The Chant of Savant

Friday 11 October 2013

Fungieni wanasiasa kabla ya vyombo vya umbea


Kama kuna upuuzi unataka kumtoa roho Mlevi hata kabla ya kujinyonga si mwingine bali ukandamizaji wa akili na fikra. Heri kukandamizwa mwili kuliko fikra. Heri kuukeketa mwili kuliko ubongo. Yanatoka wapi yote haya?

Mlevi katika harakati za kuusaka umbea si niliangukia kanyaboya linaloitwa sharia ya kudhibiti vyombo vya umbea! La hawla wala quwwata! Kwanini kufungia vyombo vya umbea badala ya wale wanaotenda madudu hadi vikapata cha kuandika? Hivi kosa kati ya kupiga picha mtu aliye uchi na aliyeamua kutembea uchi ni la nani kiakili?
Kwanini kudhibiti vyombo vya umbea badala ya mahabithi wanaosabaisha kuwapo na habari hizo zinazowakera wenye kukereka hadi wakafungia fikra? Uhuru uko wapi kama hatuna hata uhuru wa kuchonga Yarabi?

Kwanza, hii si sharia kitu bali ukandamizaji na mizengwe ya ovyo. Ni uhuni wa kimfumo so to speak. Huwezi kuleta sharia kandamizi halafu tukanyamaza wakati sisi ndiyo hao waathirika.

Mnataka tule polisi? Mbona polisi nao wanakula kwetu? Mnataka wote tugeuke kondoo au kasuku kuimba sifa na utukufu hata tunapoumizwa? Nasema tena kwa kinywa kipana. Mmenoa kweli kweli. Mmechemsha kuunguza na kuungua. Je mwataka wote tuwe praise singers, courtiers, au journo? Mlevi hayumo humo na hataki kuwemo hata kwa kuhongwa ulaji kama wale wa Udhuru na Mzalendoo.

Ukisikia kinachoitwa sharia utashangaa hadi ufe kwa presha ya ugonjwa wa moyo.
Sharia gani ya kukandamiza sauti ya umma? Hamjui kuwa waandishi wa umbea ni the voice of the voiceless?
Inashangaza wasiojua hata maana ya habari au uandishi ni nini kuwafungia wana taaluma. Hebu waulize swali simpo kabisa. Habari ni nini?

Hebu waulize Intro ni nini au hata One husband five wives ni nini? Watakimbilia ndoa za mitala wakati siyo. Hayo tuyaache. Leo nimelewa na kuvuta hadi nahisi kuruka na kumfanyia mtu kitu mbaya.

Yote tisa, leo sipayuki mengi. Kilichotaka kunitapisha hata kuniharishisha si kingine ni kile kipengee kuwa mchoraji maneno (world flinger) eti aandike kila wanachotaka kuficha wanachochukia au kuogopa kuanikwa madudu yao.

Kwani kazi yetu ni U-PR aka Urweyependekezamu siyo? U-PR gani bila kulipwa? Go tell it to the birds.
Leo naongea kibangi bangi ili nieleweke. Nitakaowakwaza wanisamehe kama walivyowasamehe waliochakachua katiba mpya. Leo nimekumbuka upuuzi mwingine uliowahi kupendekezwa na waishiwa kuwa mwandishi wa umbea lazima awe na shahada wakati wao wana za kughushi.

Mwadhani hatujui mambo yenu? Hivi wahusika wanaijua digrii au wanaisikia?

Kuwa na digrii si vibaya. Lakini je nchi yetu inao ubavu wa kuhakikisha kila mwandishi wa habari anakuwa na shahada tena isiyo ya kughushi au kuandikiwa kama wale? Vyuo vyenyewe viko wapi? Pesa yenyewe ya kusomea iko wapi? Mikopo yenyewe mbinde na longo longo tupu ukiachia mbali rushua tena ya ngoni!

Isitoshe hawa waliotaka kila mchonga maneno awe na digrii kama wanazo wengi walizipata wakati wa elimu ya bure ya Mwalimu Mchonga Meno chini ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea wanayoikandia kwa vile ilikuwa haitoi ulaji na nafasi za wizi kwa viongozi wezi.

Hivi kweli siasa yao ya Uhujumaa na Kujimegea inaweza kuzalisha wasomi kiwango cha shahada. Tuache kutiana madole machoni jamani. Mshiko wenyewe tunalipwa kwa mbinde ukiachia mbali mazingira hatarishi ya kufanyia kazi.

Sasa mnaongezea na kutudhibiti na kutufungia! Ai wee! Hamna huruma wallahi.
Najua kuna makanjanja wanaojikomba kwa wafanya madudu ili wapewe mshiko. Huu nao ni ujambazi na uchangudoa wa kimaadili. Huko leo siendi.

Kuna siku yake. Hamjasikia waheshimiwa waliodanganya elimu zao na kughushi vyeti? Hayo tuyaache japo yapo.
Hivi hawa wanaotaka tuandike kwa matashi na matakwa yao wanadhani sisi ni taahira? Kama kuandika rahisi si wajiandikie mambo yao waone kama yatasomwa. Hawa wanaotudhibiti wanadhani hii kaya ni mali yao peke yao? Sisi ni watu, si waramba matapishi wala nepi za kutumiwa na waovu.

Tunakataa. Mlevi pamoja na kwamba wanasema hazinitoshi, naona hawa wamekosa la kufanya na hawataki kuwa wakweli kuwa lengo lao ni kuzuia uhuru wa vyombo vya umbea pamoja na walevi. Kwanini wasitamke wazi kuwa wanataka kuleta ukandamizaji wa kiakili kwa mlango wa nyuma?

Yaani hawa watu hawajatosheka kuona tulivyokwisha kandamizwa kimwili? Hivi kuandika kuwa gabacholi fulani kwa kushirikiana na waziri fulani wameiba pesa ya umma kwenye dili la rada kunahitaji digrii?
Isitoshe kama digrii zingekuwa ni dili na siyo makaratasi ya kutafutia chakula, tungetegemea watawala wetu wangefanya vizuri kuliko waliowatangulia ambao hawakuwa hata na cheti ukiacheia mbali stashahada.

Hivi Mkwawa alikuwa na digrii? Mbona aliwachapa wajerumani au tuseme Mzee Milambo naye alikuwa nayo?

Hao tuwaache. Je Marehemu Mzee Abeid Amani Karume naye alikuwa na hiyo digrii? Nasikia hata mwanae hanayo kama anayo hayo ni mengine. Angalia mzee Karume aliweza kujenga maghorofa ya Michenzani na kutokuwa na digrii kwake wakati wenye nazo wakiuziana nyumba za umma. Ajabu walifuata madaktari tena wa falsafa wakashindwa kuyapaka hata rangi acha kuyaendeleza.

Uhuru wa vyombo vya umbea siyo wa kupimwa na muungu mtu mmoja wala idara ya ulaji iitwayo Maelekezo isiyo na maelekezo zaidi ya makengeza. Kama wahusika wataendelea na longo longo tutakuja kugeuziana kibao. Waache kuipaka matope awamu ya nne au kuifanya ionekane bure kwa wananchi walioichagua kwa vishindo. Au hayo ndiyo maisha bora kwa waachonga maneno? Shame on you all!

Kwa vile waathirika wakubwa wa “madudu” yanayoandikwa na vyombo vya umbea kuwa yalifanywa na wafanya madudu ni wanasiasia, basi wafungieni wao kwanza ili wache kufanya madudu ndiposa mfungie vyombo vya umbea ambavyo kosa lake ni kuona na kusema vilichoona. Pia msiwahukumie walevi kana kwamba hawana akili ya kujua urongo na ukweli ni vipi?

Mlevi Benjamin Constant, (1767-1830) aliwahi kusema, “With newspapers, there is sometimes disorder; without them, there is always slavery.” Mwingine tena Rais Abraham Lincoln aliwahi kusema, “Let the people know the facts, and the country will be safe.” Tafsiri mwenyewe.

The old true soldier never dies. He just fades away. See you guys.

Chanzo: Nipashe Jumamosi Okt., 12, 2013.

No comments: