The Chant of Savant

Wednesday 25 June 2014

UDA: Ni Maziku na si Mwanakijiji inayepotosha umma

Tunaandika makala hii kujaribu kutoa ufafanuzi, kama si majibu, kwa makala ya ndugu George Maziku ya tarehe 18 Juni 2014 kwenye gazeti la Tanzania Daima la Jumatano akijibu makala ya Mwanakijiji ya tarehe 11 Juni 2004 katika gazeti lile lile. Kutokana na ufinyu wa nafasi, tutadurusu na kuonyesha udhaifu wa makala ya Maziku japo kwa ufupi ili kutoa nafasi na kwa wengine watakaotaka kufanya hivyo wafanye hivyo.
Japo Maziku anadai alifanya utafiti bila kuunyesha, alitoa tuhuma za jumla na reja reja bila hata chembe ya ushahidi unaoingia kichwani dhidi ya, kwanza, watanzania wote, pili, wabunge wa Dar Es Salaam wote na tatu, Mwanakijiji. Kutokana na makala husika kuwa nyepesi na yenye kujaa mapofu, dhambi ambayo mwandishi aliwatuhumu wenzake, akairudia, hatutajibu neno kwa neno (verbatim) zaidi ya kuonyesha baadhi ya mapungufu na si yote. Maana, kama ni kuijibu makala nzima ipasavyo, unaweza kuandika hata kitabu. Tutatumia lugha nyepesi ili wahusika wajue wanachofanya siyo na hawajafanikiwa.
Kwanza, hoja za Mwanakijiji bado zina mashiko kwa watu wenye utashi na utambuzi wa mambo katika uhalisia wake. UDA imeuzwa kifisadi na haina tija kwa wakazi wa Dar. Hili liko wazi tu. Ushahidi?  Mosi, rejea maneno ya mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) Zitto Kabwe, aliyekaririwa akisema, “Kama kuna watu ambao wameuziwa chochote wameingia choo cha kike (maana ni batili maana hawana kibali cha CHC).” Hili halihitaji ufafanuzi. Liko wazi.
Pili, rejea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa fedha za serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni inasomeka, “Bodi ya wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hisa bila kupata kibali cha Serikali na hata CHC.” Tatu, rejea tamko la Mei14, 2014 la waziri mdogo wa Fedha na Uchumi, Adam Malima, aliyeliambia bunge kuwa UDA haijauzwa. Je hawa wote wanatetea mkate wao na maslahi binafsi? Kama ni hivyo, tungemwomba Maziku na yeyote m wenye ushahidi atoe.
Pia Maziku, bila mafanikio amejitahidi kutetea kampuni ya Simon Group na wazawa.Bila hata tahadhari, Maziku alianza kwa tuhuma dhidi ya watanzania akisema, “Watanzania ni watu ajabu sana. Mara nyingi wanaweza kutumia nguvu nyingi na muda mwingi kupigania jambo ambalo hata hawana faida nalo.” Hii si kweli. Watanzania sawa na watu wengine popote pale duniani ni watu wa kawaida wenye akili na si mapenzi kibubusa wala kutetea upuuzi hata kama wapo baadhi wanaotetea upuuzi. Madai kama haya ni mazito. Ni vigumu kuyathibitisha kisomi. Laiti Maziku angeonyesha “uajabu” wa watanzania tena wote, angeeleweka na hata kuheshimika ukiachia mbali hoja yake kuleta tija na kuwa na mashiko. Pamoja na Maziku kutoa tuhuma za ajabu bado hawezi kuitwa mtu wa ajabu zaidi ya mtu asiyejua anachotetea tokana na kushindwa kuleta ushahidi wenye ithibati na ushawishi kiakili. Sana sana alichobainisha Maziku kwenye mwanzo wa makala yake ni kuonyesha hisia za ukabila na unasaba pale na hata kutumiwa anaposema, “wanufaika ni watu wengine ambao hata hawana nasaba nao.” Kwa mantiki ya haraka ni kwamba Maziku anajifichua kuwa ana nasaba na Simon Group. Hii haikubaliki. Huwezi kumtetea mtu kwa sababu ni Msukuma au Mtumbuka mwenzako. Huu ni unepi na ufisadi wa kiakili.
Ukiachia mbali na watanzania wote aliowazushia uajabu na hata ulimbukeni wa kutetea wasicho nacho faida, Maziku amewatuhumu wabunge wa Dar akisema kuwa wanatetea maslahi binafsi na si taifa bila kutoa ushahidi pale alipoandika, “Bali wanafanya (baadhi ya watu na wabunge wa Dar) hivyo kwa kusukumwa na maslahi binafsi, wanatetea mkate wao.” Dai hili ni tata. Huwezi kusema mtu anatetea maslahi binafsi au mkate wake bila kutaja hayo maslahi ili wasomaji wayajue na kupitisha hukumu yao kama watu wenye akili na maarifa.
Kimsingi, hoja anayotaka kujenga Maziku ni kwamba wanaopinga ufisadi katika uuzaji wa UDA wanatetea maslahi binafsi na ni watumwa wanaotumiwa na wenye kutaka kunyakua UDA. Je yeye anatetea maslahi ya nani kama si binafsi baada ya kutumiwa?  Huu unaweza kutumika kama ushahidi kimazingira (circumstantial evidence) wa kujifunga (incupatory evidence) dhidi ya Maziku kuwa anatumiwa na Simon Group.
Katika kutaka ku-justify hoja yake nyepesi, Maziku anaweka mbele uzawa bila kujali haki na kanuni. Je kila mzawa ni wa kuungwa mkono hata kama anafanya madudu?  Kwanini Maziku hahoji madai kuwa Idd Simba, meya wa Dar Es Salaam, Didace Massaburi na Victor Milanzi, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa UDA waligawa shirika la umma kwa faida binafsi?Sijui kama kweli Maziku anajua jinsi UDA ilivyouzwa kifisadi chini ya ushawishi wa Simba ambaye anadaiwa kuhongwa shilingi  milioni 400? Je Maziku huwa hasomi magazeti au anafanya makusudi? Mbona wizi na ufisadi uliozunguka uuzaji wa UDA unajulikana hata kwa wasioishi Tanzania?
Tunachoweza kusema ni kwamba Simon Group inaendelea kupigiwa kifua na baadhi ya vigogo wa CCM kama alivyodai mbunge wa Ubungo John Mnyika bila wahusika kukanusha au kutoa utetezi. Mnyika alikaririwa akiliambia bunge ifuatavyo, “Ni kwa nini watuhumiwa wameachiwa? Mheshimiwa Spika, haya yasipojibiwa tutaamini kuwa jambo hili linawahusu vigogo wa CCM na mnawalinda katika ufisadi huu.” Mnyika alikuwa akishangaa ni kwanini serikali hasa DPP haikuchukua hatua ilhali ripoti ya CAG ilibaini ufisadi. Si serikali, CCM wala DPP aliyejitokeza kujibu hoja ya Mnyika. Hii maana yake ni kwamba wahusika wanakiri ukweli wa madai husika.

Kwa vile nafasi haitoshi, tunaishia hapa tukimshauri Maziku ajitahidi kufanya lau utafiti kidogo anapojibu hoja nzito kama ya Mwanakijiji. UDA imeuzwa kifisadi atake asitake. Anayepinga hili aje na ushahidi wenye mashiko badala ya jazba na kuzulia watu katika kutetea uoza. Huwezi ukatetea uoza eti kwa vile anayeufanya ni mzawa. Mwandishi makini ni yule anayetetea haki ya wasio na haki na kuwa sauti ya wasio na sauti (Voice of the voiceless). Kinyume na hili huku nako ni kutumika kwa aina fulani ambako hakufai kuwa sifa ya mwandishi au mchambuzi. Mwenyekiti Mao Tse-Tung wa China alizoea kusema, No investigation (research), no right to talk. Kama huna ushahidi tafitishi huna haki ya kusema.
Chanzo: Dira Juni 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Kama iwapo Simon Group siyo Kampuni ya ubabaishaji. Je kwa nini wasingeanzisha kampuni yao mabasi Dar from the start.

Uzoefu ukiona viongozi wa C.C.M wanatetea sana jambo basi fahamu fika kuwa kuna uozo mkubwa umefanyika katika kuiba mali ya umma.

Huyu Maziku hana tofauti na hao walevi wengine wanaotetea huu wizi na ujambazi unaofanyika kukiwa bado mchana kweupe.

Maziku kumbuka Ulimwengu unabadilika na iwapo njaa ndiyo inayokusababisha kutetea uozo basi elewa hilo suluhisho lako ni kwa ajilia muda mfudpi. Mwanakijiji anazungumzia suluhisho la muda mfupi na mrefu pia.

Watu wote wenye uelewa tosha wanafikiri leo, kesho na keshokutwa siyo kama wewe unafikiri maisha ni leo...husiwe kama wanyama porini, hawalimi lakini wanaishi.

Binadamu tumeumbwa kutatau matatizo na siyo kuleta matatatizo hapa duniani.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umesema vyema. Asante sana naamini ujumbe wako utawafikia walengwa ili waache kufikiri kwa usawa wa pua.