The Chant of Savant

Wednesday 11 June 2014

Kijiwe chalaani wizi wa SCREW na UdAR

BAADA ya Kijiwe kugundua kuwa Chama Cha Mafisi na Mafisadi (CCMM) kimezima harakati za kuzuia kuchunguza ujambazi wa SCLOW aka Screw wa madafu bilioni 200, Kijiwe kimekaa kama kamati kulaani ujambazi huu.
Pia Kijiwe kinalaani danadana na sanaa zilizoonyeshwa katika ujambazi wa UdAr ambapo majambazi waliofanya hivyo wanafahamika kuwa ni Juma Kapuyanga, Dida Masaburiz, Idd Lion, Riz Kiqueet, Bob Kisenha na wengine waliojificha nyuma ya pazia. Msishangae kuona Kijiwe kimeingia full masnonda kwenye politiki.
Ni kutokana na kuwepo ombwe hasa tangu Njaa Kaya aanze kufuja kaya kwa uongo badala ya uongozi, sanaa badala ya sera na ufisi na ufisadi badala ya usafi na uzalendo.
Mgosi Machungi siku hizi amegeuka mwanasiasa. Anasoma magazeti kama hana akili nzuri. Anaingia na kulianzisha. “Wagosi mmesoma hii habai ya wizi wa mabiioni kupitia kampuni la kijambazi la IpIITL na hii danadana kuhusiana na UdAR mjengoni? Watu wazima hovyo. Wanafanya mambo kama hawana akii! Kia siku sanaa sanaa wanadhani hatina akii? Shame on them all!”
“Unaongelea hii EPAA mpya kuelekea kwenye uchakachuaji? Nilijua. Wataiba. Wamezoea. Usishangae kutokea ujambazi mwingine. Hata ujambazi huu wa UdAR si bure.
“Hamkuona waishiwa walivyovuana nguo juzi mjengoni huku wale wa genge la uchakachuaji wakichekelea bila kuchukua hatua?” Anadakia Msomi huku akituma SMS kwenye mtandao wake wa kiganjani.
“Hakuna waliponikuna kama kuanza kukamata uchawi hata mabalozi. Hivi huyu kihiyo Maselee aliyepata ulaji tokana na kujuana na mwana wa mteule Riz anaongeaje wakati madarasa hayapandi? Mnaona alivyoharibu hadi mabosi wake kumkana na kumwangukia mama wa Kikameruni asiwanyime njuluku na viza wanapokwenda kuzurura na kukagua akaunti zao kule?” Anachomekea Mijjinga.
“Hawajamuangukia mtu. Hayo ni mambo ya kidiplomasia.” Anachomekea Bi. Sofi Lion aka Kanungaembe.
Mbwa Mwitu anadakia. “Wamemwangukia ili wamfanyeje? Waangalie asiwakameruni. Maana hawa jamaa kwa kupenda kamchezo haka hakuna mfano.”
Mchunguliaji anajibu. “Wakameruniwe mara ngapi iwapo bajeti zinategemea wafadhili kila mwaka? Bila shaka walishawekewa masharti ambayo wengine hatuyajui.”
Kanji hajivungi. “Kameruni nini? Hapana jua hii Kameruni bwana.”
Muishiwa Bwege naye analonga. “Kwani kukameruniwa vibaya? Wakitaka kuliwa acha waliwe maana ni mali yao au vipi?”
Msomi anagundua kuwa wakianza mambo ya kukameruniana wataharibu mada. Anakula mic. “Hawa jamaa kweli wameishiwa. Kila mwaka wanarudia madudu yale yale. Maana yake ni kwamba ni wavivu wa kufikiri kiasi cha kukalia wimbo ule ule wa jogoo. Jamaa ameingia kwa kutumia EPAA na sasa ataka kuondoka na EPAA ya kumwezesha kujilipa na kutafuta kibaraka wake amrithi na kumlinda kama alivofanya kwa Tunituni Ben Makapu aloasisi na kutekeleza EPAA. Nasikia amuandaa Abduli Al Somali Kinamna.”
Mpemba anakula mic. “Yakhe hujakosea. Hawa weshaishiwa siku nyingi. Wemelewa ulaji kiasi cha kufanya mambo kama hayawani. Mie siku zote nalaumu wachovu waniojifanya hayawahusu wakati waliwa kila uchao. Hivi kweli huu ujambazi wa IpIITL Srew na UdAR wahitaji elimishwa ndiyo waandamane au nao wana uvivu wa kuamua? Utaona hata hili zengwe la Mizengwe Pinder kupinga kuundwa kamati ya kuchunguza litapita bila kupingwa ati.”
“Mgosi tiheshimiane. Unawezaje kusema kuwa tinaliwa wakati tikiwa tinaona na kusikia kama si uchokozi? Hemu tiombe msamaha haaka kabla sijapiga mtu zongo.” Mgosi Machungi analalamika huku akimkazia macho Mpemba.
“Yakhe simaanishi wote japo ni wote kwani hata wao waliwa japo watula sie. Huoni wanivolindana? Wasingekuwa wote waliwa wangewachukulia hatua akina Saada Mkuyati, Freddie Wereema, A liar Kim Maswii, Dida Masaburiz Makalio, Ben Ndururu, Sossie Mwongo, Juma Kapuyanga, Idd Lion, Vikta Milaanzi na majambazi wengine waniojulikana kufanya huu ujambazi wa nchana. Nani ankamate nani wakati wote wevi?” Anajitetea Mpemba kiasi cha kukivunja mbavu Kijiwe.
Mipawa aliyekuwa ndiyo anamkabidhi mzee Maneno gazeti anakwamua mic. “Hakuna kituko kilichoniacha hoi kama wapingaji kupendekeza eti buge liunde kamati ya kuchunguza EPAA hii iitwayo Screw kwa Kisukuma. Nani aunde kamati wakati yaliyomkuta mwenzao Eddie Ewassa mwana wa Luwasha hayajasahaulika? Siku hizi amenywea kiasi cha mbio zake za kutaka ukuu kufifia huku al Shabuub Kinamna eti naye akiutaka. Si aende akatawale kwao Mogadisho.”
“Usinitajie huyu Kinamna. Hamjui kuwa ni mmojawapo wa waliochonga EPAA hasa ikizingatiwa kuwa ndiye alikuwa kiongozi wa propaganda wa Njaa Kaya? Kama jamaa huyu atapitishwa tumekwisha! Mie nitahama kaya. Maana itakuwa ni aibu iliyoje?” Analalamika Kapende.
“Mie sisikitishwi na wachovu kwa vile kama wataamua kujihujumu kwa kuruhusu hata majangili kukaa ikuu hiyo shauri yao. Mie nasikitikia tembo wetu na faru. Kama waliweza kumsimika balaa huyu Njaa Kaya hata huyo al shabuub wanaweza kumsimika na wachovu wasifanye kitu kama kawaida yao.” Anazoza Mijjinga huku akiwa amekula ndita ile mbaya.
“Kipindi hiki hakubali mtu upuuzi tena. Hebu wajaribu watuletee hao mafisadi wao waone tutakavyowafanyia kitu mbaya,” anatishia Mipawa.
Msomi hamkawizi. “Kama mmeletewa hili balaa kama alivyosema Mijjinga na hamkufanya kitu, mtakifanyaje sasa? Kama mmeshindwa kuwachoma moto majambazi wa Screw ya IpIITL na hawa wa UdAR mtafanya nini kukwepa kutawaliwa na TX? Mtatawaliwa na hata mkewe Njaa Kaya kama ataamua kumuachia maulaji.”
Kapende anachomekea hata bila kungoja Msomi amalize. “Usemayo kaka ni kweli mtupu. Mna habari hili kampuni la bandarini la Ticks ni mali ya Niziro Kadamage na hakuna anayehoji wakati alilipata alipokuwa waziri? Ulize ili kashfa ya Tunituni Ben na Ana Tamaa kujitwalia Kiwila limeishia wapi? Ulizia mabilioni ya Uswizi yameishia wapi? Jamani, hii kaya ni shamba la chizi mtake msitake. Kila mwana kaya analiwa kivyake vyake hata kama haipendezi.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga yalipita mashangingi ya akina Kapuyanga, Ndururu, Mkuyati, Were-ma, Idd Lion na Masaburiz. Acha tuyakimbize ili tuue mtu! Kama si madereva wao kuongeza kasi tungewachoma kama vibaka wallahi.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 11, 2014.

No comments: