The Chant of Savant

Tuesday 26 November 2013

Mkapa: Usemayo kweli japo nyani haoni ...?



HAKUNA  sehemu mstaafu Benjamin Mkapa aliniacha hoi kama pale aliponukuliwa hivi karibuni akisema, “Kutegemea Serikali peke yake kulete maendeleo kutafanya maendeleo kuvia kwani nchi yetu ni kubwa na watu ni wengi na matarajio ni makubwa na gharama zake ni kubwa na mapato ya Serikali hayawezi kukidhi mahitaji yote.”
Ni kweli kuwa hakuna anayeweza kutegemea Serikali akapata maendeleo. Je kuna anayeweza kujiletea maendeleo chini ya Serikali isiyotengeneza mazingira ya kufanya hivyo?
 Ni bahati mbaya kuwa kinachoisumbua Tanzania ni matokeo ya sera za akina Mkapa ambao badala ya kujenga uchumi imara wenye kujitegemea kwa kulinda rasilimali zetu walizigawa kiasi cha kuwaacha Watanzania wakihangaika kana kwamba nchi yao haikujaliwa neema.
Hebu jiulize. Chini ya utawala wa Mkapa na chama chake unaoendelea kuwapo madarakani Tanzania inapoteza mabilioni mangapi kwenye ukwepaji kodi, ufisadi, rushwa, uzururaji na wizi unaofanywa na wakubwa?
Mkapa mwenyewe aliondoka akiwa amejitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira na hajataka kuongelea hili. Je Mkapa anadhani kuwa Watanzania hawajui jinsi alivyolitia hasara Taifa kutokana na kujitwalia Kiwira ambapo Serikali ililazimika kutumia pesa nyingi ya walipa kodi kuununua toka kwake wakati yeye aliupata kwa  bei ya chee sawa na asilimia moja ya thamani ya mradi?
Kwani Watanzania hawajui kuwa Mkapa , familia yake na wakwe zake waliununua mradi kwa Kiwira kwa shilingi  milioni 70 wakati thamani yake wakati ule ilikuwa shilingi trilioni nne?
Je pesa iliyopotea hapa ingeweza kutengeneza ajira ngapi au kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo?
Je kwanini Mkapa aliamua kujitwalia Kiwira chini ya kampuni yake ya kifamilia ya ANBEN yaani Anna and Benjamin?
Jibu hili hapa, “Watu wanaogopa maisha baada ya kustaafu urais, uwaziri, ukurugenzi ukuu kwenye shirika la umma, ndiyo maana vinapokuja vishawishi hawawezi kuhimili.”
Hakuna ubishi kuwa Taifa letu limo msambweni hasa tukizingatia malengo tuliyokuwa tumejiwekea wakati wa kudai uhuru. Ni bahati mbaya kuwa miaka Zaidi ya hamsini tangu kupata uhuru, watu wetu bado wanasumbuliwa na mambo yale yale tuliyodai tungetekeleza baada ya kupata uhuru.
Wakati na baada ya kudai uhuru, Tanzania ilisema wazi kuwa ilikuwa na maadui wakubwa wanne yaani malazi, umaskini, ujinga na dhuluma.
Baada ya kupata uhuru hapo mwaka 1961 Serikali ya awamu ya kwanza chini ya mwanzilishi wake Mwalimu Julius Nyerere ilianza kuhangaika kupambana na maadui tajwa. Kwa kiasi fulani Serikali ya awamu ya kwanza ilifanikiwa sana hasa kutokomeza ujinga, magonjwa, dhuluma ingawa umaskini hakuguswa.
Baada ya kuondoka madarakani kwa mwalimu akiwa anajivunia kuwa na Watanzania wengi wenye kujua kusoma na kuandika, wenye kupata huduma za afya hata kama hazikuwa za kisasa na wenye kuchukia rushwa na dhuluma, waliofuatia waliamua ima kwa upogo au makusudi kuturejesha miaka mia nyuma. Ghafla tulianza kusikia sera za ajabu ajabu kama vile ruksa , baadaye utandawazi na mwisho maisha bora ambavyo vyote havina tija kwa watu wetu.
Je nini chanzo cha haya yote? Chanzo kikuu kinaweza kuwa wanasiasa wenye sura mbili au Zaidi. Tutafafanua.
 Leo ukimsikia rais mstaafu Benjamin Mkapa akitoa nasaha unashangaa alikuwa wapi.
Hivi karibuni alikaririwa akiwa na viongozi wastaafu wengine wa Afrika akilaani rushwa wakati yeye ndiye alikuwa muhimili wake.
 Rejea waziri wake wa fedha Basil Mramba aliyewahi kudai kukwa alito msamaha kwa kampuni ya Alex Stewart kutokana na amri ya Mkapa.
Je kama siyo  kupewa rushwa, Mkapa aliingiliaje shughuli za wizara ya fedha bila kulishwa kitu? Ni bahati mbaya kuwa Mkapa hajawahi kukanusha wala kuzungumzia hili kwa kuhofia kuzuka mengine mengi.
Ukiacha hilo, juzi juzi Mkapa alisikika  akiwahimiza Watanzania walinde rasilimali za Taifa wakati ni Mkapa yule yule aliyezitoa zawadi kwa wawekezaji chini ya dhana yake uchwara ya uwekezaji ambao uligeuka uchukuaji.
Tuliwekeza kwa wingi lakini  tukaibiwa kwa wingi zaidi. Tutatoa mifano.
Wakati Mkapa akijisifu kuvutia wawekezaji, Taifa letu liliingia mikataba mingi ya kijambazi kiasi cha uwekezaji kuwa chanzo cha maafa yetu badala ya nyenzo ya ukombozi.
Ni bahati mbaya sana kuwa Mkapa amesahau yote kiasi cha kudhani wengine nao wamesahau.
Nani hakumbuki Mkapa alivyofikia hata  hatua ya kumnyang’anya uraia Jenerali Ulimwengu kutokana na magazeti yake wakati ule kuanika rushwa na ufisadi wa Serikali ya Mkapa? Nani hakumbuki msemo wake maarufu wa masimango kwa waliompinga au kumwambia ukweli wa “ wana wivu wa kike na ni wasomi uchwara”?
Leo ukimsikia Mkapa unaweza kudhani ni  mzalendo wa kweli wakati siyo. Sura mbili za Mkapa zinanikumbusha sura nyingi za aliyewahi kuwa kiongozi wa juu Edward Lowassa ambaye amejitokeza kuwa mtetezi mkubwa wa wananchi,  wakati ni Lowassa yule yule aliyewadhulumu hao hao wananchi kwa kuingiza kampuni la kijambazi la Richmond lililoiba pesa ya walipa kodi na kulifiilisi shirika lao la umeme la TANESCO kiasi cha mgao na ulanguzi wa umeme kuwa the order of the day. Je huu si undumila kuwili?
Tuhitimishe kwa kumshauri Mkapa kuwa anafikiri na kukumbuka kabla ya kusema. Vinginevyo anazidi kutusimanga kwa kutomchukulia hatua kwa madhambi aliyotutendea yeye na wenzake.
Ushauri wa bure kwa Mkapa na wengine wenye mawazo kama yeye. Hakuna anayependa kutegemea Serikali kumletea maendeleo.
 Pia hakuna anayetaka kuongozwa na Serikali zigo inayomuibia maendeleo kutokana na wakubwa zake kuiba, kutumbua na kutapanya mali na fedha za umma kama alivyofanya kwa kujitwalia mgodi wa umma.

Chanzo: Dira Novemba 25, 2013.

2 comments:

Anonymous said...

Mimi huwa na mashaka makubwa na uwezo wake wa uelewa na kujitambua huyu Bwana wakati anapoongelea Tanzania. Nyakati amaekuwa akiongelea Tanzania kama vile yeye anaishi sayari nyingine vile!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ni kweli Mkapa anaishi kwenye sayari nyingine iitwayo ukwasi hata kama imezungukwa na bahari ya ukapa na umaskini. Anafanya hivyo kwa vile analindwa na Jakaya Kikwete kwa vile lao moja. Mara hii imesahau walivyoshirikiana kutengeneza EPA iliyomsaidia Kikwete kuwahonga wapiga kura?