The Chant of Savant

Thursday 29 May 2014

Uchumi mnao ila mnaukalia


       Marehemu baba wa taifa mwl Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa Tanzania uchumi tunao ila tunaukalia. Wapo waliomwelewa.  Pia wapo ambao hawakumuelewa kiasi cha kumtafsiri walivyojua na walivyotaka. Habari kuwa Tanzania inapoteza dola za kimarekani bilioni 1.8 kwa mwaka tokana na utawala na usimamizi mbovu wa raslimali za nchi ni ushahid wa usemi huu. Nia ajabu zilipotangazwa viongozi wetu hawakukereka wala kuona lau aibu. Wameendelea na upuuzi ule ule kudai wapo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wakati ni unafiki mtupu.
Hukuna kuzungusha. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo imetufikisha hapa. Ajabu wakati ikitusaliti na kutuuza mchana kweupe walevi wake wa madaraka wanapoteza pesa na muda wetu kutwambia nani anafaa kutuongoza kwa kuwakandia wapinzani wakati wa kuambiwa hawafai ni hao hao walimu wetu wa nani atuongoze na mfumo upi ututawale. Ajabu hawa wanaoshindwa kusimamia raslimali zetu wanajisifia ubingwa wa kuombaomba na kukopa kopa wasijue wanazidi kuzamisha taifa! Wengine wamestaafu na kujiingiza kwenye magendo na uchuuzi.
          Sikumbuki kumsikia katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana wala katibu wa uenezi, Nape Nnauye wakiongolea uchafu huu zaidi ya kuendelea na wimbo ule ule wa jogoo. Lau kutokana na chuki za kibinafsi na ukweli wa hali halisi ya mparaganyiko wa serikali Nape amerudia kuwaita wenzake mizigo japo naye ni mzigo huo huo. Huu ni ushahidi kuwa tusingekuwa na viongozi na watendaji mizigo, kwa raslimali tulizojaliwa Tanzania haipaswi kuwa maskini. Sana sana ilipaswa kushindana na Singapore na Korea ya Kusini nchi  ilizokuwa ikizipiku kiuchumi wakati wa kupata uhuru.
 Bahati nzuri habari hii ilitoka wakati wa ziara yao mkoani Tabora. Watu wa Tabora walitumia fursa hii kumtumia salamu rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Kinana wakitaka atimize ahadi yake ya kujenga bomba la maji toka ziwa Nyanza. Nadhani wangemwendea angesema hakuna fedha ya kufanya hivyo wakati serikali yake ikisifika kwa upuuzi wa kuacha wageni waje wachote na kwenda kujitajirisha wao na nchi zao wakati watu wetu na taifa letu wakiendelea kutopea kwenye umaskini wa kutengenezwa na watawala wavivu wa kufikiri kama aliyeanzisha msemo huu. Kujitoa kimasomaso na kukwepa uwajibikaji, Kinana aliwarushia lawama viongozi wa afya akisema, “Viongozi hawa ni wazembe, wamangimeza na warasimu wanaokwamisha maendeleo ya wananchi. Nakwenda kushikana nao mashati ni lazima wasajili zahanati hizo.”  Ama kweli nyani haoni nonihino lake! Kuna wazembe kama viongozi wa juu wa taifa wanaoruhusu uchumi wetu kunufaisha majambazi wa kimataifa wanaoshirikiana nao? Sikutegemea lolote toka kwa Kikwete kwa kujua fika yeye ndiye mzizi wa balaa hili.
          Hakuna kilichokera kama kugundua kuwa deni la taifa limeumka huku tukipoteza pesa ambayo ingeweza hata kulilipa tena pesa yenyewe tuliyopoteza ndani ya miaka kumi tu. Japo Nyerere alisema: Uchumi tunao tumeukalia, unaweza kuongeza: Akili tunazo lakini hatuzitumii na kama tunazitumia basi ni vibaya na mbaya.
          Kuna viongozi wababaishaji na wasanii wanaotoa ahadi wasizitekeleze ukiachia mbali wanaodandia mambo ya kuwarushia lawama wengine wakati wa kulaumiwa ni wao kama tulivyoonyesha hapo juu. Kuna viongozi manunda na manyang’au wenye uroho na roho mbaya. Hata uwaseme vipi wanajifanya hawasikii wala hawaoni na kuendelea na jinai yao ya kuhujumu taifa letu. Juzi mbunge wa Kigoma Kusini kwa mfano amewatuhumu maafisa wakubwa wa serikali kwa wizi wa shilingi bilioni 200 toka Benki Kuu. Ajabu ya maajabu hakuna anayewashinikiza wawajibishwe na kuchunguzwa hata kuchukuliwa hatua za kisheria. Nani amwambie nani wakati wote lao ni moja? Ni bahati mbaya kuwa na wananchi wetu nao wamekuwa kama kondoo wanaojirahisi kuelekea machinjioni. Hwafurukuti wala kuonyesha hasira zao. Imefikia mahali habari kama hizi zenye kuchusha na kukera zinaonekana kama udaku na burudani kwa waathirika maskini wa nchi hii. Uchumi yaani akili wanazo lakini wanaukalia. Uchumi yaani umoja na nguvu wanavyo lakini wanavikalia huku wakalia kulia na kulalamika bila kuchukua hatua. Wanaliwa lakini hawastuki. Je tatizo ni nini? Woga, au ukosefu wa uaminifu na uzalendo kwa watu binafsi?
          Jiulize ni kiasi gani cha madini tunapoteza kila mwaka ukiachia mbali pesa ya kodi ambayo imefikia hizo dola za kimarekani takribani bilioni mbili? Je ni watalii kiasi gani wanaingizwa kinyemela kutokea nchi jirani ukiachia mbali wanyama wanaouawa kwenye ujangili hadi kuweza kusafirishwa wakiwa hai bila mamlaka kufanya lolote? Tanzania ingekuwa na watu makini na wenye kupenda taifa lao bila shaka serikali ya rais Kikwete ingeishatimuliwa miaka mingi iliyopita. Lakini nani wa kumwajibisha nani iwapo hata watu binafsi hawako tayari kuwajibika kwa nafasi yao kwa kulikomboa taifa lao toka mikononi mwa wababaishaji na matapeli wa kisiasa?
          Jiulize taifa linapoteza mabilioni kiasi gani kwa kulipa wafanyakazi hewa, walioghushi wasiofanya kazi bali kubabaisha na matumizi mengi ya kipumbavu kama ilivyogundulika hivi karibuni ambapo tiketi za ndege za wakubwa kwenda kutanulia nje zililanguliwa mara 16 na serikali ikaendelea na wimbo wake wa kuleta maendeleo kwa watanzania? Mnaleta maendeleao au maangamio?
          Jiulize ni wahalifu kiasi gani toka Asia na kwingineko wamegeuza Tanzania kichaka cha kufanyia uovu wao. Mmojawapo wa hivi karibuni ni yule anayejidai kununua IPTL wakati ni mwizi wa kawaida.
          Imefikia mahali mtu akikutajia jina Tanzania kinachokuja akilini haraka haraka ni utapeli, usanii, uzembe, ubabaishaji na maangamizi ya kujitakia. Kuna kipindi watu walilalamikia ujenzi wa viwanja vya ndege binafsi kwenye machimbo ya madini ambavyo vinatumika kutorosha madini. Ajabu watanzania wameendelea na mambo yao kama kawaida kana kwamba kadhia hii imeshughulikiwa. Kwa kujua udhaifu wao serikali wala huwa ahangaiki na kutatua kero yoyote zaidi ya kuongeza spidi ya kula na kufanya madudu.
           Wakati wa kuwataka watanzania watumie uchumi wao uwe raslimali, akili, urathi wa utulivu na nyingine nyingi kujikomboa badala ya kuendelea kushikwa matekwa na genge la wahalifu ni huu. Hakika, uchumi mnao ila mmeukalia tu.
Chanzo: Dira Mei 2014.

No comments: