The Chant of Savant

Saturday 28 December 2013

Mlevi ataja umaskini wake

Nitafunga  mwaka huu wa ufisadi kwa staili ya namna yake. Wakati wengi wakijiandaa kuwaibia walevi, mie naonyesha njia ya uadilifu na uwajibikaji.Baada ya wenye mali na mamlaka wanaopaswa kutangaza utajiri na mali zao kisheria kula pini, mlevi nimeona niwape changamoto kwa kutangaza umaskini wangu.

Huenda hii itakuwa suto na hamasa kwao watie akilini na kuacha utoto. Nina sababu nyingi nzuri tu za kutaja umaskini wangu. Cha mno ni kwamba nafanya hivyo ili kuondoa dhana kuwa mimi ni kibaka mwenye madaraka niwaambiao watu walipe kodi ili nisweke ndani mimi na mke wangu, vitegemezi vyangu na waramba viatu wangu.
Pia ni ushahidi kuwa sijaficha hata njuluku moja ughaibuni. Hivi ile so ya wazito kukwapua njuluku na kuzificha Uswizi ya Uswazi nalo limeishia wapi au wahusika wameamua kula pini na kufunika kombe ili mwanaharamu ayeye?
Nasema wazi. Tangazeni mali zenu, za wake zenu hata nyumba ndogo na vitegemezi, marafiki na washikaji wenu wote.
Mkifanya hivyo mtaondoa dhana kuwa ni wezi wasiopenda mali zenu za wizi na ufisadi kujulikana.
Nisingependa dhana hii ienee ingawa sitazuia isienee iwapo wahusika hawataki kuliona hili kama nionavyo mimi.
Inashangaza kusikia wazito wakihimiza walevi wawajibike wakati wao hawawajibiki.
Wanahimiza watu walipe kodi wakati wao wanakwepa kufanya hivyo huku wakitumia nafasi zao hata kutoa misamaha ya kodi kwa wezi wengine!
Kutangaza umaskini kunahitaji moyo. Kunahitaji kile ambacho waingereza huiita ‘the courage of the mad’. Nami kwa vile nina moyo wa mwendawazimu, naamua kutangaza umaskini wangu tena bila aibu.
Heri umaskini wangu ujulikane ambao ni kigezo cha ukweli wangu kuliko kuendelea kuficha mali haramu itokanayo na ujambazi na ufisadi.
Napanga kuwaita waandishi wa habari na kutangaza mali zangu ambazo nitazitangaza kwanza kwenye uga huu.
Hii si mara yangu ya kwanza wala mwisho kutaja mali zangu hata kama zinatia aibu.
Nafanya hivyo mara kwa mara ili kuwakumbusha walevi wenzangu wa mali na ulaji madaraka na ufichi nao wataje mali zao.
Pia hufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa kipato hukua na kupungua kila mara. Hivyo lazima nitoe ‘update’ ya mali zangu.
Naomba ifahamike kuwa sina mali ya wizi hata moja. Ukiachia mbali kumwibia bi mkubwa uchache kidogo wa chakula kwenda kununua gongo na bangi, mie si mwizi wa kuitwa mwizi wala kidokozi. Hivyo, umaskini ‘sorry’ mali nitakazotaja kwa mujibu wa sheria ni halali.
Pia nichukue fursa hii kuwataka wezi wasijihangaishe kuja kuvunja ubavu wa mbwa wa mwenye nyumba wangu bure.  Nyumba ninayoongelea haina hata choo.  Inapotokea mtu akabanwa mara nyingi huwa tuna ‘download’ vichakani.
Sina cha maana cha kuiba zaidi ya umaskini mtupu.  Pia nichukue fursa hii kusema wazi. Kwangu asiyetaja mali zake ni mwizi bila kujali ni mkubwa au mdogo.
If there is anything that roils me to death is this behavior of concealing one’s wealth.  To me, those who don’t declare their wealths are thieves and corrupt creatures that shouldn't be in public offices stealing and abusing them.
Lo! Naona nimechukia hadi ukameruni unanitoka hata bila kituo!
Zifuatazo ni mali ninazomilki.
Kwanza, ni tunguli nilizorithishwa na baba yangu ambaye naye alirithishwa na baba yake yaani babu yangu.
Pia nina panya kama nane hivi mmoja ni mjamzito na mwingine alitoa mimba siku zilizopita. Waliobaki ni vitegemezi.
Pili ninamilki kikosi cha chawa ambao idadi yake siijui. Laiti kama chawa wangekuwa wanawekwa benki Uswizi basi ningekuwa tajiri.
 Pia ninamilki kigoda nilichorithi toka kwa baba yangu ambacho ni alama ya kuwa mfalme wa walevi na wavuta bangi.
Tatu, ninamilki kitanda cha kamba ambacho kimesaidia ndoa yangu na bi mkubwa isivunjike. Maana kila aniudhipo nikataka kumchapa talaka, hunywea atishiapo kuwa ataondoka na kitanda chetu cha kamba.
Wakati mwingine hulalamika kumwambia kuwa nitaondoka mimi yeye abaki mradi kitanda kibaki. Huhofia kukosa pa kulala.
 Hivyo, kitanda hiki kimekuwa nyenzo na sababu ya kudumu kwa ndoa yetu ya uhakika kama ni makapuku hasa ikizingatiwa kuwa asiye na kitu mara nyingi hana utu.
Sambamba na kitanda, namilki bi mkubwa wangu na nyumba ndogo kadhaa. Moja ni mama muuza mataptap na nyingine mama ntilie wa pale mtaani na ya mwisho ni shugamami anipaye mshiko wa kwenda kujinoma ulabu.
Nne lazima nikiri kuwa ingawa jiko la mkaa na la mchina nilinunua mimi, zana hizi adhimu zinamilkiwa na bi mkubwa.
Pia hizi zana zimegeuka silaha anazotumia bi mkubwa kunitesa akijua fika kuwa siwezi kumpa talaka kwa kuhofia nitapikia nini.
Tano, namilki mchupa wangu wa kunywea gongo ambao ni zana muhimu katika maisha yangu. Maana, baada ya bi mkubwa mpenzi wangu anayefuatia ni mchupa huu.
Nilipookota mchupa huu sikujua kuwa ungenimeza.
Nilijikuta nimetumbukia ndani yake. Hakika ni rahisi kungia kwenye chupa lakini ni vigumu kutoka. Kuingia kwenye chupa hakuna tofauti na kumtoa jini kwenye chupa.
Sita, namiliki shahada ambazo ni magunia zisizo za kughushi wala kunisaidia kuukata kwa vile siko tayari kujikomba wala kutumiwa kama sina maana.
Saba, namilki daftari ambamo huandika wote niliowakopa au kukopesha ili wasinidhulumu au kunibambikia madeni kama kesi za ndata kwa watu wasio na hatia.
Nane, namilki nyumba ndogo mbili ambazo moja ni mamantilie ambaye huniwezesha msosi niwapo kwenye mihangaiko yangu na nyingine ni ‘sugar mammy’ au mama sukari anipigaye tafu wakati wa msoto.
Tisa, namilki taa ya chemli ambayo hutusaidia kutokana na ubavu wetu wa mbwa kutokuwa na umeme.
Ulikatwa baada ya kushindwa kulipia ‘bills’ baada ya Tanesco kuwa wakipandisha bei kila mara ili kuwalipa mafisadi wao hasa Dowanis na IpTL ambao wameigeuza kaya yetu shamba la bibi.

Chanzo: Nipashe J'mosi Des., 28, 2013.

No comments: