The Chant of Savant

Saturday 24 May 2014

Sera ya Mlevi sasa ni kububujikwa michozi

        Baada ya kuinyaka kuwa Katibu mkuu wa Chama Twawala Abduli Kinamna alibubujikwa michozi kule kwa akina Mwanawetu, Mwanawima, Mzindakaya na wengine wengine wengi, akiwalilia wakulima wanaonyonywa, mlevi amependa staili hii ya kukwepa kuwajibika kwa kumwaga michozi ya mamba.  Ukisikia usanii uliotukuka ndiyo huu.  Jamaa anafaa kupewa nishani ya kuweka walevi sawa. Haiwezekani mtu mwenye mamlaka ajilizelize tena akishindwa kuwawajibisha watu wadogo wa chini yake kusiwe na namna. Hata hivyo, ni rahisi mtu na staili ya namna hii kustukia. Cheats never prosper walisema waswahili.
Hawa jamaa kama walioingizwa mkenge kwa machozi ya mamba kama si kuendekeza huruma si wangemtwanga angalau juju. Sijui nini mantiki ya kushindwa kusumbawanga lau akashika adabu mjivuni huyu? Nisingekuwa bize, nilitamani niende kule kulikoungua jembe ukabaki mpini nimzodoe Kinamna kuwa uongozi si uongo na kulialia bali kutatua matatizo ya walevi. Hivyo, walevi wasimwamini bali wamzomee hata kumtia adabu kama aliyotia jamaa yangu Njaa Kaya kule kipindi fulani kule kwa akina Twambombo Tununu waliompenda hadi wakamrushia mawe ya upendo.
Kwa vile Mlevi amekuwa akiwaibia na kuwatapeli walevi hasa wanapompa ofa au kumkopesha asirudishe njuluku, basi ataanza kuangua kilio kila akikutana na anayemdai. Badala ya kumlipa fweza unamlipa fedheha ya michozi kama Kinamna. Badala ya kutatua tatizo ambao kwa mlevi ni deni au kutoa huduma kwa Kinamna na sirikali ya rafiki yake, unamwaga chozi na wajinga na walevi wanakuamini kuwa unawamaindi wakati unawa-fool. You better fool them before they fool you for if they fool you without fooling them you’ll end up in trouble like Muamar Gaddafi they fooled that they used to love while they actually loved to hate him up till they butchered him like Kibaka the way they wish they should treat you the one they love to hate and fool that they love. Kwa unyambilisi wangu hili sitafsiri otherwise mniahidi kuwa mtaacha ukondoo na unjiwa na ukijiko na uupawa.
Kijicho huchota chakula lakini huwa hakili sawa na upawa. Kondoo hujifanya mtiifu hata kwa mchinjaji wake huku njiwa akijifanya hayamhusu wakati yanamhusu. Hata hivyo, hivi ni vitu na hayawani si walevi wanadamu kama nyinyi. Ni matusi ya nguoni mwanadamu kutenzwa kama kitu au hayawani.
Usishangae kuandika sentensi ndefu namna hii. Nina uwezo wa kuandika sentensi moja ikajaza ukurasa mzima. Mie sijagushi ati. Nimesoma tena ughaibuni mnakozimikia kuanzia shahada ya kwanza hadi ya mwisho. Hayo tuyaache. Sitaki nionekane najidai au kujipigia debe kama akina Kinamna na Nipe Mapepe Nnauyee Ninaye walioishiwa hadi wanaanza kukamatana uchawi kwa kuita wenzao mizigo. Japo ni kweli wale walioitwa mizigo ni mizigo kweli kweli hata waliowaita mizigo nao ni mizigo ile mbaya au siyo. Hebu tuachane na akina Kinanae na mapepe yao yasiyo na maana.
“Heri kufa nimesimama kuliko kuishi nimepiga magoti,” alivyosema Field Marshal Dedan Kimathi wa Kenya ambaye tulizoea kupata kanywaji pamoja kabla ya wenzake hawajamsaliti na kumnyotoa roho halafu wakamwaga michozi kama Kinamna ilhali ni michozi ya mamba aliyeshiba “anayemlilia” aliyemuua na kumgeuza kitoweo.
Si juzi nilituhumiwa kuwa nauza bwimbwi na pembe za ndovu kana kwamba mimi ni ndata. Kama Kinamna, baada ya kutuhumiwa badala ya kutoa maelezo, nilimwaga michozi hadi ndata wakanichangia uchache kwa kunionea huruma wasijue tuhuma zenyewe ni kweli. Hata jamaa yangu alipotuhumiwa kusafirisha vipusa, si alimwaga chozi hadi Njaa Kaya akaingia mkenge na kumpa ulaji anaoutumia kupiga fweza kwa njia ya kumwaga michozi. Michozi, kama mipasho na mitusi kule Idodomya inalipa.
Kwa vile michozi inalipa,ningeshauri hata wale mafwisadi papa waliotuhumiwa hivi karibuni kujichotea bilioni 200 kwenye akaunti ya Scrow iliyogeuka screw wamwage michozi walevi watawaonea huruma waendelea kutesa na kupiga njuluku nyingine kama hawana akili nzuri. Hata yule karasinga gabacholi anayejifanya kuinunua IpTl wakati ni tapeli wa kawaida akistukiwa anaweza kumwaga chozi na mambo yakaisha au vipi?
Ndugu zangu akina Sossie Muongo, Benny Ndururu, Elyakim Maswi, Saada Mkuyati na Freddie We-rema mpo? Yaani mmeamua kufuata nyayo za akina Basiri Mlamba na David Balalii kwa kuchonga EPA nyingine siyo? Huwa najiuliza sipati jibu. Sijui kamana walevi wote na wadaganyika huwa wanajiuliza swali hili. Kwani njuluku huwa zinaibwa karibu na kuelekea uchaguzi wa uchafuzi wa uchakachuaji kama hakuna mkono wa nambari wahedi na madingi wake majizi? It is too boring to evidence such megalomia every year. Nawashauri mkipata jukwaa la kujieleza mmwage michozi kama Kinamna ili wale mnaowaibia wawaonee huruma na kudhani hamna hatia. Mara hii mmesahau akina Yuda Iskarioti walivyomwaga chozi wakati ndiyo hao waliomsaliti mwana wa Adamu siyo? Mwanikumbusha mlevi mmoja aliyefumwa na bi wa mwenyewe tena amekumbatia akamwaga michozi na kudai walikuwa wakionyesha mshikamano!
Najua wengi wasiojua faida za kanywaji na bangi huwa wanapenda kunikosoa na kuniona kama hamnazo. Nawashaurini, tena kwa upole, msihangaike na mimi nisemaye bali yale nisemayo. Mie ni mtume, sawa na yule Paulo aliyekuwa akiuwa wanafunzi wa Yesu. Alipoona ngoma inakuwa nzito aliamua kujisalimisha. Fikiria. Kama waliweza kumwamini muuaji, kwanini wasiniamini mlevi na mvuta ganja ambaye wala simkwazi mtu zaidi ya kumpa vipande ili angalau aamke na kudai kilicho chake mapema kabla akina Chukua Chao Mapema hawajamaliza kila kitu? Hawa jamaa wanaweza kumaliza kila kitu sitishii kama akina Joni Kombakombo na Bill Lukuvie au Njaa Kaya Kiquette. Jamaa wana roho mbaya na wanaweza kufanya kweli.
Salamu maalumu kwa walevi na wavuta bangi wote wanaofia ukweli bila woga. Heri kufa mmesimama kuliko kuishi mmepiga magoti au siyo?
Chanzo:  Nipashe Mei 24, 2014.

No comments: