The Chant of Savant

Saturday 4 January 2014

Nipeni wizara ya Mali ya siri na utajiri

Baada ya mlevi kushuhudia wakubwa wakitibuana, kuchongeana, kung’oana hata kufichuana, anapendekeza apewe Wizara ya Mali ya siri ya utajiri ili akomeshe ulaji wa kijinga na kilafi unaoendelea.  
Japo sina uhusiano mzuri na jamaa yetu Njaa Kaya kwa vile anajua kichaa changu cha kupenda haki, nawaomba watu wa mjengoni watumie turufu yao kuhakikisha napewa wizara ya Mali ya Siri na Utajiri wa vigogo ili niinyooshe once and for all.  
Naomba wanipe rungu nirejeshe heshima na usalama wa raslimali zetu kwa vile ufujaji, wizi, ujambazi na ujangili unaoendelea usipokomeshwa, kuna uwezekano vizazi vijavyo vikakojolea makaburi yetu kutokana na kuvisaliti kwa tamaa za kipumbavu na ubinafsi vilivyopindukia. 
Japo inaitwa wizara ya Maliasili na Utalii, kwa walevi hii si chochote wala lolote bali wizara ya mali ya siri na utajiri wengine huiona kama wizara ya mali ya siri na ujangili ambayo wengi wanainyemelea ili wale bila kunawa tena kwa mikono miwili. 
Hatuwezi kuendelea kuvumilia ushenzi huu. Lazima jinai hii ikomeshwe tena haraka na mara moja. 
Kama nitapewa rungu, nitarejesha Loliondo na kuwakamata akina Mhunidin Ndongala na wale wote walioshiriki na kushirikiana kuhujumu taifa bila huruma wala kuangalia nyani usoni. 
Sitanii wala kufanya sanaa kama wale wanasanii mliokwishawachoka. Wala si fikra za kilevi na bangi. Walevi wanajua fika kuwa waliibiwa na kutendewa jinai chini ya utawala kidhabu ulioruhusu ufisadi na ujambazi mbuzi vianze kujichimbia kwenye kaya.  
Hivyo, amini nawambieni wenye kusikia wasikie na wenye kuelewa waeleve maneno haya ya unabii. Lazima Loliondo irejee mikononi mwa walevi hata kama itabidi kunyonga watu.  
Kwani, wao wananyonga wangapi hasa wanapoendelea kuchuma huku dhiki zikiwadedisha walevi? Isitoshe wananyonga wanyama wetu hovyo hovyo na kwa kasi ya kutisha kiasi cha wengine kama faru kuanza kutoweka.  
“We can’t stay a side and look while our hunk is being raped by evil’s and devil’s agents in the name of investment. How can we invest in destruction as if we’re zombies and vagabonds?” 
Ili kutimiza ahadi zangu, nitawahoji wote wanaotuhumiwa kuhusika na ujambazi huu wa kuliangamiza taifa hata kama itabidi kumhoji mzee Ruxa kwa kunyamazia ujambazi wa Loliondo.  
Japo ana kinga, nitataka nimhoji anipe mantiki ya kuruhusu jinai hii itendeke chini ya uangalizi wake kama hakuwa na maslahi yoyote.  
Itabidi nipate maelezo ni kwanini wahusika waliruhusu huu ujambazi wa mchana kama kweli hawakuwa na maslahi binafsi? 
Kwanza, nitahakikisha nalipa fidia kwa familia ya marehemu Stan Katabaro aliyenyotolewa roho na ujangili na kumtangaza shujaa wa utokomezaji ujangili hasa wa kiutawala na wale wote walioathiriwa na ujambazi huu wa mchana. Hii itatoa motisha kwa walevi wote wanaojua madudu na mbinu za watenda jinai hii kujitokeza na kunipa taarifa na ushirikiano.  
Pili, nitawahakikishia usalama wao na familia zao. 
 Tatu, nitahakikisha nataifisha mali za mawaziri na vigogo wote na maajenti wao wanaosadikiwa kuigeuza wizara hii mali ya siri na ulaji. 
Nne, nitamtimua mtoto wa mfalme wa kimanga ambaye alijinyakulia Loliondo kupitia kwa mawakala wake washenzi waliokuwa na madaraka. 
 Wote waliopata vitalu na vibali kupitia rushwa au kujuana wakae mkao wa kuliwa. Naapa kabisa. Sitanii wala sijaribishi bali kufanya kweli. Kwani kama walevi tumechoka kugeuzwa mashahidi wa maangamizi yetu na vizazi vijavyo. 
Tano, nitahakikisha namtoza fidia huyu mmanga kwa muda aliotumia Loliondo bila kulipa kodi wala kufuata sheria. 
Sita, nitahakikisha wale wote waliouza wanyama wetu nje wananyongwa hadharani mbele ya walevi.  
Saba, nitahakikisha wale waliouza mahoteli yetu ya kitalii kwa bei mchekea wakae mkao wa kuliwa. Wakae wakijua kuwa nikichukua ukanda nitawanyongelea mbali na kuhakikisha mali zao zinataifishwa huku nikibatilisha mikataba ya uuzwaji wa hoteli husika. 
Nane, nitawasweka ndani vigogo wote wenye kulalamikiwa kupewa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria. 
Nadhani akina Pio Msekua, War Kawawa and family, Andaaman Kinamna na Mood Sefu Khatib wananipata.  
Najua mambo yao na jinsi ambavyo walitumia madaraka kujinyakulia vitalu. 
Tisa, nitakomesha ujambazi unaoendelea ambapo vigogo wa wizara huenda ughaibuni kutanua huku wakijilipa ‘per diem’ kwa kisingizio cha kwenda kule kutangaza utalii. 
Kumi, nitakomesha uwindaji haramu na ujangili kwa kuwaongoza walevi kusimamia mbuga zetu za wanyama. Hata uwanja wa ndege na mipakani nitajaza walevi na wavuta bangi ili waonyeshe wanavyoweza kufanya kazi vizuri kuliko walevi wa ngawira.  
Heri wangevuruga walevi kwa vile ni walevi kuliko washenzi wanaoitwa waheshimiwa wakati ni wezi wa kawaida tu waliojificha nyuma ya madaraka. 
Kumi na moja, nitaendesha operesheni Tokomeza Ujangili kwa kuwashughulikia majangili wote yaani wale wa mbugani na wa maofisini.  
Sitakuwa na cha msalie Mtume wala nini bali kukamata tu. Pia sitaruhusu kuingiliwa na kiumbe yoyote awe mdogo au mkubwa. Nikipitisha uamuzi umepita. Atakayejiletaleta na cheo chake namuanika kwenye magazeti ili jamii imjue. Wale ndata wanaotumia bunduki na magwanda yao kufanya ujangili, wakae mkao wa kuliwa. Nitawakamata na kuwanyonga sambamba na mabosi wao wanaowaachia watende jinai hii kwa walevi.  
Wanadhani hatuwajui na jinsi migari yao inavyotumika kufanya ujangili kama wale waliokamatwa kule Mugumu? 
Walevi wanawajua wao na mitandao yao. Wanajua kila kitu na wako tayari kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa bila huruma wala upendeleo. 
Ifahamike wazi. Sitatoa muda wa watu kujipima na kufanya maamuzi magumu. Nitafanya maamuzi magumu mwenyewe kwa vile mimi na walevi ndiyo tunaokabiliwa na maisha magumu yatokanayo na maamuzi na tabia za kipumbavu za baadhi ya watu kuuza mali ya kaya kwa manufaa yao binafsi.  
Hii kaya ni yetu wote kwa usawa bila kujali cheo wala mitandao.
Kama nitaeleweka na kupewa rungu, aminini hii ndiyo saa ya ukombozi wa kaya hii na raslimali zake.  
Lazima nirejeshe wizara ya Mali ya Siri na Utajiri kuwa ya Maliasili na Utalii na si ujambazi na ushenzi.  
Nawatakieni heri ya Krismas na Mwaka Mpya wa ku fanya maamuzi magumu 

Zikomo kwa mbiri.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Jan., 4, 2014.

No comments: