The Chant of Savant

Tuesday 25 February 2014

Kufungwa mtoto wa rais faida ya kuchagua upinzani

Taarifa za kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili kwa mwana wa aliyekuwa rais wa Zambia Rupiah Banda aitwaye Andrew (53) ni faraja kwa wanaochukia ufisadi na utawala wa kifamilia ambapo madaraka ya mtu mmoja hutegemewa na kutumiwa na ukoo mzima.
Andrew Banda alifungwa kwa kosa la kutumia madaraka ya baba yake na kujipatia rushwa ya mamilioni ya shilingi toka kwenye kampuni moja ya ujenzi ya kitaliano. Je kwanini tukio lililotokea Zambia livute hisia za wengine nje ya nchi? Jibu ni rahisi kuwa kutokana na utawala wa kifisadi kutamalaki ambapo watoto au wake wa marais nao hugeuka marais wadogo na kujipatia utajiri wa haraka kwa njia haramu, kusikia kuwa mmoja wao hata kama ni kutoka nchi nyingine ni ushindi wa aina yake.
Zambia imekuwa mbele kwenye suala la utawala bora na demokrasia. ni nchini Zambia ambako mke wa rais amewahi kuhukumiwa kifungo na akafungwa kweli. Hii ilitokea mnamo Machi 3, 2009 ambapo Regina Chiluba mke wa rais wa zamani Fredrick Chiluba alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu kutokana na kutumia madaraka ya mumewe kujipatia mali kinyume cha sheria. Je Afrika inao akina Andrew na Regina wangapi ambao hawajafikishwa mbele ya haki? Tunawaona wakituibia au kutumia ofisi zetu kujipatia utajiri kupitia NGO na biashara za ajabu ajabu kama kuwatumia makuwadi wao kununua mashirika ya umma kwa bei ya kutupwa kama ilivyotokea hivi karibuni kwenye kashfa ya uuzaji wa kutupwa wa UDA ambao nyuma yake  kuna mtoto wa mkubwa fulani ambaye ikifika wakati wa kumtaja tutamuanika. Kinachokera ni kushuhudia wezi hawa na makuwadi wao wakitukoga hata wakati mwingine kutunyanyasa, na kutudhulumu hata baada ya kutuibia kama umma.
Wakati Andrew Banda akifungwa kwa kujipatia $ 63,000, Regina alikuwa amejipatia dola 300,000. Hii ni rushwa moja. Je ni rushwa kiasi gani ambayo haikufichuka?
Kitu kinachovutia na cha kuigwa mfano ni namna mamlaka zilivyogundua ufisadi wa Andrew. Alikutwa akiwa na dola 63,000 kwenye akaunti yake. Alipotakiwa aeleze alivyozipata alishindwa na hivyo mahakama kuhitimisha kuwa alizipata kihalifu. Hivyo, ikaamua kumkuta na hatia. Je watoto na wake wa watawala wa nchi kama yetu inayosifika kwa uwekezaji wa kijambazi wana akaunti nono kiasi gani? Je tunaweza kuwakamata vipi? Jibu ni rahisi. Chagua upinzani kila kitu kitafichuka. Zambia haikupiga hatua hii ya kupigiwa mfano kwa ujanja zaidi ya kuwa na serikali ya upinzani madarakani. Tumeyaona kama haya nchini Malawi hata kama hayakufikia ukubwa wa Zambia.
Hivyo, njia rahisi kwa watanzania kupambana na kizazi cha kijambazi kitokanacho na ndugu na jamaa wa wakubwa kutumia nafasi zao kuibia umma ni kuondoa chama tawala madarakani ili kila kitu kifumuliwe upya. Tumekuwa tukilalamikia kashfa kama EPA, Richmond, Kiwira na nyingine nyingi. Uking’atua CCM kila kitu kinakuwa wazi na wale waliojiona hawawezi kunyea debe wanajikuta gerezani. Najua watanzania wengi wanakasirishwa na wizi wa kilafi na kiroho mbaya ambapo wengi wa wanaoiba hawaibii shida bali roho mbaya na tabia mbaya.   Haiwezekani umaskini uendelee kuongezeka huku genge la majambazi likiwashika matake taifa na kusiwepo na harakati za kukomesha jinai hii. Sasa ni juu ya watanzania kujilaumu kutokana na kutopenda mabadiliko. Bila kubadilika na kubadili utawala uliopo wengi watazidi kuumia. Tukichagua upinzani kashfa zote kama zile za kuficha fedha nje, mihadarati, mikataba ya kijambazi na uwekezaji wa kiwizi vyote vinafumliwa na haki inatendeka. lakini kama tutaendelea kuchagua status quo pro quo itakuwa ni kuteseka sana na sana huku wahalifu na mafala waliopata ukwasi si kwa ujanja wao bali vyeo vya baba zao au waume na jamaa zao wataendelea kututambia kwa chumo la wizi utokanao na pesa yetu wenyewe. Mafala watatugeuza mafala kiasi cha wao kuonekana wajanja wakati ni wahalifu wa kawaida tu.
Andrew kabla ya kukutwa na hatia alikuwa anatumbua na kuonekana mjanja wakati ni mhalifu wa kawaida.kabla ya Regina kupatikana na hatia alikuwa akiabudiwa kama first lady wakati ni mwizi wa kawaida tu. Tutaendelea na utawala wa kijambazi hadi lini? Tumezidiwa na wakoloni ambapo mke wa gavana wa kikoloni wala wanae hawakuwa magavana wadogo wala wabia wa wahalifu waliowatumia kama makuwadi wao!
Kwa umri wa Andrew ni aibu kumtegemea baba yake wakati ni mtu mzima mwenye akili anayepaswa kujitegemea. Wenzetu ni wa kweli kwao binafsi na wale wanaowaongoza. Mfano mwingine ni wa Hilary Clinton. Alipokuwa first lady wala hakutumia madaraka ya mumewe ingawa alikuwa akipenda madaraka. Baada ya muwe kumaliza muda wake, Hilary aliamua kujaribu kugombea urais na kushindwa. Hata hivyo, alijijengea heshima kuwa hakutumia madaraka ya mumewe kutimiza malengo yake ya kisiasa kama wanavyofanya wake za watawala dhalimu na fisadi. Hilary hakuiba hata dime moja ya wamarekani. Hakuanzisha NGO wala binti yao Chalsea hakutanua na kuiba kwa jina la baba wala mama sawa na wengi tunaoshuhdia.
Tumalizie kwa kuwahimiza watanzania kuchagua mageuzi ili kuondoa mfumo mbovu uliotamalaki wa kuhudumiana ambapo utawala unageuka mali ya ukoo ambao nao unageuza taifa kuwa shamba la bibi. Tukichagua upinzani tutaweza kuwakomesha akina Andrew na Regina wetu kiasi cha kurejesha heshima na maadili katika utumishi wa umma. Hatuwezi kuendelea na mazoea mabovu yaliyopo ambapo wachache wananufaika kwa kuuibia umma. Lazima tuwajibishane na wakati wenyewe ni huu.
Chanzo: Dira Feb., 2014.

No comments: