The Chant of Savant

Wednesday 18 June 2014

Tunataka uongozi kwa Kinana si uongo

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana, ana sura nyingi, tena tata. Ni mfanyabiashara, tena mwenye kutia shaka, ambaye amewahi kutuhumiwa kusafirisha pembe za ndovu. Ni mwanasiasa anayechanganya biashara na siasa kiasi cha kutia shaka zaidi. Pia Kinana ni mtu anayeweza kusema lolote na akatenda tofauti.
Kinana ana sura nyingine. Anajulikana kwa kuwa mwepesi wa kushambulia wenzake na kunywea pale wanapojibu mapigo kama ilivyotokea mwaka jana alipowaita wenzake mizigo, akaishia kuonekana mzigo zaidi pale bosi wake, Rais Jakaya Kikwete, alipompuuzia na kuwapandisha vyeo na kumwacha akizodoka na kuadhirika. Wengi walidhani angejiuzulu. Lakini wapi?
Pia, unaweza kusema ni mtu mwenye kudharau, kuwatisha hata kuwageuka wenzake. Hata hivyo, ana uchungu gani na taifa ambalo hajawahi kujinasibisha nalo ukiachia mbali kulitumia kupiga madili kama walivyo wengi wa namna yake? Hivi karibuni alikaririwa akisema kitu ambacho kimsingi si kweli bali uongo wa wazi aliposema; “Nataka niwaambie wananchi, hatufanyi mambo kwa kutafuta kura kwenu, hivyo anayetaka kurudisha kadi arudishe wala hatutishiki, mkitaka kurudisha 1,000 hata 2,000 rudisheni.”
Ya kweli haya shehe au ni kudanganya mchana kweupe kama si kugundua kuwa kweli watu wameishachoka siasa za uongo? Hata hivyo, ana shida gani na kura zao wakati wanaweza kuchakachua?
Kinana aliongeza; “Sisi tunafanya mambo kwa mujibu wa kuwahudumia wananchi, mtu asikae akafikiri akirudisha kadi sisi tutakuja kuhangaika.” Hivi Kinana anaishi wapi? Anapata wapi mshipa wa kusema eti CCM inahudumia watu wakati inasifika kwa kuwahujumu na kuwaibia?
Anaongelea CCM ipi au ile Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambayo ilikufa hata kabla yake? CCM ya sasa, kama alivyowahi kukiri Kinana, imejaa mizigo iliyowalemea wananchi na majini yanayowanyonya wananchi.  Tumkumbushe.
Chini ya CCM hii inayodanganya inawahudumia wananchi, mwaka 2005 iliiba mabilioni ya shilingi toka Benki Kuu toka fuko la madeni ya nje almaarufu EPA na kuyatumia kwenye uchaguzi kuhujumu wanaCCM walioonekana tishio kwa bosi wake jambo ambalo hata Kikwete mwenyewe hajawahi kukanusha.
Ikumbukwe. Wakati wa wizi huu Kinana alikuwa meneja kampeni wa mtuhumiwa. Hivyo, kwa njia moja au nyingine Kinana alihusika. Je, Kinana alitumia neno kuhudumia akimaanisha, kujihudumia au kuhujumu? Maana, ndicho kitu sahihi ambacho CCM inafanya.
Mbona Kinana haongelei mambo muhimu na makubwa kwa wananchi kama kugunduliwa upotevu wa sh bilioni 200 toka huko huko zilikotoka, fedha za EPA kipindi hiki kwenye fuko liitwalo Escrow ambalo limegeuka Screw?
Laiti Kinana angejua kuwa wananchi wanajua uchafu wao wote sema wanaogopa kupatiliza, angejua kuwa kama wangekuwa na demokrasia ya kweli kumuuliza maswali, wangemvua nguo kiasi cha kuacha kujisemea kama mwenzake Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye anasifika kwa kupayuka na kubwata akiishia kuzodolewa na kupuuzwa na bosi wake, asingeendelea kujidanganya huku akiwadanganya wananchi.
Kuonyesha Kinana alivyo na sura na hata ndimi nyingi, alikaririwa huko Hanang’ akisema; “Tunataka mashamba ya ngano yaendelee kulimwa ngano na siyo wawekezaji kuyakodisha kwa wananchi ambao wanalima mahindi.”
Kwanini hakueleza hayo mashamba yalivyokuwa ya serikali halafu yakabinafsishwa kijinga kiasi cha kugeuka kuwa balaa kwa wananchi? Kwanini hakutaka kujua kuwa sera za uwekezaji za CCM zimewaumiza wananchi kiasi cha wanaoitwa wawekezaji kuishia kuwa wachukuaji, tena mchana kweupe?
Kwanini Kinana hakujua kuwa wananchi wanajua madudu ambayo ni sawa na majini kama vile IPTL ambayo imekuwa ikiwalangua umeme huku ikitumika kuliibia taifa kiasi cha kufikia kutaka kuua Shirika la Umeme la Tanesco?
Kwanini Kinana hakutaka kujua kuwa wananchi wanajua uwekezaji wa ki-CCM ulivyogeuka wizi wa mchana kama ilivyotokea kwenye Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA) ambapo serikali ilivuliwa nguo hivi karibuni baada ya kugundulika kuwa lilihujumiwa kutokana na mtoto wa kigogo wa CCM kuwa nyuma ya ujambazi huu?
Kwanini Kinana hataki kujua kuwa wananchi wanajua wizi wa kampuni ya kihindi ya Rites iliyoletwa na wezi wakubwa madarakani na kuondoka na mabilioni bila kufanya kazi yoyote? Huyu ndiye anayeutaka urais wakati anawadharau wananchi kuwaona kama mabwege wasio na akili au kumbukumbu?
Kwanini Kinana anashindwa vitu vidogo visivyohitaji elimu kubwa kama kujua kuwa CCM iliiba ardhi ya wananchi kuanzia Kapunga Mbeya hadi Hanang’ na kuwauzia wawekezaji wanaotumiwa kuhujumu wananchi?
Muulize, huu uwekezaji kwenye kilimo umelisaidia nini taifa iwapo, chini ya CCM, kila mwaka linakabiliwa na baa la njaa ambalo limegeuka ugonjwa sugu kwa taifa? Fedha inaibwa huku ardhi ikihodhiwa na kutumiwa vibaya kiasi cha kuwafanya Watanzania wawe masikini kwa kuzalisha kidogo na kukiuza kutokana na kulanguliwa pembejeo na kuibiwa fedha yao ya umma kunakofanywa na makada wa CCM.
Kuonyesha Kinana alivyo na matatizo ya kumbukumbu na uelewa au tuseme kuwatapeli wananchi, hivi karibuni akiwa mjini Singida alikaririwa akisema; “Haiwezekani mtu anafanya makosa ya kiutendaji halafu anahamishiwa katika idara nyingine kwa kisingizio cha utawala bora, ni lazima hatua zichukuliwe kulingana na makosa wanayoyafanya.”
Kinana anamdanganya nani kudai haiwezekani mtu akafanya makosa akahamishiwa sehemu nyingine wakati yeye alituhumiwa kusafirisha nyara za taifa akahamishiwa hapo alipo?
Je, anayewahamisha hao wahalifu ni nani kama si serikali yake ambayo imeitawala Tanzania tangu uhuru? Japo anachosema kina ukweli kuwa kuna watu wanahamishwa wanapovurunda kama ilivyotokea kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ladislaus Komba aliyeteuliwa na Mwenyekiti wa CCM kuwa Balozi nchini Uganda baada ya kutuhumiwa kuhusika na kusafirisha wanyama hai 130 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akishirikiana na Kamran Ahmed ambaye CCM imemsaidia kukimbia toka nchini kama ilivyofanya kwa Chavda.
Anadhani wananchi hawajui? Kama Kinana angechukia tabia chafu ya kuhamisha au kulinda watendaji wabovu angekuwa wa kwanza kuachia ngazi ya ukatibu mkuu wa CCM.
Tumalizie kwa kumtaka Kinana aache kuwadanganya Watanzania na kuwageuza mataahira. Hakuna chama kinachoweza kushamiri bila wanachama. Hivyo, asiwatishe wanachama.
Nao wanapaswa kumuadhibu kwa kurejesha kadi zao ili auone ukweli mchungu japo CCM kweli haiwataki wanachama kwa vile ina mbinu ya uchakachuaji kubakia madarakani kutokana na Watanzania kutotumia nguvu ya umma kuiondosha madarakani japo siku zake zinazidi kuhesabika. Nitawaletea sehemu nyingine ya makala kuhusu Kinana dhidi ya chama chake.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 16, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Siku hizi tumebadili siasa kuwa porojo tena kila wanaporojo wa CCM ndiyo inawanachama wengi sana, na kamwe porojo haziwezi kuleta teja.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umesema vyema ila tunapaswa kupambana na usanii huu mfu na uchwara kabla haujatuangamiza kama taifa.