha. Sishangai. Maana kwa kaya yetu ilivyogeuzwa cha mwendawazimu, Pinder anaweza kununua magazeti ya umbea na makanjanja wakampamba akapambika na akasimikwa ili atuumize. Kama makapi kama Makidamakida, Miguiro yanatajwa itakuwaje mzee Pinder asitajwe? Kama wasaka tonge kama Jan Makambale, Eddie Ewassa, Sam Sixx na mafisadi wengine wanautaka kwanini mzee wa kuota ndoto asiamke na kusema kuwa ameoteshwa kuwa agombee urahisi? Hii kaya imegeuka ya vichaa, matapeli, wezi na majambazi yanayoiba mchana kweupe.”
          Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa amefura nusu kupasuka anakwea mic, “Semeni msemayo BMK  na Ikulu hazibinafsishwi. Vinafanya kazi zake kisheria na vinalindwa na sheria. Halo halo!”
          Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akitafuta upenyo anaamua kuchomekea. Anasema, “Da Sofi acha nikuchomekee. Wewe unababaishwa na sheria inayoweza kutungwa na kufutwa. Tukiacha ushabiki, BMK inalindwa na sheria gani zaidi ya kanuni za kifisadi na ujambazi wa mchana?”
          Kanji kuona watu wanazidi kuzoea ujiko anakamua mic, “Mimi ona kama iko mtu hapana rizika nenda kashitaki kwa mahakama tatoa haki.”
          “Kanji waishi dunia gani? Yaani mtu nzima waingizwa nkenge na wasaka sifa kama akina Alifu na Kubenua wanokwenda mahakamani kushitaki BMK ili kutafuta ujiko wakati walishaambwa sharia ya kulisimamisha hakuna! Sie hatushitaki bali kutafuta mwekezaji ambaye ni Kijiwe hichi walllahi. Kama watu wazima wafanya ujuha kwanini nasi tuwe majuha badili ya kutumia akili?” anang’aka Mpemba.
          Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shangingi la Sam Sixx. Acha tulitoe baruti tukitaka kumkamata na kumtia adabu! Bahati yake aliokolewa na ndata kabla hatujamfanyia kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 3, 2014.

No comments: