The Chant of Savant

Wednesday 8 January 2014

Tumerudi upya mambo mapya mwaka mpya


           Wapendwa wasomaji wa safu hii,
Kabla ya kuwaletea nini ajenda na mjadala wa kijwe cha leo, tuonaomba  kwa niaba ya wazee wa kijiwe na kwa  unyenyekevu msamaha kwa kutokuwa hewani kwa takribani mwezi. Tunawashukuru kwa utulivu na uvumilivu wenu. Maana kuna msomaji aliniambia kuwa alikuwa na mpango wa kutangaza maandamano ya kutaka kujua kwanini kijiwe hakikuwa kikitoka.
Mengi yalisemwa. Wapo waliodhani kuwa tumekolimbwa au kunyamazishwa. Wapo waliomzonga mhariri kutaka kujua kunani. Wapo waliosema nimekamatwa baada ya kukibandiwa kabla ya kumwangosiwa au kumvungiwa na mambo mengine mengi. Wapo waliodhani kuwa Kanji na Kanungaembe Sofia walitia mtima nyongo wasijue wachawi si wao bali wengine. Nawashukuruni sana hasa msomaji wangu Shaddy Mijjinga ambaye alinisumbua na maswali kweli kweli.
Kwa ufupi ni kwamba wote tu wazima kuanzia mimi Mgosi Machungi, Msomi Mkatatamaa, Mbwamwitu, mzee Mipawa, Kapende, mzee Maneno na mzee Kidevu na akina Mchunguliaji bila kuwasahau ami Mpemba, bi Sofia aka Kanungaembe na dugu moja Kanji.
Pia n achukua fursa hii kutoa rambi rambi kwa kufiwa na mzee Mandela ambaye bahati nzuri nilihudhuria maziko yake ingawa kwa staili tofauti na wale mafisadi waliokwenda kula kuku na kutalii. Wanakijiwe walinichangia uchache nikawakilisha na rambirambi zao. Sitaki niseme makufuru niliyoshuhudia kule ambapo malaika alizikwa na wenye dhambi kibao.
Tuyende ku nchito. Kijiwe cha leo ni cha aina yake. Naona kama kawa mgosi Machungi anaingia akiwa amevalia kanzu yake na kofia ya tarabushi.  Mpemba naye keshajaa tele kama pishi la mchele huku Kapende na Mipawa wakiwa tayari ugani farasi kufungiana nyama na nyangwa.
Msomi kama kwaida yake hakosi mabuku makubwa mkononi huku Mbwamwitu akiwa na bashasha zake.
Mpemba analianzisha, “Yakhe hebu tupe habari za safari yako kwa Madiba.”
Nakunywa kahawa yangu huku nikijiweka vizuri kwenye benchi.
Nasema, “Kwanza nawashukuru nyote kwa kuniwezesha kufika Sauzi. Licha ya kufikia J’burg kama wao wanavyoiita Johannesburg nilifika kijijini kwa Mandela kule Mvezo. Ni kama Butiama. Hakuiba wala kujenga makazi ya kifahari kama yale ya kijijini kwa Zuma Nkandla. Sema kwa jina la Mandela na wema wake, bado Mvezo panaheshimika kuliko hata hiyo Jo’beg.”
Mpemba anachokemea, “Yakhe wataka sema paheshimika kama Nsata au Bwagamoyo?”
Msomi anadakia, “Ami acha utani. Huwezi kulinganisha chawa na tembo. Huwezi kulinganisha pango la wezi na hekalu la Mungu.”
Msomi anakunya kahawa na kukatua kashata na kuendelea na kuchomoa gazeti la kikameruni toka nchi jirani na kusema, “Umeona hiki kibonzo kinachoonyesha viranja wetu wakiingia kwenye viatu vya Madiba na kupwaya?”
Kapende anachomekea, “Hao pamoja na kumezwa humo aangalie wasivijaze vinyesi au kuviguguna kama panya kama siyo kuvipiga mnada.”
Kijiwe hakina mbavu isipokuwa Kanji na bi Sofi ambao walionyesha wazi kutopenda vimondo vilivyokuwa vitupwa kwa walaji wa kaya.
Sofi anachomekea, “Kwani mawazo ya huyo mchora vibonzo ni msahafu hadi yawe kweli?”
 Mipawa anakwanyua mic haraka, “Ukitaka kujua ukweli wa jambo uangaliage jinsi watu wanavyolipokea au kulipenda au kuliponda. Hiki kibonzo kimeeleza ukweli ndiyo maana wengine unawachoma.”
Mbwamwitu anadakia, “Unawachoma wapi?
Mipawa anajibu kwa mkato, “Popote watakapoona unawachoma.”
“Yakhe mie naona mambo ya kuchomana tuyaache tuongelee uaminifu na mchango wa Madiba ati.”
Nlisema kwa ufupi kuwa Madiba hakuwa fisadi wala mpenda maulaji kama wengi wa waliomzika toka barani kwetu.
Kwa vile tulikuwa na mambo mengi ya kuzungumzia, tulirukia kwenye hali halisi ya mambo kwenye kaya ambapo tunafunga mwaka.
Mgosi Machungi anasema, “Wagosi naona tinafunga mwaka kwa mkuu kuendelea kuzuua kiasi cha kutisha. Juzi tilimuona akienda kwa akina Bonjour, mara kwa Diba mara kwa Nyayo sijui kwanini hajifunzi.”
“Ajifunze nini wakati wanaopaswa kumshikisha adabu hawajifunzi?”  Anajibu Msomi kwa kejeli.
Anaendelea, “Mie naona tungeangalia hili la Mzigo sorry Mzito Kabwela kuonyesha makucha yake asijue watayakata kabla hayajaparura.”
Mipawa anadandia, “Mbona walishayakata kiasi cha mtu mwenyewe kuanza kuweweseka!”
Kapende naye hajivungi, “Hakuna kitu kilimmaliza huyu limbukeni kama Chama Cha Mafisadi kuonyesha eti huruma kwake. Wao ya Chakudema yanawahusu nini?”
Sofia anadandia, “Kwani ni vibaya kumuonea huruma mtu hata kama ni adui yako?”
Kanji ambaye alikuwa kimya naye anaamua kukatua mic, “Hapana baya Sofi. Naona chama penda vatu diyo maana naona huruma kwa Bwela.”
Mzee Maneno ambaye naye alikuwa kimya anaamua kuweka timu, “Ukiona hivyo jua lao moja. Si nasikia walikuwa wakimlipa pesa nyingi ughaibuni ili aibomoe chakudema na hajakanusha.”
“Kwa vile msimu wa wanasiasa kusiasia urongo na kamba zao unawadia, tunapaswa kujiandaa kuona mengi.” Alidokeza Kapende.
Mgosi naye hakutaka kujivunga, “Nashauri mwaka ujao tijiandae kuwatia adabu wanaotaka kutitumia kama majembe. Tihakikishe pesa ya ughaibuni inaejeshwa, kina Kagoda wanakamatwa, mafisadi wanaojipitishapitisha wakihonga njuuku za wizi wanapigwa chini na mambo mengine.”
Mipawa anaingilia kati, “Tuazimiege kuwa mwakani badala ya kutwambia kilimo kwanza watwambie mibwimbwi na kuficha njuluku nje kwanza.”
“Yakhe mie naona mwakani iwe ni kamba kwanza ukweli mwisho. Hivi ile nguvu ya soda ya Mwakiwembe ya kupambana na wauza bwimbwi nayo imeishi wapi?” Alichomekea Mpemba.
“Si ajabu hata wale dagaa wa airport washarejeshwa kwa mlango wa nyuma au kuhamishiwa  kwingine. Bongolalaland hii ati,” Anajibu Mchunguliaji.
Msomi anadakia, “Nadhani Mwaki naye ni mzigo kama Mizengwe, Mgimua, Chiizi, Milima na Hawa wana Ghasia na wengine. Nadhani kama kungekuwa na uwezekano wa kuwachapa bakora hawa jamaa ingewafaaa sana. Maana they are good for nothing so to speak.”
Naona bi Sofi na Kanji wanaamua kukitoa baada ya kugundua kuwa vimondo vingi vinaelekezwa kwenye genge lao.
Kwa ufupi ni kwamba kijiwe kimepania kuja na ukali mpya mwaka mpya kuhakikisha wababaishaji na mizigo wanapigwa chini.
Kikiwa kijiwe kinanoga si mvua ikaanza kunyesha! You know what followed guys. Guess what. Kila mtu alitimka kutafuta pa kujikinga.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 8, 2014.

No comments: