The Chant of Savant

Wednesday 18 June 2014

Kisena, Mitandao Ridhiwani na UDA

Kwanza, nikiri. Mimi ni shabiki wa mpendwa shujaa, mteule, msifika Ridhiwani Kikwete kufa mtu. Lazima kutangaza maslahi yangu kwenye mjadala huu. Namshabikia Ridhiwani ajabu. Kuna kipindi nilitaka kubadili jina langu niitwe Ridhiwani. Kwa kuogopa ngoa ya wavyele nimeamua kumpa jina hili mtoto wa kiume nitakayempata.
Pia namshabikia Robert Kisena kwa ujeuri wake hasa kwenye mambo ya connection na mshiko. Hivyo, kuna kipindi nilitaka nijiite Ridhiwani Kisena lakini sababu ile ile ikanizuia. Hivyo, kuonyesha ushabiki wangu, nikipata mtoto wa kiume namwita Ridhiwani Kisena na kama ni wa kike nitamwita Ridhwana Kisenia. Hayo tuyaache.
Leo naandika kuwapasha wanaowachafua wateule wangu. Huwa sipendi umbea. Huwa roho inaniuma ninaposoma habari za kuwazushia na kuwachafua wateule wangu hawa.
Juzi katika kusoma kwenye mitandao nilikuta tuhuma kibao dhidi ya wawili hawa.  Mtandao mmoja ulizusha eti Ridhiwani ndiye anayemtumia Kisena kuendesha kampuni yake ya marehemu Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA) ambalo sasa linaitwa Simon Group utadhani mtoto si ridhiki.  Chochezi jingine lilichangia likisema, “Inashangaza Ridhiwani bingwa wa kujibu kwenye mitandao amekaa kimya. Je tuhuma hizi ni mbinu za wabaya wake kumchafua au ni ukweli mtupu? Vyovyote iwavyo, kuna chembe za ukweli kwenye madai haya hata kama si kwa kiwango kikubwa. Sipendi kuamini kuwa huu ni ukweli wala uzushi. Ndiyo maana nimejitolea kuwasaidia wahusika waweke mambo sawa na kusafisha majina yao huku wakifanya hivyo kwa hoja zinazoingia akilini.”
                Baada ya kusoma huo upuuzi hapo juu nilikaribia kupasuka kwa hasira. Chini yake jingine liliandika, “Huwa siamini kwenye conspiracy theory ambayo sina tafsiri yake kwa Kiswahili.  Hivyo, naanidika waraka huu kutaka kujua ukweli zaidi. Naandika kwa sababu kuu mbili. Mosi, kutetea mali ya umma ambao nami ni mmojawapo. Pili, kumpa nafasi Ridhiwani kujitetea angalau hasa ikizingatiwa kuwa kuna maisha baada ya baba yake kuachia ngazi.” Hili nusu lininyotoe roho kwa ngoa.
Jingine liliandika, “Kwa wanaofahamu historia ya Robert Kisena, hawana shaka yoyote aliibuliwa na vigogo wa CCM hasa waziri Juma Kapuyanga kabla ya kudakwa na Ridhiwani ambaye anajulikana walivyo marafiki.  Ushahidi wa wazi ni uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo Ridhiwani alimpigia kampeni Kisena lakini akaangushwa na John Shibuda.  Katika kampeni hizi alipigia pia Steven Masele ambaye pamoja na udhaifu wake sasa ni waziri. Mwingine aliyetumika kama mbuzi wa shughuli ni Salum Mbuzi.” Liliendelea, “Hata kunyimwa nafasi kwa Shibuda hadi akaihama CCM na kujinga na CHADEMA na kuiadhibu kwa kuishinda kuna mkono wa Ridhiwani. Laiti Shibuda angeamua kulisema la moyoni kijana huyu angeumbuka si kawaida.”
Wakati roho ikiendelea kuniuma jingine liliongezea, “Wapo wanaosema kuwa pamoja na Ridhiwani kujionyesha kama rafiki wa Kisena, ukweli ni kwamba wote wawili ni wajanja wanaotumiana. Kisena anajua kuwa Ridhiwani ni mtoto wa rais tena rais mwenyewe asiyejali wala kuwa mkali kwa familia yake.  Hivyo, ni lulu kutokana na kuwa mtoto wa mwenye nchi kwa sasa. Hivyo, kumnasa Ridhiwani ni kuunasa utajiri tena wa haraka. Anayebishia hili ambane Kisena aeleze alivyopata utajiri wake kama hakuna mikono ya watu tena wazito kabla ya Ridhiwani.” Baada ya kusoma hii nilikwenda kujipumzisha.
Niliporudi nilikuta jingine limeandika, “Kwa upande wake Ridhiwani anajua kuwa Kisena ni msanii mzuri anayeweza kufanya madili kirahisi na kwa ufanisi. Pia Kisena, tokana na historia yake ya kubebwa si rahisi kumuasi bosi wake kwenye biashara ya nyuma ya pazia. Hivyo, ni kiraka mzuri na mtiifu hasa kwa kuzingatia jinsi anavyotoka kwenye familia maskini na jinsi kinachoitwa utajiri wake kisivyo kuwa chake bali wale wanaomtumia.” Nilitamani nilikamate hili na kulinyongelea mbali.
 Jingine liliandika, “Kutokana na ukaribu huu wa Kikwete na Kisena, baadhi ya wachambuzi wanaunganisha mistari na kupata kitu kizima. Wengi wanahoji. Ni kwanini serikali imekuwa ikijikanganya kuhusiana na umilki wa UDA kama hakuna wakubwa nyuma ya pazia wakivuta Kamba? Swali ambalo liliibuka bungeni hivi karibuni ni kwanini serikali imetoa msamaha wa kodi kwa Kisena kuingiza mabasi 300 wakati ikimkana kuwa si mmiliki wa UDA? Je kama hakuna wakubwa wezi nyuma ya Kisena inakuwaje apewe msamaha wa kodi kwenye biashara binafsi hasa ikizingatiwa kuwa biashara anayofanya si ya lazima kama vile madawa na chakula wakati wa dharura? Je Kisena kama Kisena bila kuwa na Ridhiwani nyuma ya pazia ana ubavu wa kupata msamaha mkubwa wa kodi bila kuwapo wakubwa wanaofaidika? Wenye kutaka kujua nani yuko nyuma ya pazia shupalieni huu msamaha wa kodi wa Kisena mtagundua kuwa yeye ni mtumiwa kama watumiwa wengine.” Baada ya kusoma hii nilijisikia nikipandisha Usherukamba na kusema f**ck you.
Jingine lilizidi kunipandisha presha kwa kuandika, “Wapo wanaounganisha kufutwa kwa kesi ya Idd Simba na kutochukuliwa hatua Victor Milanzi, mkurugenzi wa UDA aliyemuuzia UDA Kisena ushahidi wa kuwepo Ridhiwani nyuma ya Kisena. Hata hii jeuri anayoonyesha Kisena akijuwa wazi kuwa hajawahi kurejesha fedha ya stimulus aliyoipata kwa mchongo si bure. Kuna Riz nyuma yake.”
Jingine liliongezea, “Kitu kingine kinachoweza kumuumbua Kisena kama mtu anayetumiwa ni historia yake ambayo waandishi wengi wameishaianika tangia akiwa sekondari.”
 Mtandao mwingine uliandika, “Japo serikali haitaki kusema ukweli, UDA ilianza kuhujumiwa pale mkurugenzi wake aliyetimuliwa Milanzi kushirikiana na Simba kuitoa chini ya siasa za kindoto za uzawa mfu ambao uligeuka kuwa ujambazi wa wazi. Hapa ndipo Kisena alipopiga bongo kiasi cha kumnasa Simba jambo ambalo baadaye lilimvutia Ridhiwani.”
Kwa kuwazushia wateule wangu nashauri TCRA ifungie hii mitandao ya kimbea. Wakishindwa sisi wapenzi wao tutadedisha mtu. Wapendwa endeleeni kula kwani hiyo UDA ni mali ya mtu au umma? Hakuna haja ya kukanusha wala nini. Pigeni dili kama kawa mwenye wivu ajinyonge.
Tuache umbea. Mkiambiwa Ridhiwani ni mtoto wa Jakaya Kikwete mtasema ni umbea au uzushi? Heri yasifike ya akina Saif al Islam Gaddafi. Akili kichwani.

Chanzo: Dira Juni 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Nasikia kutapika

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon huna haja ya kujihisi kutapika. Badala yake ondoa hicho kinyaa kinachokufanya ujihisi kutapika. Hamasishaneni tuondoe hiki kinyaa.