The Chant of Savant

Wednesday 11 June 2014

Mgimwa, eti wewe si mzigo?


MBUNGE wa Kalenga, Godfrey Mgimwa (CCM), ameanza ngwe yake kwa vibweka, hata mipasho, tena inayowalenga wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliompigia chapuo.
Hivi karibuni alikaririwa akisema, “sitaki kuitwa mbunge mzigo au mtu wa kusinzia bungeni na kupigwa picha kwa kuwa wapiga kura wangu Jimbo la Kalenga bado wana matatizo mengi na mimi ndiyo tegemeo lao, ndiyo maana walinichagua kwa kura nyingi sana na nitahakikisha nawabana mawaziri bungeni.”
Bila shaka maneno haya ya Mgimwa yatakuwa yamewaumiza wabunge kama John Komba na Stephen Wassira, waliowahi kupigwa picha wakiuchapa usingizi bungeni.
Bila kujali kama walikuwa wameutwika au kumeza dawa, Mgimwa anatupa aina nyingine ya mizigo iliyojaa bungeni. Tutamsaidia kubainisha aina nyingine za mizigo bungeni.
Japo anayosema Mgimwa yana ukweli, ila amesahau kuwa mizigo siyo ile inayolala tu. Bungeni kuna mizigo mingi. Kuna ile iliyorithi nafasi za wazazi wao. Kuna ile iliyoshindwa, lakini ikatangazwa imeshinda baada ya uchakachuaji.
Kuna ile inayotoa ahadi za uongo. Kuna aina nyingine ya mizigo yaani ile inayohongwa kupitisha mambo ya ajabu ajabu. Pia kuna mizigo inayowekwa sawa kama kamati ya chama na kuridhia upuuzi.
Mizigo bungeni ni mingi sawa na maofisini. Kuna ile iliyoghushi vyeti vya kitaaluma na ile ambayo imo bungeni kwa kupendelewa ukiondoa ulemavu hasa kutokanako na ushikaji kwa wenye madaraka ya kuteua. Kuna mizigo mingine.
Hii si mingine bali ile inayokwenda bungeni kuchangamkia mshiko bila kuchangia lolote. Pia ipo mizigo ambayo imo bungeni kulinda maslahi ima ya biashara zao au baba zao kama si jamii yao.
Aina nyingine ya mizigo iliyopo bungeni ni ile inayosifika kwa mipasho na matusi kama ule uliowatukana wenzake “f*ck you” au ule ulioita wenzake Boko Haram ukiachia ile inayotishia Watanzania kuwa wasiporidhia kile inachokitaka majeshi yatachukua dola au mizigo kwenda mwituni.  Aina nyingine ya mizigo bungeni ni ile ambayo imeishiwa kila hali na haina cha kuchangia zaidi ya kuwa bungeni kama mapambo.
Hakika mizigo mingine bungeni ni ile inayokwenda kwenye serikali za mitaa kudai kitu kidogo ili kupitisha hesabu zake. Hii iko mingi na inajulikana.
Mizigo mingine ni ile ambayo huongea kwa kupayuka ikikariri maneno ya wakubwa zao kama ile inayomshambulia Jaji Joseph Warioba badala ya hoja alizotoa yeye na tume yake.
Hii ni mizigo inayonuka kweli kweli. Ikipokoma utahisi kichefuchefu, hasa inapotokea mizigo inataka kumuua mjumbe badala ya yule aliyemtuma.
Mizigo mingine ni ile ambayo imo bungeni si kwa nguvu ya kura bali kununua kura na kutoa hongo takrima na upuuzi mwingine. Hii ni mizigo inayopaswa kuchomwa moto.
Turejee kwa Mgimwa aliyekaririwa akisema, “nitabanana na Waziri wa Nishati na Madini katika bajeti yake ili kuhakikisha vijiji hivyo vinapata huduma ya umeme kabla ya uchaguzi mkuu ujao ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena mwaka kesho.” Yale yale! Mgimwa anaongea kana kwamba serikali yake inajitegemea kibajeti. Huyu ndiye anasema ana Masters sijui ya uchumi sijui nini? Mgimwa hukusoma research method kabla ya kutetea andiko lako la kupewa hiyo masters au ulifanya ile ya kufanya mitihani kwa kukwepa thesis?
Uchumi gani kuongea bila kufanya utafiti? Taarifa zilitolewa siku moja kabla ya Mgimwa kumwaga upupu wake, ni kwamba wizara nyingi zinapokea pesa pungufu zaidi ya ile iliyoidhinishwa. Bahati mbaya Mgimwa hasomi magazeti wala kutafuta habari vinginevyo alipaswa kulijua hili.
Inashangaza Mgimwa hajui vitu rahisi kama hivi, hasa ikizingatiwa kuwa taarifa kuwa serikali iko taabani kifedha ilitolewa ndani ya Bunge hilo hilo analohudhuria vikao vyake.
Mbunge Idd Azan wa chama tawala alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na umahututi wa serikali kifedha: “Angalia bajeti ya mwaka jana, zipo wizara zimeishia kupata asilimia 25 mpaka 30 na mwaka ndiyo umeisha na mwaka huu tunapitisha bajeti harakaharaka ili mradi tu tupitishe, hili ni tatizo.”
Kwa kuangalia hali hii ya serikali “kucharara” huku ikitegemea kutembeza kapu, bila shaka wale wote wanaohusiana na serikali ya namna hii inayoruhusu nchi kupoteza dola bilioni 1.8 kwa mwaka huku ikiombaomba na kupata pungufu ya hizi nao ni mizigo.
Tena hawa ni mizigo ya uoza au tuseme mabomu hasa ukiangalia wanayofanya. Mizigo hii ni ile ile iliyofuja mamilioni hata mabilioni ya shilingi kwenye kinachoitwa sherehe za Muungano zilizolenga kutoa mwanya kwa jeshi kuwatisha Watanzania kama alivyodai Amiri Jeshi Mkuu Jakaya Kikwete.
Aina nyingine ya mizigo ni ile unayoweza kuita “Ndiyo mzee.” Hii mizigo si mingine bali ile inayowasaliti wale walioichagua na kutoa kodi ya kuwezesha ilipwe mishahara na marupurupu yake kwa kuunga mkono kila upuuzi wa chama.
Hii haina tofauti na mizigo ya kinyesi. Kwani licha ya kunuka, husababisha hasara kwa taifa. Haiwezekani miaka zaidi ya hamsini ya kuwa huru tuendelee kutegemea wafadhili tena kwa bajeti yetu huku CAG akiripoti wizi wa fedha nyingi kuliko hii tunayoomba tena kwa kujidhalilisha sisi binafsi na taifa.
Ni mwanamume gani anaweza kuwa huru huku mkewe na watoto wakilishwa na kuvishwa na wafadhili? Je, siku wakiamua kudai mke na watoto ni wao ataweza kuwazuia? Ajitokeze mbunge toka kwa wale wanaotawala akane umzigo huu nimuone.
Tumalizie tulikoanzia kwa Mgimwa. Kama atakwepa kuwa mzigo kwenye eneo moja atakuwa kwenye eneo jingine. Je, hadi hapo Mgimwa bado si mzigo tulioachiwa na baba yake na mfumo wa kulindana, kujuana, kufadhiliana, kubebana na upuuzi mwingine ambao sasa umegeuka wa kurithishana kila kitu?
Je, tunayo mizigo kiasi gani itokanayo na koo za wakubwa bungeni na hata kwenye Baraza la Mawaziri ukiachia idara na ofisi nyingine za umma? Aina za mizigo bungeni ni nyingi tu.
Nafasi haitoshi. Eti Godfrey Mgimwa wewe si mzigo sawa na mingine? Teh teh teh! Kwekwekwekwekwe! Kituko!
Chanzo: Tanzania Daima Juni 11, 2014.

No comments: